Tunakujali, Tunakuthamini na Pia Tunakupenda!

Showing posts with label Michapo. Show all posts
Showing posts with label Michapo. Show all posts

July 17, 2014

  • Ikulu: Wanaomkosoa Jakaya Kikwete Kuhusu Katiba Hawako Sahihi




    Ikulu: Wanaomkosoa Jakaya Kikwete Kuhusu Katiba Hawako Sahihi
    Ofisi ya Rais imesema kuwa wanaomkosoa Rais Jakaya Kikwete kuhusu msimamo wake katika mchakato wa Katiba Mpya hawako sahihi kwa kuwa ni mlezi na ana haki ya kutoa maoni yake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa.

    Pia, imewataka wasiokuwa wajumbe wa Bunge la Katiba waiache kazi hiyo mikononi mwa Bunge hilo kwa sasa hadi hapo rasimu itakapowasilishwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura ya kuikubali au kuikataa.

    Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu ikiwa ni siku moja baada ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), kutoa tamko zito kwa Rais Jakaya Kikwete ikiishangaa kauli yake ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya Watanzania.

    Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa na taasisi na watu binafsi baada ya kulieleza Bunge la Katiba kuwa kuna baadhi ya mambo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo hayawezekani kutekelezeka, akitoa mfano wa muundo wa Muungano wa serikali tatu, jambo ambalo CCT ilisema jana kuwa alitakiwa alifanye wakati Kamati ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa ikimfuata kumweleza maendeleo ya kazi yao.

    Hata hivyo jana, Rweyemamu aliliambia gazeti hili kuwa: "Kinachoendelea kwa sasa kwa baadhi ya makundi ya kidini kutoa matamko dhidi ya Rais si sahihi, kwa kuwa Rais ni mlezi na ana haki ya kutoa mtazamo wake kama mkuu wa nchi na kama mwanasiasa."

    Alisema kimsingi mchakato huo ni wa kisiasa na Rais ni mwanasiasa, pia ni mkuu wa nchi hivyo ndiye mwenye uwezo wa kutoa ushauri na kutoa angalizo pale inapohitajika, hasa anapoona kuna jambo lisilokuwa sawa, hivyo hakuna haja ya kuendelea kusimama kupinga kile alichokielekeza nje ya Bunge.

  • July 16, 2014

  • JAJI KADURI AJITOA KESI YA MAUAJI YAPROFESA JWANI MWAIKUSA


    JAJI KADURI AJITOA KESI YA MAUAJI YAPROFESA JWANI MWAIKUSA

    Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, amejitoa kusikiliza kesi ya mauaji ya watu watatu akiwemo aliyekuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria, Profesa Jwani Mwaikusa (pichani).

    Jaji Kaduri alijitoa katika kesi hiyo juzi wakati ilipotajwa kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri kwa siku nne mfululizo, akidai ana maslahi nayo.

    Alisema hawezi kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa alisoma na Profesa Mwaikusa na alikuwa naye kila mahali hivyo akisikiliza hawezi kutenda haki. Shauri hilo liliahirishwa hadi kipindi kingine kitakachopangwa.
    Hii ni mara ya pili kwa majaji kujitoa katika kesi hiyo, ambapo Jaji Dk Fauz Twaib alijitoa kwa kuwa aliwahi kufanyakazi na Mwaikusa.
    Washitakiwa katika kesi hiyo ni Joseph Machecho na Jackson Zebedayo, ambao wanadaiwa Julai 13, 2010, katika eneo ya Mbezi Salasala, mtaa wa Mkonde, Dar es Salaam kwa makusudi walimuua Profesa Mwaikusa, Gwamaka Daudi na John Mtui.
    Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mwaka 2010 na baada ya upelelezi kukamilika kesi ilihamishiwa Mahakama Kuu.


