November 29, 2015

  • MAGUFULI AWAWEKA ROHO JUU VIGOGO WA MASHIRIKA YA UMMA




    MAGUFULI AWAWEKA ROHO JUU VIGOGO WA MASHIRIKA YA UMMA  Rais John Magufuli akisalimiana          na Waziri

    Siku moja baada ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa kuwasimamisha watendaji wa Bandari na TRA, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue amemtaka kila mtendaji mkuu au ofisa masuhuli wa Serikali kujiuliza ni kwa kiasi gani anatekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.



    Alitoa kauli hiyo jana katika taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ikifafanua maagizo ya Rais kuhusu kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika wizara, idara na taasisi za Serikali.
    Juzi, Majaliwa alifanya ziara ya ghafla katika ofisi za Bandari na kuwasimamisha watumishi hao akiwamo Kamishna wa Kodi na Forodha wa TRA, Tiagi Masamaki na Habibu Mponezya wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja ambao wanatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha uliotokana na upotevu wa makontena zaidi ya 349.
    Baadaye, Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade baada ya kubaini 'madudu' katika ofisi za mamlaka hiyo ikiwa ni mwendelezo wa kasi aliyoanza nayo katika ukaguzi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.
    "Rais ameonyesha njia, sasa kwa wakati huu ni vyema kila mtendaji mkuu wa Serikali, ajiulize endapo Rais Magufuli atafika katika eneo langu la kazi, ni kwa kiasi gani atakuta nimetekeleza maagizo yake?" alisema Balozi Sefue.
    Balozi Sefue pia alizungumzia uchapishaji wa kalenda na vitabu vya kumbukumbu huku akihoji umuhimu wa wake.
    "Kila mtendaji mkuu wa Serikali au afisa masuhuli apime mwenyewe kama ni lazima kutengeneza na kuchapisha kalenga na diary na kama ni lazima achapishe kwa kiasi gani?
    "Ni matumizi mabaya ya fedha za umma kwa kila wizara, idara na taasisi za Serikali kuchapisha idadi kubwa ya kalenda na diaries ambazo wakati mwingine hata hazitumiki mpaka mwaka unakwisha," aliongeza Balozi Sefue.
    Kwa hatua zinazochukuliwa ni dhahiri watendaji wakuu wa mashirika, taasisi za umma na wizara mbalimbali watakuwa matumbo joto kwa kuwa hawajui ni lini viongozi hao watatua kwao.
    Hayo yanatokea wakati ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa mapema mwaka huu inaonyesha ukaguzi uliofanywa katika taasisi 176 za Serikali Kuu, halmashauri 163 na mashirika ya umma 109 ulibaini ufisadi katika mishahara hewa na katika miradi ya maendeleo.
    Mashirika ya umma yanayotazamwa ni Shirika la Nyumba (NHC), Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC), Kampuni la Reli Tanzania (TRL), Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara), Tanesco, mifuko ya hifadhi ya jamii; NSSF, PPF, LAPF, PSPF, GEPF, NHIF na mashirika ya hifadhi za taifa kama Tanapa na Ngorongoro pamoja na mamlaka za udhibiti kama Ewura, Sumatra, TCRA, TCAA na SSRA.
    Kutokana na hatua hizo za Rais Magufuli na Majaliwa, Waziri Mkuu wa zamani, Dk Salim Ahmed Salim alisema kasi hiyo inawathibitishia Watanzania kuwa alichokuwa akikisema Dk Magufuli na kukiahidi kipindi cha kampeni ni cha kweli.
    Alisema hayo wakati akizungumza na mwandishi wetu baada ya kufungua mahafali ya 13 ya Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), yaliyofanyika, Dar es Salaam jana.
    "Watumishi wa Serikali hivi sasa wajizatiti kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili waendane na kasi hii ya Dk Magufuli.
    "Nina imani hata hawa wauguzi na madaktari waliohitimu leo (jana), ambao wamepikwa na kuiva, wataweza kuendana na kasi hii," alisema Dk Salim ambaye pia ni mkuu wa chuo hicho.

    Watendaji wazungumza
    Baadhi ya watendaji wa mashirika ya umma waliozungumza jana kwa nyakati tofauti walisema wako tayari kwenda sambamba na kasi ya Rais Magufuli huku wengine wakiahidi kuzungumzia hilo siku tano zijazo.
    Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema Tanesco imejiandaa kufanya kazi na Magufuli kwa kasi aliyoanza nayo.
    Alipoulizwa atawezaje kwenda sambamba na kasi ya Rais Magufuli katikati ya shirika linalokabiliwa na changamoto nyingi, Mramba alisita kutoa ufafanuzi wa swali hilo kuahidi kulitolea majibu hivi karibuni.
    Shirika hilo la umeme limekuwa likikabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya usambazaji wa umeme, mikataba mibovu kwa kampuni zinazouza umeme, kushindwa kukusanya fedha za mauzo ya umeme na uhujumu na mitandao ya wizi wa umeme.
    Alipoulizwa, Msemaji wa Tazara, Conrad Simuchile alitaka atumiwe maswali kwa mtandao ili aweze kujibu kesho kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji, Ronald Phiri.
    Januari mwaka huu, Phiri aliliambia gazeti hili kuwa mamlaka hiyo inaweza kufa endapo nchi washirika hazitawekeza mtaji mkubwa ili kuongeza uzalishaji.Tazara imekuwa na migogoro ya muda mrefu na wafanyakazi wake katika malipo ya mishahara lakini uongozi wake unadai hali hiyo inachagizwa na kushuka kwa uzalishaji. Kuhusu mpango wa kwenda na kasi ya Rais Magufuli ndani ya TRL, Mkuu wa Masoko, Charles Ndenge alisema atatoa ufafanuzi kesho ofisini kwake.
    Mei mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa uchukuzi, Samuel Sitta aliwasimamisha kazi vigogo watano akiwamo Mkurugenzi Mtendaji TRL, Kipallo Kisamfu na watumishi wengine wanne baada ya kupitia uchunguzi wa tuhuma zilizowakabili.
    Watendaji hao walisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za kuhujumu mamlaka hiyo kupitia ununuzi wa mabehewa mabovu 274 ya mizigo, uliofanyika chini ya mkataba kati ya TRL na Kampuni ya M/S Hindusthan, hatua iliyosababisha hasara ya Sh230 bilioni.
    MWANANCHI.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.