Wataalamu wa afya wameonya kuhusu matumizi holela ya mafuta yanayopakwa mwilini kama dawa za kuzuia mbu, kwa kuwa zinaweza kuwa na madhara kwa baadhi ya watumiaji.
Kwa nyakati tofauti wataalamu hao wa masuala ya afya wamesema dawa hizo ambazo zimekuwa zikitumika kupaka mwilini kama mafuta na matumizi yake kuongezeka zaidi wakati huu kutokana na tishio la homa ya Dengue, zinaweza kuwa na madhara kwa sababu mbalimbali.
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa Homa ya dengue katika Hospitali ya Mwananyamala, Mrisho Rupinda alisema jana kwamba watumiaji wanapoona madhara ya aina yoyote wanatakiwa kuchukua hadhari hasa kwa wenye mzio (alerge).
Alisema kwa kuwa dawa hizo ni kemikali zinahitaji utaratibu na kwa watoto inahitaji uangalifu mkubwa ambapo ni vyema kuwavalisha nguo ndefu na iwapo kuna mbu wengi dawa hizo ni vyema zikapakwa juu ya nguo.
Alisema kwa kuwa ngozi za watoto bado ni changa na laini si vyema kutumia dawa hizo moja kwa moja kwani zimetengenezwa kwa kemikali zinazoweza kuwa siyo salama kwa ngozi za watoto.
Alisema wenye vidonda wanatakiwa kujihadhari kwa kuhakikisha dawa hizo hazigusi vidonda au sehemu zenye michubuko na inapobidi wapake juu ya nguo, kwa wanawake wavaa nguo fupi ameshauri kuvaa soksi kisha kupaka dawa hiyo juu yake kwa kuwa si lazima iguse ngozi.
"Madhara yanaweza kutokea kwa baadhi ya watu hasa wenye alerge (mzio) na wenye matatizo ya ngozi, ni vyema kuchukua tahadhari. Madhara yanaweza kutokea kwa yeyote na wakati wowote," alisema Dk Rupita.
Mtaalamu wa afya ambaye ni Ofisa wa Taaluma na Udhibiti wa Magonjwa wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Grace Saguti ameonya matumizi yasiyo sahihi ya dawa hizo za kuzuia mbu mwilini na kusema watumiaji wanatakiwa kupaka kwa kufuata taratibu na si kutumia kiholela.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Dk. Saguti alisema japokuwa suala hili ni la kitaalamu zaidi watu wanapaswa kuwa makini kuhusu namna wanavyotumia vizuizi hivyo vya mbu katika miili yao.
"Vizuizi hivyo vinaweza kuwa na reaction kutokana na mwili wa mtu. Sitalizungumzia kwa undani zaidi kwa kuwa kila kitu kina madhara yake lakini watu wasikimbilie kutumia dawa hizo bila kupata ushauri. Ninajua iwapo mtu atakuwa na vidonda si vyema kutumia dawa hizo bila kufuata maelekezo kwa usahihi," alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Saguti, suala hilo la matumizi linahitaji pia tahadhari na kufuata maelekezo ikiwamo kuhakikisha mwili unakuwa safi wakati wa kupaka dawa hizo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza kwenye ngozi.
Matumizi ya dawa hizo yameshika kasi katika maeneo mengi nchini kwa sasa hasa kutokana na tishio la ugonjwa wa dengue unaoenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae ambao mara nyingi huuma wakati wa mchana.
0 comments:
Post a Comment