Raia wanne kutoka China, jana walipandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya kujibu mashtaka matatu ya uhujumu uchumi likiwamo la kukutwa na pembe kumi na moja za faru zenye thamani ya Sh 902.8milioni.
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Achiles Mulisa akisaidiana na Simon Wankyo, alidai kuwa washtakiwa wote kwa pamoja walishiriki kuhujumu uchumi kinyume cha sheria ya nchi.
Pia, alidai kuwa walipanga njama na kutekeleza kuingiza nchini pembe hizo za faru bila kibali cha Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa, kwa kumiliki nyara hizo bila kibali.
Mulisa alidai kuwa washtakiwa walikamatwa Novemba 6, mwaka huu katika mpaka wa Kasumulu wilayani Kyela wakiwa wamezificha pembe hizo kwenye gari walilokuwa wakisafiria kutoka nchini Malawi kuja Tanzania.
Hata hivyo, washtakiwa wote walikana mashtaka na Wakili Mulisa alisema upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Alimuomba Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa, Michael Mteite apange tarehe ya kuendelea kusikilizwa kesi hiyo.
Wakili wa upande wa utetezi, Ladslaus Lwekaza aliiomba mahakama iwapatie dhamana wateja wake kwa madai kwamba mashtaka wanayokabiliwa nayo yanatoa fursa ya kuwapo kwa dhamana hiyo. Hoja hiyo ilipingwa na mawakili wa Jamhuri, waliodai kuwa Mkurugenzi wa mashtaka amezuia dhamana.
Mteite alikubaliana na hoja ya upande wa mashtaka ya kuzuia dhamana kwa washtakiwa hao na aliamuru warudishwe mahabusu. Kesi hiyo itaendelea leo na itasikilizwa kwa mfululizo siku mbili.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment