Hapa Kazi tu ndiyo Tunaweza Kusema!! Novemba 26,2015 asubuhi..Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro anafanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya cha Kambarage katika manispaa ya Shinyanga ili kujionea hali halisi ya huduma zinazoendelea katika kituo hicho.
Kubwa zaidi lililomfikisha hapo asubuhi asubuhi ni kuhusu sakata la muuguzi wa kituo hicho Joseph Nkina kukamatwa na wananchi akiwa na dawa za serikali ikiwemo kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin kinyume na utaratibu.
Baada ya kukutana na uongozi wa kituo hicho na wananchi waliofanikisha kukamatwa kwa muuguzi mkunga wa kituo hicho Joseph Nkila amemwagiza mkurugenzi wa manispaa hiyo kumsimamisha kazi muuguzi huyo kuanzia leo Novemba 26,2015, ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.
"Nimekuja hapa kuona uhalisia wa jambo hili,Kuna ushihidi wa wazi kabisa kuwa muuguzi huyu kweli kaiba dawa za serikali,mbaya zaidi akataka kudanganya kwa kuchukua stakabadhi kutoka kwenye duka la dawa za binadamu (pharmacy), nimekutana na msimamizi wa kituo cha afya Kambarage na mfamasia anayetunza dawa,na kinachoonekana hapa ni uzembe kwenye uongozi kwani dawa zinatoka bila kufuatiliwa kuwa dawa hizo zinafanya nini",amefafanua Matiro.
"Nitamshangaa sana hakimu atayepindisha kesi hii kwani ushahidi uko wazi kabisa kutoka kwa wananchi kwamba amekuwa akijihusisha na wizi kwa muda mrefu na kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu katika kituo hiki cha afya,wananchi wananyimwa dawa,kumbe watu wachache tu wanacheza mchezo huu mchafu wa kuiba dawa",ameeleza Matiro.
"Kila siku wananchi wanalalamika hakuna dawa,lakini tumeangalia stoo tumekuta dawa zipo za kutosha na Shinyanga hatuna tatizo la dawa,dawa moja tu ambayo ni Antibiotic ndiyo haipo,na tumeagiza iletwe",alieleza Matiro. "Cha kusikitisha msimamizi wa kituo hiki Dkt Nassoro Yahya anasema hakuna upotevu wa dawa,huyu naye hatakiwi kuwa hapa kazi imemshinda,nimemwagiza mkurugenzi pia amsimamishe kazi kwani haiwezekani dawa zitoke kwenye kituo bila yeye kufahamu",amesema Matiro.
Katika hatua nyingine Matiro amewashukuru na kuwapongeza wananchi waliofanikisha kumkamata muuguzi huyo na kuahidi kuwapa zawadi kwa kazi nzuri waliyofanya akiwataka wananchi wengine kuendelea kuwafichua watumishi wasiofanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo kwa muuguzi aliyekamatwa,ndugu na marafiki kuacha kutoa vitisho kwa wananchi waliokamata dawa hizo na kufanikisha juhudi za kukamatwa kwa muuguzi huyo kinyume na hapo hatua kali za kisheria zitachukulia dhidi yao.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog SOMA HAPA HABARI YA JINSI MUUGUZI HUYO ALIVYOKAMATWA
0 comments:
Post a Comment