Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bi.Jane Mutagurwa akiwasisitiza Wataalam katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata ya Mwamalasa, Masanga na Langana Wilayani Kishapu wakati akifungua mafunzo ya jinsi ya kutekeleza Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo wa kupunguza Athari Za Maafa katika kata zao, mafunzo hayo yanaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa Tarehe 1-5 Septemba, 2014. (Kulia) ni Mratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Harison Chinyuka (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Bi.Jane Mutagurwa amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inaweza kupunguza athari za maafa ya ukame ikiwa Wataalam katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata ya Mwamalasa, Masanga na Langana Wilayani Kishapu watashirikishwa katika Kuijengea Jamii Uwezo wa kupunguza Athari Za Maafa katika kata zao.
Akiongea wakati akifungua mafunzo ya kuijengea uwezo jamii wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame kwa Wataalam waliopo katika Ngazi ya Kata yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Maafa kwa Tarehe 1-5 Septemba, 2014, wilayani Kishapu, Mutagurwa alibainisha kuwa kupitia mafunzo hayo wataweza kuvieimisha vikundi vya kata zao husika juu ya kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame.
"Katika mafunzo haya nimeambiwa mtafundishwa matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa, Dhana ya Maafa ikiwa ni pamoja na Sera na sheria ya maafa, namna ya kubainisha viashiria vya upungufu wa chakula, tathmini ya upungufu wa chakula pia na mwongozo wa ugawaji wa chakula cha msaada. Napenda niwasihi tumieni fursa hii ya mafunzo haya vizuri ili muweze kuwaelimisha wananchi wa Wilaya yetu namna bora ya kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame nami naahidi nitafuatilia kuona jinsi mnavyo elimisha wananchi katika kata zenu" alisisitiza Mutagurwa.
Mutagurwa alifafanua kuwa Kishapu bila athari zitokanazo na maafa ya ukame inawezekana ikiwa wataalam wa ngazi ya kata watashirikishwa kwa kuwa wao ndio wanao uwezo mkubwa kwa ngazi ya kata wa kutambua viashiria na vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa na hatimaye kutoa ushauri sahihi kwa wananchi wa kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame.
"Kwa mfano Maafisa Ugani kwa utaalam wao kutokana na mvua kutonyesha mara kwa mara katika wilaya yetu, kupitia mafunzo haya wataelewa matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa ili waweza kuwashauri wakulima matumizi ya mbegu na pembejeo za kilimo kwa kipindi muafaka cha kulima mazao yanayostahimili ukame, na hatimaye kuepukana athari ya ukame ambayo ni wilaya yetu kuwa na upungufu mkubwa wa chakula" alisema Mutagurwa.
Aliongeza kuwa waratibu wa Elimu katika kata na Watendaji wa Kata hawana budi kuhimiza upandaji wa miti katika kata zao, kwakuwa miti ikipandwa kwa wingi wilayani humo inaweza kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwemo ukame.
Awali akimkaribisha Mkurugenzi huyo, Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu Maafa, Bw.Harison Chinyuka alibainisha kuwa mafunzo hayo ni sehem ya utekelezaji wa Mradi Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa Iliyoathirika Zaidi Na Ukame ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji Wakuu wa Mradi huo. Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 uliozinduliwa Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba2013.
0 comments:
Post a Comment