KIONGOZI              wa Kanisa la Katoliki Duniani, Papa Francis, amewasili              nchini Kenya jana jioni huku akitoa baraka kwa nchi hiyo kwa              lugha ya Kiswahili.
          Baada              ya hotuba yake, Papa Francis, alimaliza kwa kusema "Mungu              Ibariki Kenya" jambo lililowafanya watu waliokuwa katika              ukumbi wa Ikulu ya Nairobi kulipuka kwa furaha.
          Katika              ziara yake hiyo ya ya siku tatu nchini Kenya, alipokewa na              mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta, ambapo moja ya mambo ya              kukumbukwa ni ujumbe alioutoa kwa Kiswahili akilibariki              taifa hilo baada ya kulihutubia taifa Ikulu jijini Nairobi.
          Pamoja              na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa amani, maridhiano,              kusameheana na uponyaji katika taifa hilo lililogawanyika              kwa misingi ya ukabila.
          PAPA                AHUTUBIA TAIFA
          Baada              ya mazungumzo yao Ikulu, Rais Kenyatta akagusia kwamba leo              ni siku ya maombi ya taifa la Kenya na baadaye akamkaribisha              Papa Francis kulihutubia taifa.
          Papa              alianza kutoa hotuba akishukuru kwa makaribisho mema kwenye              ziara yake ya kwanza Afrika.
          Kuhusu              matarajio ya ziara yake, Papa alisema Kenya ina vijana              wengi, na hivyo katika siku zake za kuwa humo anasubiri kwa              hamu kubwa kukutana na kuzungumza nao na kuwapa matumaini              katika ndoto zao za siku za usoni.
          Aidha              alisema Kenya ni taifa change, linalokua na lenye jamii              mseto na ambalo limekuwa likitekeleza jukumu muhimu katika              kanda hii na kupitia changamoto nyingi katika uundaji wa              demokrasia kama ilivyo kwa mataifa mengi Afrika.
          Akihimiza              amani na maridhiano Papa Francis alisema: "Jamii zetu              zinapoendelea kukumbwa na migawanyiko ya kikabila, kidini au              kiuchumi, binadamu wote wenye nia njema huitwa kufanyia kazi              maridhiano, msamaha na uponyaji.
          "Yote              ni katika juhudi za kuunda mfumo wa demokrasia, kuimarisha              utangamano na uwiano, kuvumiliana na kuheshimiana, lengo              kutenda mema linapaswa kuwa kipaumbele kikuu."
          Aidha              alisema kwamba historia inaonyesha kuwa ghasia, mizozo na              ugaidi huchochewa na kuogopana na kutoaminiana ambako              husababishwa na umaskini na kupoteza matumaini.
          "Vita              dhidi ya maadui wa amani na ustawi vinapaswa kuendeshwa na              wanaume na wanawake wanaoamini katika kushadadia, maadili              makuu ya kidini na kisiasa ambayo yalisababisha kuasisiwa              kwa taifa," alisema.
          Akizungumzia              umuhimu wa utunzaji wa mazingira, Papa Francis alisema:              "Kenya imebarikiwa si tu na umaridadi, katika milima, mito              na maziwa, misitu, nyika na maeneo kame, bali pia katika              utajiri wa maliasili.
          "Wakenya              wamethamini zawadi hizi kutoka kwa Mungu na wanajulikana kwa              utamaduni wao wa kuhifadhi mazingira. Mgogoro wa kimazingira              unaoikumba dunia kwa sasa unahitaji kutambua zaidi uhusiano              kati ya binadamu na maumbile."
          Alihimiza              taifa kuwajali masikini, ndoto za vijana, na kugawana vyema              maliasili na nguvu kazi ambazo Mungu ameibariki Kenya na              ameahidi kuendelea kwa juhudi za Kanisa Katoliki, kupitia              kazi zake za elimu na kusaidia jamii, kutoa mchango katika              hilo.
          Akimalizia              hotuba yake kabla ya kuondoka katika ukumbi wa Ikulu, baada              ya kusalimiana na baadhi ya wageni waalikwa alisema:              "Nawashukuru tena kwa kunikaribisha vyema, na kwenu na              familia zenu, na watu wote wa Kenya, ziwe baraka tele za              Mwenyezi Mungu." Kisha akamalizia kwa Kiswahili akisema:              "Mungu Ibariki Kenya".
          Baada              ya hotuba hiyo, Papa alikaribishwa katika dhifa ya kitaifa              iliyofanyika katika hema kubwa la mviringo eneo la Milimani,              Nairobi, ambako ni makazi ya rais na ofisi yake.
          NDEGE                ILIYOMBEBA
          Awali              ndege iliyombeba Papa ya Shirika la Ndege la Italia,              Alitalia, ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo              Kenyatta (JKIA) saa 10. 33 jioni.
          Viongozi              wa Kanisa la Katoliki nchini humo, wanasiasa na mabalozi              wakiongozwa na Rais Kenyatta walionekana wamejiandaa              kumlaki.
          Waandishi              wa habari walioambatana na Papa walitangulia dakika 17              baadaye, kabla ya yeye mwenyewe kuchomoza kutoka katika              ndege hiyo dakika mbili zilizofuata.
          Papa              alilakiwa kwa shangwe na nderemo huku kwaya ya kumkaribisha              ikitumbuiza, na alianza kusalimiana na Rais Kenyatta kabla              ya kutembezwa kutambulishwa na kushuhudia vikundi mbalimbali              vya utamaduni.
