Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone amesema hawezi kusononeka kuhusu agizo la Rais John Magufuli la kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Kitaifa, pamoja na kwamba alishazindua.
Akizungumza na Mwananchi, Dk Kone alisema Serikali ya mkoa imepokea kwa mikono miwili agizo na kiongozi wa nchi, licha ya kuwa aliyazindua juzi saa nne asubuhi na kumaliza saa saba mchana, wakati huo agizo la mkuu wa nchi lilikuwa bado halijatolewa.
"Ilipofika saa 11.45 jioni, TACAIDS makao makuu walinipigia simu kwamba maadhimisho haya yamefutwa na hivyo fedha zilizokuwa zitumike, zinunuliwe dawa kwa watu wanaoishi na VVU…Zipo ambazo tayari tumeishazitumia kama kukodi maturubai," alisema Dk Kone.
Juzi Rais Magufuli alitangaza kufuta maadhimisho hayo na kuagiza fedha zilizokuwa zitumike katika maadhimisho hayo, zinunulie dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi na wapewe wahusika.
Wajasiriamali walalamaPamoja na maagizo hayo, wajasiriamali kutoka sehemu mbalimbali za nchi waliofika mjini Singida kutangaza na kuuza bidhaa zao ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo, wamelalamikia agizo la Rais Magufuli wakidai limewasababishia hasara.
Wajasiriamali wa vikundi vya watu wanaoishi na VVU, waliofika mjini Singida na kukodi vibanda vya kuonyesha na kuuza bidhaa zao, kwa nyakati tofauti, walidai kuwa uamuzi huo ungefanywa mapema, ingewasaidia kwa vile wasingefanya maandalizi ya kushiriki maadhimisho hayo.
Mmoja wa wajasiriamali hao, Salome Kwaya anayeishi na VVU tangu mwaka 2000 mkazi wa Wilaya ya Iramba, alisema uamuzi huo umemwachia majonzi kwa madai kuwa alikuwa amendaa bidhaa zake za vyungu na sabuni za maji, kwa ajili ya kuuza kupata fedha za kulimia mashamba.
"Uamuzi ungefanyika mapema kwa sababu maadhimisho haya huwa yanafahamika mapema na kupangiwa bajeti yake…mimi na wenzangu tumepanga katika nyumba za wageni, tumekaa siku moja wala hatujapata wateja, mara tunaambiwa maadhimisho yamefutwa," alisema kwa masikitiko. Kwa upande wake Andrew Venas mkazi wa Dar es Salaam anayeuza dawa za asili, alisema ndoto yake ya kuuza bidhaa yake na kupata kipato, zimeyeyuka ghafla na hivyo hajui atawezaje kurudi nyumbani kwake kwa vile hana nauli.
Muuza dawa za asili kutoka Moshi mjini mkoani Kilimanjaro, John Kanje alisema uamuzi huo wa kushtukiza umemwathiri katika biashara zake.
"Wajasiriamali tumefanya maandalizi ya muda mrefu kuja kutangaza na kuuza bidhaa zetu. Siyo hivyo tu, tuna utamaduni wa kubadilishana uzoefu kipindi cha maadhimisho haya yanayokusanya wajasiriamali kutoka kila kona nchini,uzoefu huo pia tumeukosa," alisema.
Wadau walongaWadau wa masuala ya Ukimwi nchini wameupongeza uamuzi wa Serikali wa kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi na kusema maadhimisho yayo yalikuwa yakiwanufaisha baadhi ya watu, huku walengwa wakiendelea kutaabika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa huduma, Afya na Maendeleo ya watu waishio na virusi vya Ukimwi, Joseph Katto alisema anamuunga mkono Rais, na kwamba uamuzi huo ni jambo jema licha ya ukweli kuwa umekuja ukiwa umechelewa.
"Sisi kama wadau tumefurahishwa sana, kwa sababu imekuwa kama mazoea, kuchezea fedha huku walengwa hawafaidiki….hata hizo sherehe zenyewe zinafanywa na hao viongozi wa Serikali sanasana walengwa tunaambiwa tuandae risala," alisema.
Alisema wapo yatima, wajane na wagonjwa wamelala vitandani wakiwa hawajui hatma yao kutokana na kukosa huduma za dawa za kupunguza hata magonjwa nyemelezi. Aliongeza kusema kuwa vile vile mashirika mengi yanayofanya kazi kuhusiana na masuala ya Ukimwi hayana pesa za kuwawezesha kufikisha elimu hiyo kwa walengwa na kuunga mkono uamuzi wa kuelekeza fedha hizo kwenye kununua dawa na vitendanishi (vifaa)
Alisema waathirika wa Ukimwi wanakaa muda mrefu wakiwa wanakunywa dawa na wanapotaka kupima afya ili kujua maendeleo yao ya kinga na kiwango cha CD4 wanaambiwa hakuna vifaa, vimeisha jambo analosema linawakatisha tamaa kwa kwakuwa wanakosa kujua maendeleo yao.
Akizungumzia hayo, Joan Chamungu, kiongozi wa Mtandao wa kina mama wanaoishi na VVU, alisema badala ya kuendelea na utaratibu wa maadhimisho kwa njia ya sherehe, kila eneo libuni utaratibu wa jinsi ya kupambana na ugonjwa huo kwa kuelimishana.
"Tunaweza kusherehekea kwa staili zingine, kila halmashauri kuhakikisha wanajipanga na kutoa elimu katika eneo lake, lengo liwe kuwa tunapunguza vifo, tunaondoa unyanyapaa kwa kiwango kikubwa," alisema. Ramadhan Masawe kiongozi wa Mtandao wa Vijana wanaoishi na VVU, alisema zipo changamoto nyingi zinazowakabili waathirika wa Ukimwi na kuwa bado walihitaji kuwa na siku ya kukumbushana kuhusu janga hilo.
Alisema taifa linakabiliwa na tatizo la kuongezeka kwa maambukizi mapya hali anayosema huitumia siku hiyo ya maadhimisho kama siku ya kukumbushana ili kuondoa kasi ya maambukizi.
"Nadhani siku ya maadhimisho ni muhimu, watu tuendelee kukumbushana ili kupiga vita maambukizi mapya, tusaidie waliopo kwenye dawa waendelee na wale ambao bado waendelee kujilinda," alisema.
0 comments:
Post a Comment