Mfuko                wa Changamoto za Milenia (MCC) wa Marekani umeonya kuwa                hali ya kisiasa Zanzibar na tukio la hivi karibuni la watu                kukamatwa chini ya sheria mpya ya uhalifu mtandaoni                yanaweza kuathiri vigezo vya kuiwezesha Tanzania kupata                msaada.
                Katika                barua ya MCC ya Novemba 19, ambayo imesainiwa na Naibu                Makamu wa Rais wa Idara ya Operesheni ya Miradi kwa                Afrika, Jonathan O. Bloom kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara                ya Fedha, Dk. Servacius Likwelile, mfuko huo umetaka                maelezo kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar pamoja na                ufafanuzi wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni.
                "MCC                  inashukuru kwa uongozi na dhamira yako wakati wa                  mchakato mzima wa maendeleo ya mradi huu. Msaada wa dola                  milioni 472 (ambazo ni zaidi ya Sh trilioni moja), una                  nafasi kubwa ya kusaidia kuleta mageuzi katika sekta ya                  nishati na kuwaunganisha maelfu ya watu katika gridi.
                "Lakini                  mgogoro wa Zanzibar na ukamataji watu wa hivi karibuni                  kupitia sheria mpya ya uhalifu mtandaoni umetutia                  wasiwasi.
                "Kama                  ujuavyo, mataifa washirika wa MCC wanapaswa kuendeleza                  na kuonyesha dhamira ya utawala bora, ambayo ni pamoja                  na kufuata misingi ya demokrasia na kulinda uhuru wa                  kutoa mawazo. 
                "Hata                  hivyo, matukio ya karibuni yanaifanya MCC na wadau wetu                  kujawa na maswali kuhusu dhamira hiyo," inasomeka                barua hiyo ya MCC iliyosainiwa na Bloom.
                Kwa                mujibu wa barua hiyo, MCC inafuatilia kwa karibu nyendo za                Serikali katika ushughulikiaji wa masuala hayo ya utawala                bora, hasa kipindi hiki kuelekea mkutano wa mwezi ujao wa                bodi ya mfuko huo.
                "Utatuzi                  wa mgogoro wa Zanzibar kwa namna ya kuridhisha pande                  zote husika na haja ya kuiona Serikali ikifafanua                  hadharani nia yake na sheria ya uhalifu wa mtandaoni,                  kama vile kuchapisha utekelezaji wa kanuni zinazoakisi                  mchango wa mdau na kuonyesha dhamira ya kuendelea                  kulinda uhuru wa kutoa maoni, kutaisaidia MCC                  kuitathimini Tanzania kwa namna chanya juu ya kuendelea                  kwa dhamira yake ya kutimiza sharti la kufuzu kupata                  misaada," ilisema barua hiyo.
                Barua                hiyo ilimalizia kwa kusema: "Wasiwasi huu ni kikwazo                  cha mipango yetu ya ushirika. Tunaamini utashughulikia                  wasiwasi huu ipasavyo na tunatarajia kupata jibu kutoka                  kwako."
                Alipotafutwa                Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk. Likwelile,                hakupatikana na hata alipotafutwa kwa njia ya simu                hakupokea.
                Pamoja                na juhudi hizo, pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu                hakujibu, ambapo alipotafutwa Msemaji wa Wizara ya Fedha,                Ingiahedi Mduma, kuhusu barua hiyo ya MCC, alisema hana                taarifa na hajaiona.
                "Sina                  taarifa na wala sijaiona barua hiyo, hivyo siwezi kusema                  chochote labda mpaka nitakapoongea na bosi aniambie kama                  amepokea barua hiyo," alisema Mduma.
                Mwanzoni                mwa Oktoba mwaka huu, Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa                nchini Marekani kuhudhuria shughuli za Baraza Kuu la Umoja                wa Mataifa (UN), alikutana na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana                J. Hyde na watumishi waandamizi, akiwamo Makamu wa Rais wa                Operesheni za mfuko huo, Kamran Khan.
                Katika                mkutano huo, MCC ilitangaza kuwa Tanzania imetimiza                masharti yote ya kupatiwa awamu ya pili ya fedha za                maendeleo kutoka katika mfuko huo, kuanzia mwakani, zaidi                ya dola za Marekani milioni 472.8, sawa na zaidi ya Sh                trilioni moja za Tanzania.
                Katika                mkutano huo, Rais mstaafu Kikwete, aliambatana na ujumbe                wa maofisa kadhaa akiwamo Waziri wa Fedha wa Zanzibar,                Yusuf Omar Mzee.
                Katika                awamu ya kwanza ya fedha za MCC, Tanzania ilipata dola za                Marekani milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46).
                Kama                MCC wataridhika na maelezo ya Serikali kupitia Wizara ya                Fedha, Tanzania itakuwa imepata jumla ya Sh trilioni 2.45                kwa awamu zote mbili kwa ajili ya miradi ya maendeleo                katika kipindi cha miaka 10.
                Awamu                ya kwanza ya fedha hizo zilitumika kujenga Barabara za                Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo- Songea-                Mbinga.
                                Desemba                10, mwaka jana, Marekani pia ilibainisha hatua ya uamuzi                wa utolewaji wa fedha za awamu ya pili za MCC utategemea                hatua zitakazochukuliwa na Serikali kuhusu sakata la                uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 200 katika akaunti ya                Tegeta Escrow.
                Uamuzi                huo wa Marekani ambayo inafadhili miradi mingi ya                mabilioni ya fedha nchini, ulionekana kama mtihani  wa                pili kwa Rais mstaafu Kikwete, baada ya ule wa maazimio ya                Bunge yaliyotaka viongozi wakiwamo mawaziri waliotajwa                katika kashfa hiyo kuwajibishwa.
                Waliowajibishwa                na Rais Kikwete ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini,                Profesa, Sospeter Muhongo na aliyekuwa Waziri wa Ardhi,                Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
                Wengine                ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,                Eliakimu Maswi na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,                Jaji Frederick Werema.
                Chanzo:                Mtanzania 
         

0 comments:
Post a Comment