Hivi
karibuni nimeshuhudia kusambazwa kwa taarifa mbalimbali kupitia ujumbe
mfupi wa simu (sms) na mitandao ya jamii zikinihusisha na tuhuma
mbalimbali.
Napenda
kuufahamisha umma kwamba taarifa zote zilizotolewa kupitia njia hizo ni
za uongo, chuki, na uzushi. Kilichonisikitisha sana ni kuona kuwa
uzushi huo unachochea kuifarakanisha jamii yetu kwa misingi ya ukabila
jambo ambalo ni hatari kwa umoja na mshikamano ambao Tanzania
tumejitahidi sana kuujenga, na mtu yeyote anayediriki kuleta uchochezi
wa kikabila hastahili kuwa kiongozi wa ngazi yoyote katika taifa letu.
Mimi
ni miongoni mwa Watanzania walio mstari wa mbele wanaomuunga mkono Mhe.
Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika kusisitiza kuwa rasilimali za asili zilizopo nchini ni mali ya
Watanzania na ni lazima wawe wamiliki wakuu wa rasilimali hizo ikiwa ni
pamoja na gesi asilia. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
aliwahi kusema mwaka 1974 katika andiko lake la “Ujamaa ni imani”
ukurasa wa 31, kwamba: “madini au mafuta yalio chini ya ardhi, n.k. vitu
hivi ni mirathi ya wananchi wote”.
Katika
miaka ya hivi karibuni dhana hii ya Watanzania kuwezeshwa na kumiliki
uchumi wa nchi yao imetambuliwa na Serikali na Chama tawala kama
ifuatavyo:
Sera ya Taifa ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 inasema kwamba:
Aya ya 1.5 TAFSIRI YA WANANCHI
“Walengwa
wa Sera ya Uwezeshaji ni Wananchi. Makampuni ya Wananchi ni yale ambayo
yamesajiliwa Tanzania ambayo walengwa wanamiliki asilimia isiyopungua
hamsini ya hisa zote za makampuni hayo. Sera ya Uwezeshaji itajumuisha
wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyakazi na wafanyabiashara katika sekta
mbalimbali na makundi mengine.”
Aya ya 3.1 DIRA
“Uwezeshaji
wa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ni sehemu ya
Dira ya maendeleo ya Taifa kufikia mwaka 2025. Kufikia wakati huo,
sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania inatarajiwa kumilikiwa na Watanzania
wenyewe.
Aya ya 4.1.2 TAMKO LA SERA
“Jitihada
za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi
nchini ni muhimu ziendane na ukuaji wa uchumi unaojumuisha na kunufaisha
Watanzania wengi, kuongeza vipato vyao pamoja na kuinua hali zao za
maisha.”
Nayo Sheria ya Taifa ya Uwezeshaji Kiuchumi ya mwaka 2004 (National Economic Empowerment Act, 2004) katika utangulizi inasema:
“Economic
empowerment is a central means for bringing about economic growth and
social justice among our people that is necessary for the promotion of
peace, tranquility and social stability that has characterized our
society.”
Tafsiri yake ni kama ifuatavyo:
“Uwezeshaji
wa Wananchi kiuchumi ni njia kuu ya kukuza uchumi na kuleta haki
miongoni mwa jamii, mambo ambayo ni ya lazima katika kudumisha amani,
utulivu na mshikamano, ambayo ni tunu ya asili ya jamii yetu.”
Chama tawala, CCM katika “Mwelekeo wa Sera za CCM katika miaka ya 2010 hadi 2020” kimetamka kwamba:
Aya ya 84 UWEZESHAJI WA WANANCHI KIUCHUMI
‘’Chama
Cha Mapinduzi katika sera zake za msingi kama zilivyoainishwa katika
Mwelekeo wa Sera za CCM katika Miaka ya Tisini na Mwelekeo wa Sera za
CCM katika miaka 2000-2010, kimetamka bayana kwamba, mkakati mkuu wa
uwezeshaji wa kiuchumi wa wananchi ni ule unaohakikisha kwamba wananchi
wenyewe wanamiliki na kuendesha uchumi wa nchi yetu ama mmoja mmoja, kwa
kupitia vyama vyao huru vya ushirika wa aina mbalimbali au kwa kupitia
makampuni ya wananchi ya ubia ambamo maelfu ya wananchi watanunua hisa”
Aya ya 103
“Wakati
umefika wa kuweka mazingira bora ya upendeleo kwa Watanzania, kama
inavyofanyika katika nyanja za kimataifa kwa mfano katika utoaji wa
kandarasi za ujenzi, manunuzi n.k. Kuwapendelea Watanzania katika ajira
na biashara nchini ni njia mojawapo ya kuwawezesha kiuchumi.”
Kwa
msingi huo nimekuwa nikiishawishi Serikali kutekeleza sera na sheria ya
uwezeshaji ili kuwashirikisha Watanzania kikamilifu katika uchumi wa
Taifa, na kwa sasa hasa katika uchumi wa gesi asilia, ili kudumisha
amani na utulivu katika nchi yetu.
Jitihada
zangu zimekuwa zikipingwa na kiongozi wa moja za Wizara za Serikali na
amekuwa akitumia mbinu na visingizio mbalimbali. Naamini kwamba
usambazwaji wa uzushi unaofanyika sasa ni mwendelezo wa mbinu hizo
chafu. Mtanzania yeyote hastahili kuwa kwenye uongozi katika ngazi
yoyote kwa staili ya kudharau na kutukana Watanzania akidhani kwamba kwa
kufanya hivyo atajijengea umaarufu. Jambo ambalo Watanzania wengi
wanajiuliza ni kwamba ujeuri tunaoushuhudia unatokana na ulevi wa
madaraka au ulevi wa fedha ama vyote viwili?
Rai
yangu kwa Watanzania ni kupuuza uzushi unaosambazwa, na kwamba
wasikubali kuondolewa kwenye hoja ya msingi ya kutaka kujua namna
serikali yao itakavyotekeleza sera na sheria ya uwezeshaji ili
kuhakikisha kuwa inawashirikisha katika mchakato mzima wa uchumi wa gesi
asilia, kuanzia hatua ya utafutaji na uchimbaji (up-stream) hadi
uchakataji na usambazaji (midstream and downstream).
Na
kwa wale wanaotumiwa na kiongozi huyo ningependa kuwasihi wawe na
uzalendo na mapenzi kwa nchi yao na wakatae kutumiwa kwenye mambo ya
uongo yasiyo na tija kwa taifa letu.
Kinachonipa
faraja katika juhudi zangu za kutetea maslahi ya Watanzania ni maneno
ya Mhe. Rais Dkt. Kikwete aliyoyasema mnamo mwaka 2009 kwamba:
“Midomo
ya Wanadamu imeumbiwa kusema na wakati mwingine wanasema
wanachokifikiria wao hata kama huo siyo ukweli, lakini watauamini,
wataueneza uongo huo na watakuhukumu kwa uongo wao.”
Dkt Reginald Mengi
28 Mei, 2014
0 comments:
Post a Comment