MAMBO yanazidi kuwa mambo kuhusu ile ndoa ya Mbunge Vicky Kamata iliyoyeyuka katika dakika za majeruhi, safari hii Risasi Mchanganyiko limefanikiwa kuwanasa baadhi ya wapambe ambao walitakiwa kuwa kwenye msafara wa harusi hiyo kutoka kanisani hadi ukumbini.
Wapambe hao walitia timu kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Vicky katika Hospitali ya General iliyopo Tabata jijini Dar es Salaam, Jumamosi iliyopita (ambayo ndiyo ilikuwa ndoa ifungwe).
WAPAMBE WATATU
Katika idadi ya watu sita waliofika kumjulia hali Vicky, watatu wakiwemo wanaume wawili ndiyo waliokuwa wamevaa sare ya harusi hiyo ambayo ingetawaliwa na rangi ya purple 'papo' (angalia picha ukurasa wa mbele).
SARE KAMILI
Iilithibitika kwamba sare za shughuli hiyo zilishashonwa, wanaume waliokuwa mstari wa kusindikiza maharusi walitakiwa kuvaa suti nyeusi (single button), shati jeupe na tai fupi (necktie) yenye rangi ya papo
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wanawake ambao pia walikuwa kwenye msafara wa maharusi (ma-maids) walitakiwa kuvaa magauni ya rangi hiyohiyo ya papo.
KWA NINI WALIVAA HUKU WAKIJUA HARUSI HAIPO?
Kwa mujibu wa chanzo chetu, wapambe hao walikuwa ndani ya mavazi hayo kwa sababu walijua baada ya ndoa kuyeyuka, wasingeweza kuvaa siku nyingine.
"Unajua wale si kwamba walikwenda pale na sare wakijua ndoa ipo, walijua kabisa kwamba haipo ila sasa kwa sababu ndiyo ilikuwa siku yenyewe ilibidi wajipigilie tu kama kusafisha hali ya hewa au wengine husema 'kuoshea' jina," kilisema chanzo.
UKUMBI WADODA
Waandishi wetu Jumapili iliyopita walikwenda mbele zaidi kwa kufika kwenye Hoteli ya Hyatt Regency The Kilimanjaro ya jijini Dar es Salaam ambako shughuli ya ndoa hiyo ingefanyikia.
Mfanyakazi mmoja ambaye aligoma kutaja jina kwa sababu si msemaji wa hoteli hiyo alisema ukumbi ambao ulikuwa utumike kwa harusi ya Vicky Kamata uitwao Kili Marquee ulilala doro baada ya wahusika kuweka wazi kwamba hakuna harusi tena.
"Ukumbi ulilala mtupu, taarifa zilishakuja mapema kwamba hakuna harusi," alisema mfanyakazi huyo.
Alipoulizwa ni kwa nini wasikodishe kwa mtu mwingine, mfanyakazi huyo alisema si utaratibu wa hoteli hiyo.
"Wale walishalipia, sasa ukisema ukodishe kwa wengine kwa sababu harusi haipo, je, ingetokea harusi ikaja ghafla na kukuta wateja wengine? Si ingekula kwetu?" Alisema mfanyakazi huyo.
MILIONI 40 ZA MCHANGO ZATATIZA
Kuna habari kwamba, zaidi ya shilingi milioni arobaini ambazo zilikuwa za mchango wa harusi hiyo zimetoweka kusikojulikana.
Fedha hizo zilichangwa na wadau mbalimbali katika kufikia kile kiasi cha shilingi milioni 96 ambazo zilidaiwa tangu awali kwamba ndizo zingefanikisha shughuli nzima ya harusi hiyo iliyotarajiwa kuwa ya kifahari.
BWANA HARUSI HAJULIKANI ALIPO
Ili kupata uwiano sawa wa habari hii, juzi Jumatatu waandishi wetu walimtafuta mwanaume aliyetarajiwa kufunga ndoa na Vicky, Charles kwenye ofisi ya kampuni moja ya simu za mkononi, Kijitonyama jijini Dar lakini baadhi ya wafanyakazi walisema ana wiki mbili hajakanyaga kazini.
"Huyu bosi hajakanyaga hapa wiki mbili, hayupo," alijibu mfanyakazi mmoja.
Risasi Mchanganyiko: "Hajakanyaga kivipi? Kasafiri, yuko likizo au?"
Mfanyakazi: "Aliandika barua ya kuomba mapumziko ya wiki mbili kwa hiyo hatujui yuko wapi kwa sasa.
NYUMBANI KWA VICKY
Baada ya kutoka ofisini kwa bwana harusi, wanahabari wetu walitinga nyumbani kwa bibi harusi Vicky Kamata, Sinza ya Vatican, Dar na kukumbana na mlinzi getini ambaye alisema mgonjwa huyo aliruhusiwa kutoka hospitali saa mbili usiku wa Jumapili lakini alikuwa amelala na haruhusiwi kuzungumza na mtu yeyote zaidi ya kupumzika.
"Mheshimiwa karudi jana usiku saa mbili lakini haruhusiwi kuzungumza na watu, amelala," alisema mlinzi huyo.
GPL
0 comments:
Post a Comment