Stori: Mwandishi Wetu, Dodoma SAKATA la mawaziri kutajwa kuwa ni mizigo,
lililoibuliwa kwa mara ya kwanza na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, limeibuka tena mwishoni mwa wiki iliyopita na
kusababisha viongozi hao kujipanga ili kujitetea, ndani na nje ya Bunge la
Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.
Wakati Nape alirudia kauli yake hiyo kwa mara
nyingine wiki iliyopita mjini Igunga, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola naye
alimwita Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza kuwa ni mzigo
kwa kitendo chake cha kushindwa kuwajibika, hasa katika sakata la mbegu za
pamba.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na mawaziri wanaotajwa kuwa ni
mizigo, zinasema ili kuhakikisha hawapati shinikizo kama ilivyokuwa mara ya
kwanza, wamejipanga kujitetea kwa nguvu zote, ndani na nje ya Bunge, kwa kigezo
kuwa wanaopiga kelele dhidi yao, wanatumiwa na wapinzani wao kisiasa
majimboni.
“Hali siyo nzuri kabisa kaka, wameshtukia kuwa kuna njama za
makusudi za kuwang’oa, wanataka kutumia hii nafasi kujinasua, kwa hiyo kuna
mikakati inapangwa kuonyesha kuwa kelele dhidi yao zina mkono wa wapinzani wao
kisiasa, wanadai hata wanaopiga kelele kutoka CCM, nao wanatumiwa,” kilisema
chanzo hicho.
0 comments:
Post a Comment