Maelezo yangu kuhusu kazi za Kigoma AllStars/LEKADUTIGITE kwa NSSF na TANAPA.
Leo
tarehe 29 Mei, 2014 Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Habari,
Michezo, Vijana na Utamaduni amenituhumu kuhusika na kinachoitwa ufisadi
katika Shirika la TANAPA na NSSF.
Nasikitika
kwamba katika hali niliyonayo ya kumwuguza mama yangu naingizwa kwenye
siasa za majitaka. Kwa sasa nitatoa maelezo kwa ufupi ili kuondoa
upotoshaji.
Kampuni ya
LekaDutigite inamilikiwa na wasanii 15 ambapo kila mmoja ana hisa 5%
ambazo niliwalipia ili waweze kushirikiana katika kazi zao. Hisa 25%
zilizobakia zinamilikiwa na kampuni ya Gombe Advisors ambayo ni kampuni
isiyofanya faida (Company limited by guarantee) na haina maslahi yeyote
ya kibiashara (not for profit company). Hivyo Mimi binafsi sina maslahi
yeyote ya kifedha zaidi ya kuwasaidia wasanii hawa katika kazi zao
mbalimbali.
Wasanii wa
Kigoma AllStars wamefanya kazi na TANAPA na NSSF, kazi ambazo
zinajulikana na zipo. Kwa upande wa TANAPA wasanii hawa waliandaa kazi
ya kuitangaza Hifadhi ya Saadani na walilipwa. Kwa upande wa NSSF
wasanii hao walitunga wimbo na video yake (http://m.youtube.com/watch?v=sMl8T-RkIdM ) na wimbo huo unatumika katika Shirika hilo.
Vile
vile walifanya matamasha mbalimbali ya kuhamasisha watu kujiunga na
NSSF. Wasanii wa Kigoma All Stars wote ni wanachama wa Mfuko huo.
Katika
kazi zote hizi Mimi binafsi sijafaidika kwa namna yeyote ile kifedha.
Kauli yeyote ya kujaribu kuonyesha kazi hizi za wasanii ni ufisadi ni
kauli za kusikitisha na kukatisha tamaa kwa mtu ambaye anajaribu
kusaidia wasanii kufaidika na kazi zao za sanaa.
Toka
mwaka 2012 nilipoanza kujitokeza kusemea wasanii watu kadhaa wenye
maslahi na tasnia hii wamekuwa wakinikatisha tamaa na hata wengine kuona
nimewaingilia kazi zao.
Hivi
sasa wasanii wa Kigoma AllStars ni wanahisa katika kampuni ya PERA
Africa limited ili kufaidika na biashara ya miito ya simu. Yote haya
nilifanya kwa uchungu nilionao kwa vijana wetu na sio kwa kutaka
kufaidika kifedha. Nimeumizwa sana na tuhuma hizi za kuokoteza okoteza.
Inaniumiza
zaidi kutokana na ukweli kwamba ninamwuguza mama yangu mzazi, kipindi
ninachohitaji kutiwa moyo na kuombewa hata na maadui zangu kisiasa.
Kipindi ambacho mama yangu yupo mahututi, tena mjumbe wa kamati kuu ya
chama ambacho watoa tuhuma wanatoka, pole ninayopewa ndio hiyo. Hakuna
namna ya kukosa ubinaadamu zaidi ya hivi.
Najua
wajibu wangu ni kusimamia Mashirika ya Umma na nikiwa mpigania
uwajibikaji nipo makini sana kuhakikisha sina mgongano wa maslahi katika
mambo yangu. Ndio maana sina biashara yeyote ile ili kuhakikisha
natimiza wajibu wangu kwa uadilifu mkubwa. Napata 'moral authority' ya
kutaka uwajibikaji kwa sababu nafanya kazi zangu kwa misingi hiyo 'at
arms length'.
Hivyo
ninataka mara moja CAG afanye ukaguzi wa kazi za wasanii hao kwenye NSSF
na TANAPA. Pia achunguze kama Gombe Advisors ( company limited by
guarantee) ina maslahi yeyote ya kifedha katika kazi hizo za wasanii.
Nataka pia Shirika la NSSF na TANAPA waweke wazi mchakato wa kazi zao na
wasanii hawa kupitia LEKADUTIGITE Limited.
Zitto Kabwe
Mei 29, 2014
Dar Es Salaam
0 comments:
Post a Comment