  • Mahakama Yamsaka Padri wa Kanisa Katoliki anayekabiliwa na kesi ya Kumlawiti Mtoto wa Miaka 17



    Mahakama Yamsaka Padri wa Kanisa Katoliki anayekabiliwa na kesi ya Kumlawiti Mtoto wa Miaka 17

    Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, limeshindwa kusikiliza rufaa iliyokatwa na upande wa Jamhuri kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru Padri wa Kanisa Katoliki, Sixtus Kimaro aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya kumlawiti mtoto wa miaka 17.
     
    Rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa hivi karibuni lakini hata hivyo padri huyo pamoja na wakili wake hawakufika mahakamani. Upande wa Jamhuri una hoja saba katika rufani hiyo.
     
    Kabla ya kuachiwa huru baada ya kukata rufaa, Padri Kimaro alihukumiwa kifungo cha miaka 35 jela na kulipa faini ya Sh milioni mbili kwa mtoto baada ya kupatikana na hatia.
     
    Kutokana na kushindwa kwa jopo hilo kusikiliza rufani hiyo wiki iliyopita, kwa kutotokea mahakamani hapo padri huyo wala wakili wake, jopo limeagiza upande wa Jamhuri kutoa taarifa ya mwito kuwa anahitajika mahakamani hapo kupitia vyombo vya habari.
     
    Hatua ya kuamriwa kutumika vyombo vya habari kunatokana na wakili wa Serikali, Salum Malick kudai kuwa amepata taarifa kutoka kwa msajili wa mahakama hiyo kuwa, hati ya mwito wa kumtaka afike mahakamani hapo ilipelekwa kwa Kanisa Katoliki.
     
    Alidai kwa mujibu wa taarifa hiyo ya msajili wa mahakama, hati hiyo ilipelekwa Jimbo Kuu la Dar es Salaam lakini waliambiwa na jimbo hilo kuwa Padri Kimaro si mwajiriwa wao na wala hawajui alipo.
     
    Jopo la majaji hao watatu ambao ni Engela Kileo, Steven Bwana na Sauda Mjasiri, limeamrisha mwito huo umtake afike kusikiliza rufaa yake kwa tarehe nyingine itakayopangwa na mahakama hiyo.
     
    Akitoa amri hiyo, Jaji Kileo alisema endapo padri huyo hatafika mahakamani baada ya matangazo hayo, rufaa hiyo itaendelea kusikilizwa upande mmoja.
     
    Katika kesi ya msingi, Padri Kimaro alikuwa anakabiliwa na mashitaka matatu; kumlawiti mtoto wa miaka 17,  shambulio la aibu na kumdhalilisha mtoto huyo.
     
    Ilidaiwa kuwa usiku wa Mei 18 mwaka 2005 katika eneo la Changanyikeni, Dampo, Padri Kimaro alikamatwa na askari aliyekuwa doria, akitenda makosa hayo.
     
    Katika hukumu iliyotolewa Agosti 9, 2006 na aliyekuwa Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo,  Pelagia Khaday,  Padri Kimaro alipatikana na hatia katika makosa yote na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 35 jela na kulipa fidia ya Sh milioni mbili kwa mtoto aliyeathirika na kitendo hicho.
     
    Alikata rufaa Mahakama Kuu iliyosikilizwa na Jaji Robert Makaramba, ambapo aliachiwa huru baada ya Jaji huyo kudai kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.
     
    Hata hivyo upande wa Jamhuri umekata rufaa kupinga uamuzi huo wa kuachiwa huru kwa padri huyo wakiwa na hoja saba ya msingi, ikiwa ni kwamba Jaji aliyesikiliza rufaa hiyo alikosea kisheria na kiusahihi kueleza kuwa hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja kuhusu walichokuwa wakifanya mjibu rufani (padre) na mtoto huyo eneo la Dampo.


