Na Mwene Said wa Blogu ya Jamii, Mahakamani
MAHAKAMA Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepanga kusikiliza mapingamizi ya awali ya pande zote mbili katika kesi iliyofunguliwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe dhidi ya Baraza la Wadhamini la Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Katibu Mkuu, Willbrod Slaa, Julai 31, mwaka huu.
Mheshimiwa, Jaji John Utamwa alisema kesi ilipangwa jana kwa ajili ya kutajwa na kwamba itasikilizwa mapongamizi ya awali ya pande zote mbili Julai 31, mwaka huu.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikitajwa jana, alikuwepo wakili Peter Kibatala wa Chadema lakini Zitto na wakili wake hawakuwepo mahakamani.
Katika Kesi hiyo, Zitto anaiomba mahakama kuiamuru kamati kuu na chombo chochote kisijadili uanachama wake hadi rufaa yake itakaposikilizwa katika Baraza Kuu la Chama.
Aidha, mbali na kesi hiyo ya msingi, Jaji John Utamwa alisikiliza maombi ya Zitto akiitaka itoe zuio la muda la kutojadiliwa uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Mahakama ilikubali katika uamuzi wake iliamuru Zitto asijadiliwe chochote kuhusu uanachama wake.
Aidha, Zitto ameiomba mahakama imwamuru, Dk. Slaa kumkabidhi nakala za taarifa na mwenendo mzima wa vikao vilivyomvua uongozi ili akate rufaa katika ngazi ya juu ya chama hicho.
Zitto kupitia wakili wake Albart Msando aliomba mahakama itoe zuio la muda la Kamati Kuu na vikao vingine vya chama kutojadili suala la uanachama wake hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
0 comments:
Post a Comment