Na Ali Mohamed
        Serikali imepiga marufuku uuzaji na ununuzi wa                karafuu usio rasmi (vikombe) kuepusha wizi wa karafuu                mashambani na ukataji wa mikarafuu unaofanywa na baadhi ya                watu kutokana na kuzoeleka kwa biashara hiyo. 
        Wakizungumza katika nyakati tofauti Wakuu wa                Wilaya za Unguja na Pemba wamesema hakuna ruhusa kwa mtu                yoyote kuuza au kununua karafuu mbichi au kavu na                atakaebainika kujihusisha na biashara hiyo atashughulikiwa                ipasavyo.
        Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla                alisema tatizo la ununuzi wa karafuu kwa vikombe, wizi na                ukataji wa mikarafuu kwa lengo la kuiba karafuu lipo.
        Alibainisha kuwa Serikali haiwezi kuvumilia makosa                hayo kwa sababu wanaofanya uhalifu huo hawana imani na                Serikali haina imani nao. Alifahamisha kuwa watakaokamatwa                watachukuliwa hatua kwa misingi ya kisheria. 
        Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini 'B'                Haji Makungu Mgongo alisema  Serikali ya Wilaya yake                kupitia kamati za Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa                kushirikiana na Masheha wataendesha zoezi maalumu la                kuwakamata watu wanaojihusisha na masuala hayo na                kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
        Alisema karafuu ni zao la uchumi wa Taifa hivyo                Serikali ya Wilaya yake haitokuwa tayari kuona baadhi ya                watu wakihujumu kwa wizi hasa kukata mkarafuu kwa tamaa ya                kupata maslahi ya muda mfupi.
        Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya                Kaskazini 'A' Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Mohamed Omar                Hamad alisema wizi wa karafuu ambao pia hupelekea kukatwa                matawi na mikarafuu midogo unawakatisha tamaa wakulima.
        Nae Mkuu wa wilaya ya Wete ambae pia ni Kaimu Mkuu                wa Wilaya ya Micheweni Hassan Khatib Hassan alisema                ukataji wa mikarafuu ni uhalifu mkubwa ambapo tatizo hilo                limewahi kuripotiwa ofisini kwake.
        Alishauri kurejeshwa kwa utamaduni wa uchumaji                karafuu kwa kambi ambapo Wakulima na Wafanyabiashara ni                vyema wakajenga kambi katika maeneo wanayochuma karafuu,                kufanya hivyo kutapunguza uhalifu unatokea katika mashamba                yao.
        Wakuu hao wa Wilaya na baadhi ya Masheha                walilishauri Shirika la ZSTC kuanzishwa dawati maalumu la                kufatilia kesi za uhalifu dhidi ya karafuu na mikarafuu                zinazoripotiwa katika vituo vya Polisi.
        Mapema akiwasilisha malalamiko hayo ya wakulima                kuibiwa na kukatiwa mikarafuu yao kwa Wakuu hao wa Wilaya                Mkurugenzi wa Mfuko wa Maedeleo ya Karafuu Ali Suleiman                Mussa alisema matatizo hayo yanawaumiza sana Wakulima.
        Alisema wizi wa karafuu na ukataji wa mikarafuu                unachangiwa na baadhi ya watu wanaonunua karafuu  mbichi                ambapo kisheria ni kosa kwa vile Shirika la   ZSTC ndio                Taasisi pekee  iliyopewa  mamlaka ya kununua na kuuza                karafuu. 
        Alisema Shirika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya                Karafuu umejipanga kufanya usajili wa wakulima wenye                mashamba na wanaokodi karafuu ambapo watapewa vitambulisho                maalumu vya kuwatambua. Alifahamisha kuwa utaratibu huo                utazuia wizi wa karafuu kwa vile wezi hawatokuwa na nafasi                ya kuuza karafuu ZSTC.
        Akizungumzia suala la ubora wa karafuu, Mkurugenzi                huyo amewaomba Wakuu hao wa Wilaya kwa kushirikiana na                Masheha kupiga vita uwanikaji usiozingatia ubora,                (uwanikaji kwenye barabara, sakafu na juu ya bati) na                kuwataka Wakulima kuendelea kutumia majamvi kwa shughuli                za uanikaji.
        Katibu ambae pia ni Mwanasheria wa Shirika la ZSTC                Ali Hilal Vuai aliwakumbusha Wakuu hao wa Wilaya na                Masheha kuwa kukata mikarafuu kwa ajili ya kuiba karafuu                ama kwa matumizi mengine  yoyote ni makosa kwa mujibu wa                sheria namba 2 ya Maendeleo ya Karafuu ya mwaka 2014.
        Alisema sheria hiyo inakataza  kuihujumu mikarafuu                kwa aina yoyote ile na atakaebainika kufanya vitendo hivyo                anapaswa kupelekwa katika vyombo vya sheria.
        Aliwaomba Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati zao za                 ulinzi na usalama za Wilaya, Masheha na Polisi Jamii                 kupambana na vitendo hivyo vya uhalifu dhidi ya biashara                ya zao la karafuu vinavyofanywa na baadhi ya watu                wasiokuwa waaminifu.
        
0 comments:
Post a Comment