December 01, 2015

  • PINDA: JITIHADA ZA DK: MENGI KWA WENYE ULEMAVU ZIUNGWE MKONO



    PINDA: JITIHADA ZA DK: MENGI KWA WENYE ULEMAVU ZIUNGWE MKONO


    Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, ameitaka jamii kuunga mkono jitihada za Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, kuwasaidia wenye ulemavu nchini badala ya kubeza.



     
    Alitoa wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kukabidhi miguu mbadala 60 kwa watu wenye ulemavu wa miguu.
     
    Miguu mbada hiyo imetolewa na kiwanda cha nondo cha Kamal Group cha jijini Dar es Salaam.
     
    Pinda alisema kila mtu ni mlemavu mtarajiwa kwa kuwa katika maisha ya binadamu, anaweza kupata ulemavu wakati wowote, hivyo kila mmoja anatakiwa kutumia uwezo wake kuwasaidia wenye shida mbalimbali.
     
    "Kila mara huwa nasema tungewapata kina Mengi wengi, kundi la wenye ulemavu haliwezi kutushinda kulitimizia mahitaji ya msingi…wapo wanaobeza mchango anaoutoa Mengi kila mwaka badala ya kuunga mkono. Hii siyo sawa kabisa, nakusihi uendelee bila kujali lolote," alisisitiza.
     
    Pinda alisema changamoto kubwa inayowakabili wenye ulemavu ni unyanyapaa kutoka kwenye jamii kiasi cha kujiona hawastahili kwenye maisha, jambo ambalo halitakiwi kwa kuwa wanahitaji kuwezeshwa kumudu mahitaji yao.
     
    Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Mengi aliwashukuru Kamal Group kwa msaada wa miguu ambayo itawawezesha wasio na mguu au miguu yote, kuendelea na shughuli za kujitafutia maisha kwa kuwa wamepata kiungo au viungo visaidizi.
     
    Alisema msaada huo ulitokana na mahitaji ya wenye ulemavu wakati wa sherehe ya Mwaka Mpya iliyoandaliwa na yeye (Mengi) kwa wenye ulemavu ambapo Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliguswa na kuamua kutoa msaada huo.
     
    "Naishukuru kampuni ya Kamal Group kwa kuwajali wenye ulemavu, wanafanya biashara, lakini wanaikumbuka jamii...utajiri una mambo mawili, kwanza kupata utajiri uliobarikiwa wenye sura ya halali na unatumia sehemu yake kwa ajili ya jamii hasa wenye mahitaji muhimu kama hawa ambao hawana miguu au mguu, hapo ndipo utajiri wako unakuwa na maana," alisema.
     
    Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Tanzania (Chawata), John Mlabu, alisema bei ya mguu mmoja bandia katika hospitali za rufaa nchini inafika Sh. milioni mbili, jambo ambalo huwafanya wengi kushindwa kumudu gharama hizo.
     
    "Msaada wa miguu 60 ni mkubwa sana kwetu, mtawawezesha watu wenye mguu mmoja au wasio na miwili, kutekeleza majukumu yao kwa urahisi tofauti na wasio na mguu kabisa. Tunawashukuru sana Kamal Group kwa kutujali," alisema.
     
    Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Donan Mmbando, alisema wenye ulemavu wa aina mbalimbali nchini ni 2,641,802 sawa na asilimia tano ya Watanzania, huku wenye ulemavu wa ngozi ni 525,019 sawa na asilimia 1.19.
     
    Alisema Tanzania imepata cheti cha kufanikiwa kufuta ugonjwa wa polio, jambo ambalo linadhihirisha mafanikio katika kudhibiti ulemavu unaosababishwa na ugonjwa huo.
    CHANZO: NIPASHE


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.