MTU mmoja aliyedaiwa kuwa ni daktari wa jijini
Mwanza, Raymond Simion (36) amekutwa amekufa ndani ya chumba kwenye nyumba ya
kulala wageni ‘gesti’ ijulikanayo kwa jina la Nesta iliyopo Ubungo NHC wilayani
Kinondoni jijini Dar.
Taarifa kutoka katika gesti hiyo zinasema
marehemu alijiorodhesha kwenye kitabu cha wageni kuwa ni daktari wa Hosptali ya
Nyamagana jijini Mwanza na alikuja Dar kikazi kwa muda wa wiki moja. Mauti
yalimkuta akiwa na siku mbili tu tangu alipowasili.
Mmoja wa wahudumu wa gesti hiyo ambaye hakupenda
jina lake litajwe gazetini alisema kuwa, daktari huyo alifika katika gesti hiyo
Jumapili ya Mei 4, mwaka huu na kuchukua chumba namba 102.
Alisema Jumatatu ya Mei 5, marehemu aliomba
abadilishiwe chumba, akapewa namba 105 ambamo mauti yalimkutia.
Uwazi lilifanikiwa kufika katika eneo la tukio
na kufanya mahojiano na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo NHC, Amani
Sizian ambaye alisema taarifa ya kifo cha daktari huyo aliipokea saa 9: 03
alasiri ya siku ya tukio ambapo mhudumu wa gesti hiyo ndiye aliyempigia simu
kumjulisha.
Kiongozi huyo aliendelea kusema kuwa mhudumu
huyo alimweleza kwamba marehemu baada ya kuchukua chumba Jumapili alitoka na
kurudi saa 3:00 usiku ambapo alilala, lakini kesho yake hakuonekana
kutoka.
“Mhudumu aliniambia kuwa baada ya kutomwona
asubuhi, hawakumfuatilia hadi ilipofika saa 9:00 alasiri ambapo walikwenda
kumchungulia chumbani kwake na kumwona katika hali ya kutokuwa hai.
“Ilibidi niende. Nilipofika tukakuta mlango
umefungwa kwa ndani.
Katika kumchungulia tulimwona mtu huyo akiwa
amekaa kitandani bila kujigeuza jambo lililonifanya nipige simu polisi ambao
walifika na kuvunja mlango na kumkuta akiwa amefariki dunia,” alisema mwenyekiti
huyo.
Aliongeza kuwa, katika chumba hicho alichofia
mteja huyo, kulikutwa mabomba mawili ya sindano ambapo moja lilikwishatumika,
pia kulikuwa na mifuko miwili yenye nguo na begi moja.
Polisi waliuchukua mwili na kuupeleka Hospitali
ya Taifa Muhimbili. Hata hivyo, ndugu wa marehemu walipatikana na mwili
kufanyiwa uchunguzi na daktari kisha kuuchukua na kuusafirisha kwenda Mwanza kwa
mazishi.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP
Camilius Wambura alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Marehemu
alikutwa na mabomba mawili ya sindano, moja lilishatumika na lilikuwa na masalia
ya damu. Pia kulikuwa na kete moja ya vitu vinavyodhaniwa kuwa ni madawa ya
kulevya.
Stori: Makongoro Oging’, GPL
0 comments:
Post a Comment