Napenda kuchukua fursa hii kuwapa pole Makamanda wenzangu wote ikiwemo Viongozi wa Chadema Makao Makuu, Viongozi wa Chadema Kanda ya Ziwa, Viongozi wa Chadema Mkoa wa Geita na wapenda Mabadiliko wote Tanzania kufuatia kifo cha Kamanda Alphonse Mawazo kilichotokea leo tarehe 14 Novemba 2015. Kwa kweli nimepokea taarifa ya kifo cha Kamanda Mawazo kwa mshtuko mkubwa hasa kutokana na mazingira ya Kifo chenyewe ambayo inasemekana ameuawa kwa kuvamiwa na kupigwa na Nondo na Mapanga na kusababisha majeraha makubwa yaliyopelekea kutoa uhai wake. Natambua mchango mkubwa aliyotoa Alphonse Mawazo kwa kukijenga chama katika kila kona ya Nchi yetu tangu alipohama CCM na kujiunga na Chadema. Alphonse Mawazo ni kamanda aliyethubutu kuongea ukweli kwenye majukwaa bila uoga. Mchango wake wa kukijenga chama hakuna wa kufananishwa naye kwa vijana wa Chadema.
Rai yangu
Napenda kuishauri Serikali kwa kushirikiana na Vyombo vya dola likiwemo Jeshi la Polisi kufanya Uchunguzi wa kina kujua waliohusika na mauaji haya ya Kinyama ili wachukuliwe hatua kali za Kisheria. Kwani muendelezo huu wa vifo tata vinavyohusisha masuala ya Kisiasa vinajenga chuki kati ya Raia wenye itikadi tofauti za kisiasa hosusani CCM na Vyama vya Upinzani. Pia inasababisha raia kutokuwa na imani na Jeshi la Polisi na kuamaini kwamba linatumika katika kukandamiza demokrasia. Vilevile muendelezo wa matukio haya unaweza kusababisha raia kukosa imani na Serikali iliyo madarakani. Mwisho wa yote vitendo hivi visipochukuliwa hatua stahiki vinaweza kusababisha uvunjifu mkubwa wa amani na kuondoa sifa ya Tanzania kuwa nchi ya amani kama ilivyozoeleka.
Ni matumaini yangu kuwa Serikali itafanya Uchunguzi wa Kina wa tukio hili kwa kuwachukulia hatua kali wahusika ili kuondoa sintofahamu iliyojaa kwenye mawazo ya Watanzania.
Mwenyekiti wa Chadema Washington DC, USA
KALLEY PANDUKIZI
0 comments:
Post a Comment