Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Mahakamani
ALIYEKUWA
Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, mke
wake Eva Mhando, na wenzao watatu, wamefikishwa katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka
sita ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kujipatia Sh.
Milioni 31.7 kwa njia ya udanganyifu.
Kadhalika,
Mhando anakabiliwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuipa zabuni
Kampuni ya Santa Clara Supplies Ltd, huku akijua ana maslahi nayo na
kwamba anaimiliki yeye, mke na watoto wake.
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi. Mbali na Mhando na Eva, washtakiwa wengine ni, France Mchalange, Sophia Misidai na Naftali Kisinga.
Mwendesha
Mashitaka wa Taasisi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),
Leonard Swai alidai kuwa kati ya Aprili Mosi na Desemba 31, mwaka 2011
katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco jijini Dar es Salaam, Mhando
akiwa mwajiriwa kama Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia vibaya mdaraka
yake.
Alidai
kuwa, Mhando alitumia vibaya madaraka yake kwa kuamgalia maslahi yake
binafsi baada ya kuipa zabuni ya kusambaza vifaa vya ofisi kampuni hiyo
inayongozwa na mke wake, Eva na watoto wake, vyenye thamani ya Sh.
Milioni 884.5 na kuisababishia kampuni hiyo kupata faida ya Sh.
31,747,000 kinyume cha sheria .
Katika
shitaka la pili, ilidaiwa kuwa kati ya Januari 6 na Julai 30, mwaka
2011, mahali pasipofahamika, jijini Dar es Salaam, Eva alighushi taarifa
ya ukaguzi wa fedha ya Kampuni ya Santa Clara Ltd, akionyesha kwamba
imekaguliwa na Finx Capital House Desemba mwaka 2010.
Swai
alidai katika shitaka la tatu, Agosti 9, mwaka 2011 jijini Dar es
Salaam, mshtakiwa Eva alighushi nyaraka za umiliki wa hisa kutoka Santa
Clara Supplies Ltd kwenda Eveta John Shing’oma huku akijua siyo kweli.
Upande
huo wa Jamhuri ulidai katika shitaka la nne, Agosti 5, mwaka 2011
katika ofisi za Makao Makuu ya Tanesco, jijini, mshtakiwa Eva
aliwasilisha nyaraka za manunuzi za kughushi akionyesha kwamba taarifa
hiyo imeandaliwa na Finx Capital House huku akijua siyo kweli.
Katika
shitaka la tano, ilidaiwa kuwa kati ya Aprili Mosi na Oktoba 31, mwaka
2011 jijini Dar es Salaam, Eva akiwa kama Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni ya Santa Clara Limited kwa nia ovu, alijipatia faida ya Sh.
Milioni 31.7 kutoka Tanesco baada ya kuwasilisha nyaraka za ukaguzi za
kughushi.
Ilidaiwa
katika shitaka la sita, Oktoba 17, mwaka 2011 katika ofisi za Tanesco,
mshtakiwa wa tatu hadi wa tano, Mchalange, Misidai na Kisinga wakiwa
watumishi wa shirika hilo, walipokea nyaraka za kughushi na kusababisha
Kampuni ya Santa Clara Supplies Limited kupewa mkataba wa kusambaza
vifaa vya ofisini.
Ilidaiwa
kuwa mkataba huo ulisababisha kampuni hiyo kupata mkataba wa zabuni ya
kusambaza vifaa vya Sh. Milioni 884.5 na kupata faida ya Sh. Milioni
31.5.
Washtakiwa walikana mashitaka hayo na mahakama iliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini
wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh. Milioni 8, kuwasilisha hati
za kusafiria mahakamani na wasitoke nje ya Mkoa wa Dar es Salaam, bila
kibali cha mahakama.
Washtakiwa walitimiza masharti hayo na wako kwa dhamana hadi Juni 13, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa.
0 comments:
Post a Comment