Katika makuzi yangu kama binti wa Kiafrika nimefunzwa mambo mengi kuhusu maisha na wajibu wangu kama mtoto wa kike.
Baada ya kuvunja ungo nilianza kuandaliwa kuwa mke mtarajiwa wa mwanaume nisiyemfahamu.
Nimefunzwa
kupika, nimefunzwa usafi wangu wa mwili, nimefunzwa usafi wa nyumba,
nimefunzwa kuvumilia maisha ya ndoa na nikaaminishwa kwamba mwanaume
ndiye kichwa cha nyumba na nikafunzwa wajibu wangu katika kumtumikia,
lakini pia nikafunzwa kupanga bajeti na kuweka akiba ili huyu mume
ambaye ni kichwa cha nyumba akikwama kupata mkate wa kila siku kwa ajili
ya familia niweze kumsaidia.
Kwa
kifupi ni kwamba nilifunzwa mambo mengi lakini yote hayo yakiniaminisha
kwamba siku isiyo na jina lazima nitaolewa na kuwa chini ya mwanaume
ambaye atakuwa ndiye kila kitu kwangu.
Nakumbuka
wakati fulani baada ya mama kuona mabinti ambao nalingana nao umri na
wengine nikiwa nimewazidi umri wakiolewa pale mtaani mama alianza
kunidodosa kama sijapata mtu kama wenzangu.
Lakini
pia alijaribu kutumia misamiati mbalimbali na mafumbo lakini nilielewa
kwamba alikuwa anamaanisha nisiwe mgumu sana kwa wanaume kwani sijui
aliyevutiwa na mimi na anayetaka kunioa.
Nadhani alikuwa anataka kufikisha ujumbe kuwa umri unasonga na wenzangu wanaolewambona miye sisomeki?
Naamini si mimi peke yangu, ninayekabiliana na changamoto hizi za wazazi na jamii kwa ujumla.
Ukweli
ni kwamba malezi ya mtoto wa kike yanamuandaa kuwa mke wa mtu,
yanamuandaa kuolewa na yanamuaminisha kwamba ndoa ndiyo kila kitu.
0 comments:
Post a Comment