May 30, 2014

  • Bunge la Bajeti kuongezewa muda....Lengo ni kujadili migogoro ya wafugaji na wakulima, pia kujadili muswada wa misamaha ya kodi



    Bunge la Bajeti kuongezewa muda....Lengo ni kujadili migogoro ya wafugaji na wakulima, pia kujadili muswada wa misamaha ya kodi

    MKUTANO wa 15 wa Bunge la Bajeti uliopangwa kumalizika Juni 27, mwaka huu, sasa utaongezewa muda kuruhusu Muswada wa Serikali na Azimio la Bunge juu ya migogoro ya wafugaji na wakulima. Kabla ya kuahirisha kikao cha juzi, Spika wa Bunge, Anne Makinda alieleza kuwa upo uwezekano huo wa Bunge kusogezwa mbele zaidi.
     
    Alisema hiyo inatokana na taarifa alizonazo kuwa Serikali inataka kuwasilisha Muswada kuhusu Misamaha ya Kodi na kuwapo kwa Azimio la Bunge kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.
    "Tutaongeza siku baada ya bajeti, kwani kwa taarifa nilizonazo Serikali inataka kuleta Muswada kuhusu VAT katika Misamaha ya Kodi," alisema Makinda.
     
    "Kuna mtu alisema hapa, sijui mimi nakwamisha nini…sihusiki mimi, hili ni la Serikali. Pia msisahau kuna Azimio la Bunge kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji," aliongeza.
     
    Wiki iliyopita, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alisema iwapo Muswada wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), hautapelekwa bungeni, atakusanya saini za wabunge kumwondoa Spika madarakani.
     
    Lugola aliyasema hayo alipoomba Mwongozo wa Spika, ambaye wakati huo hakuwa Makinda katika kiti chake, akitaka kufahamu ni lini muswada huo unaolenga kufuta misamaha ya kodi, utapelekwa bungeni.
     
    Alisema amepata taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wake wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali ya Mitaa, Rajab Mbarouk Mohamed ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Uongozi kuwa kamati hiyo iliiagiza Serikali kuwasilisha haraka Muswada wa VAT.
     
    Alisema lengo la kutaka muswada huo bungeni ni kupitia na kufuta misamaha yote ya kodi isiyo na tija. Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2012/13 inaonesha ipo misamaha ya kodi ya Sh trilioni 1.5. Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema Serikali ndiyo iliomba kuleta Muswada wa VAT katika Bunge hili la Bajeti.
     
    Kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, Bunge liliagiza Kamati ya Kudumu ya Maji, Kilimo na Mifugo chini ya uenyekiti wa Profesa Peter Msolla, kuangalia suala hilo na kupeleka mapendekezo yake ya jinsi ya kumaliza tatizo hilo linaloshika kasi nchini.
     
    Bunge la Bajeti kwa kawaida huwa halina miswada, kwani wabunge hujikita katika kujadili bajeti za wizara mbalimbali pamoja na Bajeti Kuu ya Serikali.
     
    Mkutano wa sasa ulianza Mei 5, mwaka huu na ulipangwa kumalizika Juni 27, mwaka huu.
     
    Jana, ilikuwa zamu ya wizara za Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na Nishati na Madini ambayo mjadala wake unaendelea leo. Kesho, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mnyaa Mbarawa atawasilisha bajeti yake asubuhi na jioni itasomwa ya Wizara ya Maji ya Profesa Jumanne Maghembe.
     
    Kwa mujibu wa ratiba, Jumatatu utaendelea mjadala wa Wizara ya Maji, kabla ya kumalizia bajeti za kisekta kwa kuwasilishwa Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Jumanne ijayo na kufuatiwa na Wizara ya Fedha siku inayofuata.
     
    Kuanzia Juni 5 hadi 11, mwaka huu, zitatumika kwa Serikali kushauriana na Kamati ya Bajeti kufanya majumuisho kuzingatia hoja zenye maslahi kwa taifa zilizojitokeza wakati wa kujadili bajeti za wizara.
     
    Pia kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe watakaowakilisha Bunge katika taasisi/vyuo mbalimbali na shughuli nyingine yoyote kwa maelekezo ya Spika.
     
    Juni 12, itakuwa siku ya Bajeti ambapo asubuhi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira atawasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi nchini.
     
    Kuanzia Ijumaa ya Juni 13, wabunge watasoma na kutafakari Bajeti ya Serikali kabla ya kuanza mjadala wa siku saba kuanzia Juni 16 hadi Juni 24, mwaka huu.
     
    Juni 25, itasomwa miswada miwili, Muswada wa Sheria Mbalimbali na Muswada wa Fedha ambao utasomwa kwa mara ya tatu Juni 27, ambayo ilipangwa iwe siku ya kuhitimisha Mkutano wa Bunge la Bajeti.

    Credit >>Habari Leo



  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.