  • July 11, 2014

  • SERIKALI KUKOPESHA VIKUNDI 453 VYA VIJANA



    SERIKALI KUKOPESHA VIKUNDI 453 VYA VIJANA
    lindi pixMwenyekiti wa Kikundi cha Waendesha pikipiki Likotwa Manispaa ya Lindi, Bw. Maulid Said Mohamed (kushoto) akimkabidhi Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi risala kuhusu kikundi hicho hivi karibuni Mjini Lindi. Mkurugenzi huyo alitembelea kikundi hicho ili kukagua jinsi kikundi hicho kinavyofanya kazi na jinsi kinavyonufaika na umoja huo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Lindi, Bw. Daniel Kanuse.
    (Picha na: Concilia Niyibitanga)

    ………………………………………………………………………
    Na: Concilia Niyibitanga – Afisa Habari Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
    Serikali inatarajia kukopesha vikundi vya uzalishaji mali vya vijana vipatavyo 453 katika mwaka wa fedha 2014/15 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
    Hayo yamesemwa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana, Bw. James Kajugusi alipotembelea kikundi cha Vijana waendesha pikipiki cha Likotwa kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
    Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa vijana wanajiajiri wenyewe na kuondokana na dhana ya kutegemea kuajiriwa ikizingatiwa kuwa kila mwaka vijana wapatao milioni 1.2 huhitimu vyuo vikuu lakini wanaopata ajira za kuajiriwa ni vijana 200 tu. Amesema Bw. Kajugusi.
    Mikopo inayotolewa kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni njia ya kuwakomboa vijana kwa kuwaongezea mitaji ya kuweza kufanya shughuli za ujasiri na ujasiriamali na hatimaye kujiajiri na kuajiri vijana wenzao.
    Bw. Kajugusi amekipongeza Kikundi cha Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda cha Likotwa kwa juhudi na mafanikio waliofikia hadi sasa kutokana na kuunda kikundi hicho chenye lengo la kuboresha maisha ya waendesha pikipiki hao.
    Aidha, amewataka kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuzingatia maadili mema ili kuimarisha amani na mshikamao katika sehemu wanazoishi na vile vile kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kama vijana wa kulipa kodi.
    Halikadhalika, amekitaka kikundi hicho kuwahamasisha vijana wenzao kushiriki katika shughuli za Mbio za Mwenge wa Uhuru na kuwaeleza manufaa ya mbio hizo na kuwapuuza wanobeza Mwenge kwani wanaoubeza ni watumwa kwani wanaibeza historia ya nchi yao.
    Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Bw. Maulid Said Mohamed amesema kuwa kikundi kina wanachama 13 na pikipiki 2 zinazomilikiwa na kikundi na hadi sasa wameshapatiwa viwanja 6 na Uongozi wa Manispaa kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ya Kikundi.
    Bw. Mohamed amesema kuwa mpaka sasa kikundi kimejiwekea akiba na lengo kuu ni kuanzisha SACCOS kwa ajili ya kuwakopesha vijana kwa riba nafuu na hatimaye kutengeneza ajira kwa vijana wengi zaidi.
    Kikundi cha Waendesha pikipiki Likotwa kina wanachama 13 na kilianzishwa kwa nia ya kusaidiana na kujiinua kiuchumi na kina malengo ya kuanzisha SACCOS kwa ajili ya kukopesha vijana mikopo yenye masharti nafuu.


  • JESHI LA POLISI NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WATAKIWA KUACHA KUKURUPUKA




    JESHI LA POLISI NA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA WATAKIWA KUACHA KUKURUPUKA
    imagesMahmoud Ahmad Arusha
    WAJUMBE wa Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Arusha(RCC) kimelitaka
    Jeshi la Polisi pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kuacha kukurupuka na
    kutoa matamko ya haraka haraka  badala yake wachunguze kwa kina ili kubaini nini
    chanzo cha milipuko ya mabomu yanayoendelea kulipuka kila uchwao Jijini Arusha.Aidha wameshauri kuwepo kwa vikao vinavyoshirikisha wananchi mara kwamara ili kubaini matatizo mbalimbali yanayoweza kudhibitiwa ikiwemoufungaji wa kamera kwa wafanyabiashara wenye biashara zaidi yaSh,milioni 50 hadi 100 na kuwataka kufuatilia kwa ukaribu sehemu mbalimbali zenye mikusanyiko kama zinatumia vifaa vya ukaguzi.

