![]()  |             
| Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam kujibu madai ya TEWUTA. | 
KAMPUNI ya Simu                Tanzania (TTCL) imepinga madai yaliyotolewa na Chama cha                Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano                Tanzania (TEWUTA) jana dhidi ya Menejimenti na Bodi ya                Wakurugenzi ya TTCL na kufafanua kuwa madai hayo si ya                kweli zaidi ya upotoshaji wenye nia ovu ya kufanikisha                malengo binafsi na kutaka kuikwamisha jitihada za TTCL                katika maendeleo.
        Meneja Uhusiano wa                TTCL, Nicodemus Mushi akizungumza na vyombo vya habari leo                Makao Makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam alisema                madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya                Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL hayana ukweli                wowote bali wahusika walilenga kuupotosha umma.
        "Menejimenti ya                Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), inapenda kuujulisha Umma                kuwa, madai yaliyotolewa na Chama cha TEWUTA dhidi ya                Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL si sahihi. Hoja                hizo zimejikita katika upotoshaji wenye nia ovu ya                kufanikisha malengo binafsi ya wahusika na kukwamisha                jitihada kubwa zinazofanywa na Wizara ya Mawasiliano,                Sayansi na Teknolojia, Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na                Wafanyakazi wa TTCL wenye nia na malengo ya kutekeleza                mpango mkakakti wa kuiboresha na kuiimarisha Kampuni ya                Simu Tanzania.
        Akifafanua zaidi                Meneja Uhusiano huyo wa TTCL alisema mwaka 2007 Kampuni ya                Simu Tanzania ilifanya mabadiliko ya Muundo wa Kampuni ili                kuendana na hali ya soko la Ushindani katika sekta ya                mawasiliano na Muundo uliopo sasa ni ule uliopitishwa na                kuanza Kutumika mwaka 2007 baada ya kuidhinishwa na                kupitishwa na Bodi ya Wakurugenzi.
        Alisema menejimenti                mpya ya TTCL iliyoanza kazi Februari 2013 iliainisha                changamoto mbalimbali za kibiashara na kutengeneza Mpango                Mkakati utakaoletab mabadiliko ya kibiashara na kuongeza                tija, huku ikizingatia mabadiliko ya Kibiashara na                ushindani wa soko katika  sekta ya mawasiliano,                Menejimenti iliomba na kupata kibali cha Bodi ya                Wakurugenzi wa TTCL kumtafuta Mshauri mwelekezi kwa njia                ya Zabuni ili kupitia na Kushauri juu ya Muundo Mpya wa                Kampuni utakaoendana na Mahitaji ya Kibiashara na kuleta                ufanisi.
        Aliongeza kuwa matokeo                ya Kazi ya Mshauri mwelekezi yamelenga kubadilisha muundo                wa Kampuni, Muundo wa Mishahara na Muundo wa utumishi.                Mpango huu wa Mabadiliko ya Kibiashara unategemewa                kukamilika katika kipindi cha mwaka 2016. Aidha alifafanua                kuwa muundo wa mishahara unaotumika hivi sasa ni ule                uliopitishwa Mwaka 2007 baada ya Kubadilika kwa Muundo wa                Kampuni kama ulivyoidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa                TTCL.
        "...Mfumo huu uliiweka                TTCL katika nafasi ya kukabiliana na soko la ajira                kimaslahi. Mfumo huu wa Mishahara ulizingatia pia matakwa                ya kisheria ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na                Mahusiano Kazini Namba 6/2004 zimeainishwa aina tatu za                Mikataba ya Ajira. Yaani: Mkataba wa Ajira usiokuwa na                Muda Maalumu (Unspecified period of time), Mkataba wa                Ajira wa Muda Maalum (Fixed Employment contracts) na pia                Mkataba wa Ajira wa kazi Maalum (Special Task)..."
        "...Hivyo Muundo wa                Mishahara uliopitishwa mwaka 2007 uliainisha madaraja ya                malipo na viwango husika ikiainisha aina ya mkabata,                Mkataba wa Ajira usiokuwa na Muda Maalum na Mkataba wa                Ajira wa Muda Maalum. Katika muundo huu madaraja na ngazi                za Mishahara zimegawanyika katika ngazi Kumi (10) kuanzia                TTCL 1 (Ikiwa ndio Kiwango cha Juu) hadi TTCL 10 (Ikiwa                ndio kiwango kidogo) Muundo huu uko wazi na ndio                unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni                ya Simu Tanzania. Hakuna ulipaji wa mishahara (Payroll)                yoyote ya Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa,"                alifafanua Meneja Uhusiano huyo katika taarifa yake.
        ![]()  |             
| Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Bwana Mushi akifafanua masuala mbalimbali katika mkutano huo na vyombo vya habari. | 
Akizungumzia kuhusu                Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL alisema imekuwa na mchango                mkubwa katika kusukuma maendeleo ya TTCL chini ya                uenyekiti wa Dk. Enos Bukuku na baadae chini ya Mwenyekiti                wa muda Jaji Joseph Sinde Warioba.
        Aliyataja baadhi ya                mambo mengi yaliofanywa na Bodi hiyo kuwa ni pamoja na                kuondoka kwa Mbia Mwenza Bharti Airtel na pia kuishauri                Serikali juu ya umuhimu wa kuondoka kwa Bharti Airtel                ndani ya TTCL ili kuwezesha juhudi za dhati za kuifufua                TTCL.
