November 01, 2015

  • ASKARI AJIMALIZA KWA RISASI IRINGA



    ASKARI AJIMALIZA KWA RISASI IRINGA


    Askari mpelelezi wa kikosi cha kupambana na ujambazi wa kutumia silaha mkoani Iringa, Paschal Shila, anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi shingoni.



    Shila aliyekuwa anafanya kazi Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, alifariki papo hapo, akiwa ndani ya jengo bovu lililo jirani na kituo cha polisi cha mkoa.

    Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi (pichani), alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa askari huyo mwenye namba za usajili G343 D/C alijiua kwa bunduki ya  SMG, juzi kati ya saa 9 na 10 alasiri.

    Kadhalika  alidaiwa kutuma ujumbe wa simu kwa mkewe na kumtaka awalinde watoto wake, kwani anawapenda mno.

    Kamanda alisema kabla ya kujiua, alikwenda kwenye ghala la  silaha saa 6.00 mchana ili kuchukua bunduki  na wakati huo alikuwa anaongea na simu akionyesha kuwa anawahi tukio la ujambazi.

     "Alikuwa anazungumza kana kwamba ana dharura ya kuwahi tukio hivyo kuchukua silaha ili awahi kufika Ifunda lakini baadaye ilibainika kuwa hapakuwepo na ujambazi," alisema Kamanda. 

    Alieleza kuwa baada ya kufanikiwa kuchukua silaha huenda aliitumia kujimaliza.

    Akizungumzia ujumbe aliotuma nyumbani, alisema baada ya mkewe kuupokea alikwenda kazini kwake kuulizia sababu za kutoa maagizo hayo.

    "Alipowaeleza askari wenzake walianza kumtafuta na kuangalia kwenye kamera za kurekodi matukio (CCTV) na kumuona kuwa aliingia kwenye jengo bovu baada ya kutoka kwenye ghala la silaha." Kamanda alisema walimfuatilia kwenye jengo hilo na kukuta amefariki.

    Aliongeza kuwa mwili wa Shila utasafirishwa leo kupelekwa Kyela mkoani Mbeya kwa mazishi na kwamba polisi inaendelea na uchunguzi kubaini chazo cha kifo hicho.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.