    Hayo yalisemwa jana Jijini hapa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
    Lema , Mbunge wa Arumeru Magh
    aribi ,Goodluck Ole Medeye pamoja na
    Askofu wa KKKT Dayosisi ya Meru, Dk, Paulo Akyoo wakati wakichangia kwenye kikao hicho.
    Lema alisema matukio yanayotokea ya mlipuko wa mabomu Jijini hapa si
    matukio ya masuala ya siasa bali ni matukio yanayodhuru jamii ambayo
    ni muhimu kwa maisha ya kila siku hivyo ni vyema polisi wanapopewa
    taaarifa waifanyie kazi badala ya kuchukulia kuwa taarifa hizo ni za
    kawaida huku milipuko ikiendelea kutokea .
    Alisema ni vyema sasa kila mfanyabiashara kununua kamera za CCTV ili
    kuweza kubaini matukio mbalimbali ya kihalifu pamoja na ulipuaji wa
    mabomu ambao kwa hivi sasa ni tishio kwa Jiji la Arusha pamoja na
    jamii kwa ujumla.
    "Usalama wa wananchi uko wapi kila mara mabomu mabomu na baadhi ya
    wanasiasa wanatumia masuala haya ya mabomu kama ni umaarufu wa kisiasa
    hapana tuache mambo haya tunataka matukio haya yachunguzwe kwa kina
    ili kujua kiini cha tatizo hili ni nini na si kudai masuala ya kisiasa
    au la''
    Naye Askofu, Dk Akyoo alisema ni vyema sasa ile desturi ya ulinzi na
    usalama ngazi ya kata ikarejeshwa na vikao vya mara kwa mara ili
    kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokea mara kwa mara Jijini hapa na
    kutoa rai kwa polisi kuhakikisha wanajenga urafiki na wananchi badala
    ya uadui ili hata taarifa zinapotolewa wazifanyie kazi na kutoa majibu
    sahihi kwa wananchi.
    Naye Medeye alisema kuwa Arusha inastahili kuangalia kwa jicho la pekee
    kuhusu masuala ya milipuko kwani mabomu yakitokea mji unakuwa si
    shwari hivyo ni vyema Kamati ya Ulinzi na Usalama wakachunguza masuala
    haya kwa makini na kutoa majibu sahihi ikiwemo kumshauri Rais Jakaya
    Kikwete juu ya nini kifanyike ili kudhibiti matukio haya kama vile
    tukio la ulipuaji wa bomu lililotokea ubalozi wa Marekani miaka kadhaa
    iliyopita.
    Hata hivyo  Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Edith
    Salvas aliomba ushirikiano kwa wananchi ili kubaini wale wote
    waliohusika na matukio ya ulipuaji wa mabomu Jijini Arusha ilikuweza kudhibiti matukio hayo yalichukuwa kasi hivi sasa.
    Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela aliyekuwa akiongoza kikao
    hicho aliongeza kuwa inabidi vyombo vya ulinzi na usalama vikafanyia
    kazi michango hiyo ili kuja na majibu yatakayoweza kutoa picha kwa
    wananchi ,kikao  hicho kilihudhuriwa na wabunge mbalimbali wa mkoa wa
    Arusha, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Saning'o Ole Telele pamoja na
    wadau mbalimbali wa Jiji la Arusha.


