Na Jovina Bujulu-Maelezo
        Serikali imekanusha                taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa                Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete                kuwa amekomba fedha hazina na kuiacha Serikali bila fungu                lolote.
        Hayo yamesemwa jijini                dare es salaam na Kamishina wa Bajeti kutoka Wizara ya                Fedha Bwa. John Cheyo huku akiwataka wananchi kupuuza                habari hiyo kwani hazina ukweli wowote.
        "Hazina inazo pesa za                kutosha  na tunajivunia kufanya uchaguzi wa mwaka huu,                 kununua mashine za BVR  kwa kutumia pesa za watanzania                bila kutegemea msaada wowote kutoka nje ya nchi  na kutoa                mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka huu" alisema                Bwa. Cheyo.
        Pia aliongeza kuwa                serikali imeendelea kugharamia miradi mbalimbali ya                maendeleo ikiwemo ujenzi wa bomba la gesi ambalo                limekamilika hivi karibuni, vinu vya kuchakata gesi na                ujenzi wa barabara nchini.
        Aliendelea kusema kwamba                mfumo wa serikali wa bajeti unaiwezesha serikali kupanga                vipaumbele vya matumizi kulingana na bajeti ilivyopangwa                ambapo fedha zinazokusanywa kupitia mfuko mkuu wa serikali                ndizo hutumika.
        Bajeti iliyoidhinishwa                na Bunge kwa kipindi cha 2015-2016 ni shilingi Trilioni                22.5 na bajeti hiyo inatengenezewa mpango wa makusanyo na                matumizi kwa kulipia mishahara ya wafanyakazi na miradi                mbalimbali iliyoidhinishwa.
        Pia katika matumizi                mengine bajeti hiyo inalipia chakula cha wanafunzi, mikopo                ya wanafunzi elimu ya juu, ununuzi wa dawa na vifaa tiba                na chakula cha hifadhi ya taifa.
        
0 comments:
Post a Comment