WIZARA ya Ardhi, Nyumba            na Maendeleo ya Makazi imewatahadharisha wananchi kuepuka            kujenga katika maeneo ya wazi na kuvamia viwanja, kwani kazi            ya bomoabomoa ni endelevu. Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es            Salaam na Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Mboza Lwandiko            alipofanya mahojiano na gazeti hili.
        Lwandiko alisema ubomoaji            uliofanyika katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam            hivi karibuni ni ya awali kwani wanaendelea na uhakiki ili            kubaini maeneo mengine yaliyovaamiwa na kujengwa bila kufuata            taratibu.
        Alisema Wizara inasubiri            uhakiki wa maeneo ukamilike na kisha itatangaza maeneo            yanayopaswa kubomolewa, hivyo wananchi wanapaswa kuepuka            kuvamia maeneo ya wazi na kujenga bila kufuata utaratibu ili            kuepuka kuja kubomolewa nyumba zao.
        "Ubomoaji unatia hasara            na unamrudisha mtu nyuma. Tunaomba wananchi wafuate taratibu,            wajenge katika maeneo sahihi," alisema Lwandiko. Aliongeza            kuwa ubomoaji wa nyumba hizo zilizojengwa bila kufuata            taratibu na zile ambazo zipo katika maeneo ya wazi utafanyika            kwa nchi nzima sio kwa Wilaya ya Kinondoni pekee.
        "Wahakiki wanapita katika            maeneo mbalimbali ya nchi na kuhakiki ili kuendelea kubaini            maeneo mengine ili kuhakikisha hakuna uvamizi wala nyumba            zilizojengwa bila kufuata taratibu," alisema Lwandiko.
        Hivi karibuni, Wizara            ikishirikiana na Wilaya ya Kinondoni iliendesha bomoaboamoa            katika wilaya ya Kinondoni ambapo nyumba zaidi ya 20            zilizojengwa bila kufuata taratibu na za watu waliovamia            maeneo ya wazi zilibomolewa.
        
0 comments:
Post a Comment