  • WAKIMBIZI SITA WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIEZI SITA AU FAINI YA SHILINGI ELFU THELATHINI KILA MMOJA


    Baadhi ya wakimbizi wa makazi ya Ulyankulu wakitoka kwenye Chumba cha Mahakama ya hakimu mkazi baada ya kusomewa hukumu ya kifungo cha miezi sita jela au kulipa faini ya shilingi ya elfu thelathini kila mmoja
    Na mwandishi wetu Tabora.
    Watu sita ambao ni wakimbizi katika makazi ya Ulyankulu wamehukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha miezi sita au kulipa faini ya shilingi elfu thelathini kila mmoja baada ya kupatikana na makosa ya kutoroka eneo la makazi ya wakimbizi Ulyankulu pamoja na kukutwa wakifanya shughuli za kiuchumi kinyume na kifungu cha makosa ya uhamiaji nchini.
    Watu hao sita ambao walifikishwa kwa mara nyingine katika makahama ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora ambapo wakili wa upande wa mashtaka Bw.Salehe Mgeni aliieleza mahakama kuwa mnamo tarehe 25 machi mwaka huu wakimbizi hao walikamatwa wakiwa wanafanya kazi ndani ya hifadhi ya msitu wa Ugalla katika Tarafa ya Ussoke wilaya ya Urambo, kosa ambalo liliunganishwa na lile na kutoka nje ya eneo la makazi ya Ulyankulu bila kibali cha Mkuu wa makazi.

    Pamoja na kosa hilo la kwanza la kujihusisha na shughuli za kiuchumi kiunyume cha sheria ya Uhamiaji nchini washitakiwa hao sita walikiri makosa hayo mbele ya hakimu mkazi mkoa wa Tabora Bw.Jackton Rushwela na hivyo kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi sita au kulipa faini ya shilingi elfu thelathini kila mmoja.

    Aidha wakimbizi hao waliohukumiwa ni Mapili John,Jeremia Matoli,Kitenge Sayumba,Obed Ndabasigiye,Enock Sayumo na Zarubali Sanzugwimo ambao walikamatwa katika msitu huo wa hifadhi Ulyankulu walikuwa wakifanya shughuli za uchanaji wa mbao.


  • Mary Nagu Mgeni rasmi kongamano la nne la kitaifa la makatibu muhtasi tanzania jijini mwanza leo


    Mary Nagu Mgeni rasmi kongamano la nne la kitaifa la makatibu muhtasi tanzania jijini mwanza leo
     Pichani kushoto ni Waziri wa Uweshaji na Uwekezaji Ofisi ya Waziri Mkuu,Mh.Mary Nagu ambaye ndiye mgeni rasmi wa Kongamano la nne laKitaifa la Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA),akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mshauri wa Masuala ya Kisheria wa TAPSEA wakati alipokuwa akiwasili kwenye ufukwe wa hotel ya Malaika,ambako Kongamano hilo linafanyika leo jijini Mwanza.
    Pichani kushoto ni Waziri wa Uweshaji na Uwekezaji Ofisi ya Waziri Mkuu,Mh.Mary Nagu akizungumza jambo na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mshauri wa Masuala ya Kisheria wa TAPSEA wakati alipokuwa akiwasili kwenye ufukwe wa hotel ya Malaika,ambako Kongamano hilo linafanyika leo jijini Mwanza,pichani kati Mwenyekiti wa Makatibu Muhtasi Tanzania (TAPSEA),Bi.Pilly Mpenda wakiwa wamezungukwa na washirki wengine mbalimbali wakiwasili kwenye ufukwe wa hotel ya Malaika,ambako Kongamano hilo linafanyika leo jijini Mwanza. 
    Ngoma ya asili ya wasukuma ikipigwa kuwakaribisha washiriki mbalimbali waliokuwa wakiendelea kuwasiliasubuhi hii kwenye kongamanno hilo jijini Mwanza
    Washiriki mbalimbali wakiendelea kujiandikisha kwa ajili ya ushiriki wa kongamano hilo
    Mazungumzo ya utaratibu wa washiriki wa Kongamano hilo ukiendelea kuwekwa sawa na waandaaji .

