WATOTO WATATU WAUAWA KWA MAPANGA MKOANI KILIMANJARO
WATOTO watatu wa familia moja, wameuawa kikatili baada ya kukatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao na mlinzi katika nyumba iliyopo eneo la Uru Morange, Moshi Vijinji, mkoani Kilimanjaro kutokana na ugomvi uliokuwepo kati yake na mama wa watoto hao.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fulgence Ngonyani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo Novemba 19, mwaka huu, saa 5:30 usiku.
Alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Abed Mbwambo ambaye ni mlinzi katika nyumba inayomilikiwa na Patrick Tesha, anayeishi jijini Dar es Salaam.
"Mtuhumiwa alifanya unyama huu katika nyumba anayolinda baada ya kutokea ugomvi kati yake na mama wa watoto hao anayeitwa Asha Mussa," alisema.
Akizungumzia mazingira ya tukio hilo, alisema uchunguzi wa awali unaonesha baada ya kutokea ugomvi huo, Mbwambo alimfuata Mussa kwa lengo la kumkata kwa panga lakini mama huyo alikimbia kusikojulikana ili aweze kuyaokoa maisha yake.
Alisema mtuhumiwa baada ya kuona mtu aliyemtaka amekimbia, alikwenda kwenye chumba walichokuwa wamelala watoto hao na kuwakata mapanga hadi kusababisha vifo vyao.
Aliwataja watoto hao kuwa ni Zuhura Ramadhani (8), Abdhala Ramadhani, (5) na Khalid Ramadhani mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane.
0 comments:
Post a Comment