          Kwa              mujibu wa Idara ya Habari ya Serikali ya Kenya, Papa Francis              akiwa JKIA aliandika maneno haya: "Na maombi na shukrani kwa              kuwatunza wasafiri."
          Papa              baada ya kupokewa kwa heshima zote za kitaifa uwanjani hapo,              msafara ulianza kuelekea Ikulu ya Nairobi ukipita mitaani,              ambako maelfu ya Wakenya walijipanga pembeni mwa barabara              kumsalimia, huku wengine wakipeperusha bendera na mabango ya              kumkaribisha yakiwamo yenye picha yake.
          APIGIWA                MIZINGA
          Alipokewa              Ikulu na Rais Kenyatta, ambako wimbo wa taifa ulipigwa kabla              ya mizinga 21 kupigwa kwa heshima yake kama mkuu wa taifa la              Vatican.
          Baadaye              Papa Francis alikagua gwaride la heshima kabla ya kwenda              kuonana na Rais Kenyatta na baadhi ya wageni waalikwa na              baadaye kulihutubuia taifa akiwa Ikulu.
          Rais              Kenyatta pia alimtambulisha Papa kwa wajumbe wa baraza lake              la mawaziri akiwamo naibu wake William Ruto kabla ya dhifa              ya kitaifa aliyomwandalia.
          Kabla              ya mazungumzo Ikulu, Papa Francis, ambaye anajulikana kwa              uhimizaji, utunzaji wa mazingira, pia alipanda mti              akisaidiwa na Rais Kenyatta.
          Mbele              ya hema kulikuwa na kiti ambacho Papa alikaa pembeni ya Rais              Kenyatta.
          Wakati              Papa akitarajia kukutana na watu wa kawaida wakati wa ziara              yake Kangemi kesho na kukutana na vijana huko Kasarani,              mkutano wake wa kwanza ulikuwa jana na tabaka la watawala na              vigogo wa Kenya.
          MARAIS                WASTAAFU
          Marais              wastaafu Daniel arap Moi na Mwai Kibaki, Naibu Rais William              Ruto na Mke wa Rais, Margaret Kenyatta walikuwapo viti vya              mbele wakati wa dhifa ya taifa wakiwa mkabala na Papa na              Rais Kenyatta.
          Pembeni              yao walikuwepo maspika Justin Muturi na Ekwee Ethuro na wake              zao. Wengine katika mstari wa mbele walikuwepo Jaji Mkuu              Willy Mutunga, Waziri wa Mambo ya Ndani Joseph Nkaissery,              Makamu wa Rais wa zamani Moody Awori.
          Wengine              ni Musalia Mudavadi, Kiongozi wa Wachache katika Seneti              Moses Wetang'ula, viongozi wa muungano wa Cord, Kalonzo              Musyoka na Raila Odinga na mkewe Ida pia walitarajia              kuhudhuria dhifa hiyo.
          Majaji              wa mahakama ya juu, wabunge, majaji na wengineo pia              walitarajia kuwapo jana usiku.
          Papa              leo asubuhi anatarajia kuongoza ibada itakayohudhuriwa na              watu milioni 1.4 kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Nairobi.
          Awali              kutokana na shauku ya kuwasili kwake nchini Kenya, mapema              jana Papa Francis alirusha ujumbe wa baraka kwa Wakenya              kwenye mtandao wa jamii.
          PAPA                ARUSHA UJUMBE KWA KISWAHILI
          Katika              ujumbe wake alioutuma kwenye ukurasa wake wa Twitter,              @Pontifex the Papa aliandika kwa Kiswahili na Kiingereza              maneno: "Mungu Ibariki Kenya!"
          Aliutuma              ujumbe huo jana mchana wakati akiwa safarini kutoka Rome,              Italia kuelekea Nairobi.
          Papa              pia atazuru Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) ambayo              imekumbwa na machafuko baina ya Wakristo na Waislamu.
          "Naenda              nikiwa na furaha ya kuonana na Wakenya, Waganda na ndugu              zetu katika Afrika ya Kati," aliwaambia waandishi wa habari              katika ndege yake.
          Pia              alipuuza wasiwasi wa usalama wake kwa kutania: "Ninaogopa              zaidi mbu kuliko vita."
          Nairobi,              linakuwa jiji la kwanza la Afrika, ambalo Papa huyo mwenye              umri wa miaka 78 ametua tangu akabidhiwe uongozi wa kanisa              miaka miwili iliyopita.
          Anaitumia              ziara yake ya 11 nje ya makao makuu ya kanisa hilo, Vatican              kutoa jumla ya hotuba 19 kuhusu amani, haki za kijamii,              utunzaji wa mazingira na majadiliano ya imani tofauti nchini              Kenya, Uganda na CAR.
          WASIOMJUA                MUNGU WAFUNGUA KESI
          Wakati              huo huo, muungano wa watu wasiotambua uwepo wa Mungu,              umewasilisha malalamiko yao mahakamani kupinga hatua ya              Serikali ya Kenya kuitangaza Alhamisi (leo) kuwa siku ya              mapumziko ya taifa.
          Kwa              mujibu wa mwenyekiti wa muungano huo, Harrison Mumia,              wanaitaka mahakama itupilie mbali tangazo lililochapishwa              katika gazeti la Serikali kuwa Alhamisi itakuwa siku ya              mapumziko.
          Juzi              Rais Uhuru Kenyatta aliweka bayana kuwa Novemba 26 (leo) iwe              mapumziko ya taifa kwa kuomba na kumwabudu Mungu wakati wa              ziara ya Papa.
        
0 comments:
Post a Comment