    Waandaji wa Kongamano hilo wakiendelea kujadiliana jambo.



  • KAMATI YA MAJI KING'ONGO DAR WAKAGUA UJENZI WA MRADI WAO WA MAJI ULIOFADHILIWA NA TBL




    KAMATI YA MAJI KING'ONGO DAR WAKAGUA UJENZI WA MRADI WAO WA MAJI ULIOFADHILIWA NA TBL
     Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya MO Resources Limited,Onesmo Sigalla (kulia), akitoa maelezo kwa kwa wajumbe wa Kamati ya Maji ya Mtaa wa King'ongo,  Kata ya Salanga, Kimara, Dar es Salaam,  kuhusu hatua aliyofikia ya usafishaji maji katika ujenzi wa kisima cha maji kilichojengwa kwa msaada wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kamati hiyo iliyokwenda kukagua maendeleo ya mradi huo jana, iliongozwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Demetrius Mapesi (kulia). Wajumbe wengine ni Anna Kibwana (wa pili kulia) na Emannuel Isimbula.PICHA ZOTE NA KAMANDA WA MATUKIO BLOG



  • July 09, 2014

  • WANAFUNZI WAANDAMANA HADI KWA MKUU WA MKOA KWA KUKOSA NAFASI KIDATO CHA TANO MKOANI MBEYA



    WANAFUNZI WAANDAMANA HADI KWA MKUU WA MKOA KWA KUKOSA NAFASI KIDATO CHA TANO MKOANI MBEYA

    WAHITIMU 39 wa kidato cha nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Karobe jijini hapa wakiwa na wazazi wao, jana waliandamana hadi ofisi za Mkuu wa Mkoa ili kujua hatma yao baada Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kushindwa kuwapangia nafasi za kujiunga kidato cha tano licha ya kufanya vizuri katika mitihani yao.
    Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi hao pamoja na wazazi wao, walisema kuwa waliamua kufika ofisi za Mkuu wa Mkoa ili kujua hatima yake, baada ya kuona hawapewi majibu ya kuridhisha kutoka kwa viongozi wa chini yake.Walisema tangu wizara itangaze majina kwa ajili ya kujiunga kidato cha tano wiki mbili zilizopita, wameshangazwa kuona wanafunzi kutoka shule hiyo hawajapangiwa kwa ajili ya kuendelea na masomo katika ngazi hiyo, licha ya kuwa na ufaulu mzuri.

    Wanafunzi hao ambao wamepata alama za daraja la kwanza hadi tatu, hawajui hatima yao kutokana na wizara husika kushindwa kuwapangia shule kwa ajili ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano.

    Nao wazazi ambao waliambatana na watoto wao hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu' (CHADEMA) kwa nia ya kutafuta suluhu ya suala hilo, walisema kuwa tangu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutangaza majina ya wanafunzi waliofaulu kwa ajili ya kidato cha tano na shule walizopangiwa, hakuna majina ya watoto wao.

    Mmoja wa wazazi hao, Lawrance Shimo, alisema baada ya kufuatilia kwa kina ikiwemo kuuliza uongozi wa shule, walibaini kuwa katika shule hiyo hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepangiwa shule kwa ajili ya kuendelea na kidato cha tano, licha ya kuwa na ufaulu wa alama mzuri.


  • WANAFUNZI WATUPWA JELA MIAKA 6 KWA MAUAJI YA MWALIMU WAO MKOANI SINGIDA


    WANAFUNZI WATUPWA JELA MIAKA 6 KWA MAUAJI YA MWALIMU WAO MKOANI SINGIDA

    Vijana wawili waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Chemchem wilayani Mkalama katika Mkoa wa Singida, wamehukumiwa kifungo cha miaka sita kila mmoja baada ya Mahakama kuwatia hatiani kwa kosa la mauaji ya mwalimu wao.

    Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma inayoendesha vikao vyake mjini Singida, ilitoa hukumu hiyo jana.
    Waliohukumiwa ni Shani Mtua na Mohammed Salimu ambao  wakati walipotenda kosa hilo, mwaka 2008,  walikuwa Kidato cha Tatu na walikuwa na umri wa miaka 18 kila mmoja.
    Ilielezwa mahakamani kwamba kulikuwa na washitakiwa wengine wawili katika kesi hiyo; Emmanuel Daud na Michael Msengi, walikufa wakiwa mahabusu  wakisubiri kesi yao kusikilizwa na Mahakama Kuu.
    Hukumu  ilitolewa na Jaji Rehema Mkuye baada ya washitakiwa hao kukiri shitaka la kuua bila kukusudia walilofanya katika Kijiji cha Mpambala,  Tarafa ya Kirumi Wilaya ya Mkalama.
    Awali, Mwanasheria wa Serikali,  Zakaria Elisaria aliyekuwa anasaidiwa na Karen Mrango, alidai mahakamani kwamba washitakiwa walihusika na mauaji ya  Rajabu Idude (49), aliyekuwa Mwalimu wa Nidhamu shuleni hapo. Ilidaiwa walifanya mauaji hayo  Agosti 2008.
    Mwanasheria huyo wa Serikali alidai chanzo cha mauaji hayo ni mshitakiwa wa kwanza , Shani, kupewa barua ya kusimamishwa masomo kwa wiki mbili kutokana na utovu wa nidhamu na kisha akashawishi wenzake watatu kumpiga mwalimu huyo.
    Zakaria alisema wanafunzi hao walimvizia mwalimu huyo katika kichaka cha karibu na shule yao wakampiga ngumi na mateke, kisha wakamjeruhi mwilini kwa kisu alichokuwa nacho mshitakiwa wa kwanza.
    Inadaiwa kutokana na kipigo hicho,  Mwalimu Idude alipiga kelele na mwanawe aliyetajwa kwa jina la Maye Rajabu,  alifika haraka kwenye eneo la tukio, lakini akakuta ameshakufa.
    Wanafunzi hao (washitakiwa) hawakukutwa katika eneo hilo lakini msako ulifanyika usiku huo na wanafunzi wanne walikamatwa. Baada ya kuhojiwa kuanzia ngazi ya mlinzi wa amani kwenye kijiji hicho hadi jana mahakamani, walikiri kosa.
    Kwa upande wake, Wakili wa washitakiwa, kutoka Kampuni ya Uwakili ya  Kim & Company, Raymond Kimu, alimwomba Jaji Mkuye kutoa adhabu nafuu dhidi ya wateja wake, kutokana na kuonesha ushirikiano  wa kutosha tangu siku waliyokamatwa.
    Aidha, alidai washitakiwa walifanya kosa hilo kutokana na kusukumwa na umri mdogo wa utoto. Alidai  ni wakosaji wa mara ya kwanza, wanajutia kosa hilo na kwamba wamekaa jela kwa muda mrefu wa miaka sita, hivyo wamejifunza kutokana na mauaji hayo.
    Akitoa hukumu, Jaji Mkuye alisema hakuna ubishi kwa yote aliyosema wakili wa utetezi. Hata hivyo alisema, anadhani sababu hizo siyo kibali kwa washitakiwa hao kupanga na kutekeleza mauaji dhidi ya mwalimu wao aliyekuwa anasimamia nidhamu.
    "Nadhani kosa walilofanya haliwezi kukubalika kwa  jamii hata kidogo…fujo zimekuwa zikitokea kwenye mashule na vyuo, hata kusababisha vurugu kiasi cha kuathiri utendaji…, kufuatia kosa hili, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka sita jela," alisema Jaji Mkuye.


  • Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.