HAPA kazi tu! Zile ziara za kushtukiza (bila taarifa) zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano za Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli 'JPM' zimezua kizaazaa mjini hapa, hususan katika Mahakama ya Mwanzo ya Morogoro.
Katika safishasafisha hiyo, baadhi ya makarani walivaa kanga kwa kujifunga juu ya magauni yao kama wapo majumbani mwao kwa lengo la kujikinga na vumbi la muda mrefu ndani ya mashelfu ya mafaili mahakamani hapo.
Karani wa mahakama hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Mwajuma Nyundo alipoulizwa na paparazi wetu kuhusu zoezi la usafi huo, alisema:
"Hapa ni kizaazaa tu! Si unaona kasi ya Rais Magufuli ya sapraizi akitekeleza kauli mbiu yake ya 'Hapa Kazi Tu'. Hivyo katika kutekeleza kauli mbiu hiyo leo viongozi wetu wametupa kazi hii."
Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mfanyakazi mwingine alisema lengo la kuweka ofisi katika hali ya usafi ni kuhofia kuumbuka endapo Magufuli atatia timu ghafla.
"Si unajua Magufuli anavyotikisa nchi kwa sasa. Yaani huwezi kujua muda wala saa atakayoibukia kwako. Tumeamua kufanya usafi ili mahakama iwe safi.
"Sasa hivi hata zile kesi za muda mrefu tunapanga mafaili upya, yakae mbelembele na kuweka lebo ya kutamabulisha kesi ili mashauri hayo yaendelee na kumalizika kwa wakati," alisema mfanyakazi huyo huku akiendelea na shughuli zake.
Mfanyakazi mwingine naye alisema: "Tunatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Magufuli ya 'Hapa Kazi Tu' ili akifanya ziara ya ghafla katika mahakama yetu atukute tuko vizuri."
Baada ya kusikia hayo kutoka kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo, paparazi wetu alibisha hodi kwenye mlango wa chumba cha mashtaka na kuzungumza na kiongozi wa mahakama hiyo, Mheshimiwa Janne Melle ambapo alipoulizwa alisema:
"Na mimi nimepokea maagizo haya kutoka Mahakama ya Wilaya. Halafu bwana mwandishi hizo picha ulizopiga naomba sana ukishazisafisha niletee na mimi nizipeleke wilayani."
KUMBE SI MAHAKAMANI TU
Ukiachia mahakama hiyo, wafanyakazi wengi wa ofisi za serikali mkoani hapa wamebadili tabia ambapo sasa, saa moja asubuhi wapo barabarani kwa lengo la kuwahi muda wa kuingia kazini ambao ni saa moja na nusu tofauti na zamani ambazo kuchelewa kazini ilionekana kama fasheni.
WASEMAVYO MOROGORO
Baadhi ya wakazi wa mjini hapa walipoongea na Ijumaa kuhusu tabia ya Magufuli ya kuzuka maofisini bila taarifa, walipongeza huku wakisema huyo ndiye rais anayetakiwa kwa sasa hapa Bongo.
"Tabia zetu Wabongo tunataka rais kama Magufuli. Unajua sisi ni watu wa kusukumwa sana! Sasa tukimpata rais asiyeweza kusukuma, ndiyo nchi inakwenda mrama. Mimi nampongeza sana Magufuli.
"Kwa staili hii ya Magufuli ya kushtukiza ziara ya maeneo mbalimbali watu watanyooka. Kwa wale wavivu na wazembe makazini lazima waombe po," alisema Jumanne Kihamba, mkazi wa Misufini mjini hapa.
GUMZO LA NCHI NI MAGUFULI
Kwa sasa ukiachia vyombo vya habari kama magazeti, ndani ya mitandao mbalimbali ya kijamii gumzo ni Magufuli. Hiyo yote ni kufuatia hatua yake ya kufanya ziara za kushtukiza ambapo tangu aingie madarakani ameshawashtukiza watumishi wa Wizara ya Fedha (Hazina) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kitendo hicho kimeibua mpaka utani kwenye mitandao ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitunga vituko mbalimbali kuashiria kwamba, Magufuli ni kiboko ya watendaji wazembe serikalini.
0 comments:
Post a Comment