        "..Bodi imetoa                ushauri, miongozo na maelekezo kwa menejimenti, imeshiriki                vikao vya majadiliano ya kuondoka kwa Bharti Airtel na                kipekee, imefanya mawasiliano na ofisi za Serikali                zikiwepo Ofisi ya Rais na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi                na Teknolojia kusisitiza umuhimu wa Kuondoka kwa Bharti                Airtel. Juhudi hizi zimechangia sana kusukuma swala hili                ambalo kwa sasa liko katika hatua za mwisho...," alisema                Bwana Mushi.
        Bodi ya wakurugenzi                ilipitisha uamuzi wa TTCL kuingia katika mradi ya                mabadiliko wa mfumo wa kibiashara ili TTCL iweze kupanua                mtandao wake na kuwa wa kisasa zaidi kuweza kutoa huduma                mbalimbali kwa teknolojia ya kisasa (GSM, UMTS & LTE)                zikiwemo huduma za simu za mkononi na mawasiliano ya data                kwa ufanisi zaidi ili  Kampuni iweze kukabiliana na                ushindani ulioko sokoni na kuongeza pato lake. Tayari                sehemu ya mradi huo imekamilika (4G LTE) ya kutoa huduma                ya data kwa kiwango cha juu katika sehemu ya maeneo kadhaa                ya Dar es Salaam. Utekelezaji wa mradi utaendelea kwa                sehemu zingine.
        Kwa kushirikiana na                Serikali Bodi inaendelea kutoa ushirikiano stahiki katika                hatua za kuiboresha TTCL zikiwemo kuhakikisha TTCL inapata                mtaji wa kutosha kuendesha shughuli za mawasiliano ndani                na nje ya nchi kuweza kuendana na Sera za Taifa na                kuboresha pato la Kampuni. Bodi imekua ikitoa mchango                mkubwa kuhakikiksha Mkongo wa Taifa unaendeshwa  vizuri                kwa kuwa na mawasiliano wakati wote. Aidha, sambamba na                maamuzi ya Baraza la Mawaziri juu ya TTCL kumilikishwa                Mkongo wa Taifa, Bodi ya Wakurugezi imetoa mchango mkubwa                juu ya ufuatiliaji wa swala hili kwenye Wizara husika.                Serikali kupitia wizara hya Mawasiliano iko katika hatua                nzuri katika kukamilisha swala hili." Alieleza katika                taarifa yake.
        ![]()  |             
| Baadhi ya wanahabari wakifuatilia mazungumzo hayo. | 
Akizungumzia Kampuni                ya Rubiem ambaye ni Mshauri mwelekezi aliyepatikana kwa                kufuata taratibu sahihi za manunuzi ya Umma, alisema                mchango wa kampuni hiyo katika mpango wa mageuzi                kibiashara ni mkubwa na unaonekana dhahiri tofauti na                madai yaliyotolewa.
        "...Matokeo ya kazi                yake yataanza kuonekana mwishoni mwa mwaka huu ambapo                huduma na bidhaa mpya zitaingia sokoni. Mshauri huyu                anatarajia kukamilisha kazi yake katika robo ya kwanza ya                mwaka 2016. Ieleweke pia kwamba, hatua ya Menejimenti                kumuongezea muda mshauri huyu hazihusishi gharama zozote                za nyongeza nje ya mkataba wake wa kazi na TTCL.
        Menejimenti ya                Kampuniya Simu Tanzania TTCL inaomba kutumia fursa hii                kuwajulisha Umma kwamba, hali ya Kampuni yao ni thabiti,                utendaji wa kazi unaendelea vizuri na jitihada mbali mbali                za kuboresha huduma zinaendelea kwa ufanisi mkubwa,"                alifafanua Bwana Mushi kwa wanahabari.
        "...Menejimenti ya                Kampuniya Simu Tanzania TTCL inapenda kuujulisha Umma                kuwa, oja zote zilizotolewa na TEWUTA si za kweli, ni                taarifa zilizopotoshwa kwa makusudi, zikilenga kufanikisha                malengo binafsi na kukwamisha jitihada kubwa zinazofanywa                na Wizara ya Sayansi na Mawasiliano, Bodi ya Wakurugenzi                wa Kampuni, Menejimenti na Wafanyakazi wa TTCL wenye lengo                la kuifanya Kampuni kutimiza kikamilifu Wajibu wake kwa                Umma. Ieleweke pia kwamba, Muundo wa mishahara ya                Watumishi wa Kampuni ya simuTanzania TTCL uko wazi na ndio                unaotumika kulipa mshahara ya wafanyakazi wote wa Kampuni                ya Simu Tanzania. Ofisi inayolipa mishahara ya wafanyakazi                wote wa TTCL iko idara ya Fedha na kusimamiwa na                wafanyakazi wa Kampuni ya Simu. Hakuna Payroll yoyote ya                Siri inayotumika tofauti na hiyo iliyoainishwa, hakuna                posho zozote zinalipwa kinyume na utaratibu." alieleza                Meneja huyo wa TTCL.
        



0 comments:
Post a Comment