May 29, 2014

  • SHEIKH PONDA AGOMA KWENDA MAHAKAMANI

    MKiongozi wa Taasisi ya Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, jana aligoma kufikishwa mahakamani kutoka mahabusu ya Gereza la Mkoa wa Morogoro, akidai kuchoshwa kuhairishwa kwa kesi yake kila anapofikishwa mahakamani.Pamoja na kuchelewa kufikishwa mahakamani, kesi yake iliahirishwa tena hadi Juni 10 baada ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mary Moyo kusema kuwa jalada bado halijarudishwa kutoka Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.Wakili wa kiongozi huyo, Bathelomeo Tarimo alilalamikia hali hiyo na kutaka haki itendeke kwa mteja wake.Akizungumza jana, Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Projest Kahyoza alisema kuwa kukwama kwa faili la Sheikh Ponda ni kutokana na maombi namba 25 ya mwaka 2014 yanayosubiri kusikilizwa mahakamani hadi sasa.
    Msajili alisema kuwa maombi ya Sheikh Ponda ya kutaka kuharakisha usomaji wa rufaa ili utolewe uamuzi na kesi hiyo kumalizika au kuendelea, yatasikilizwa na Jaji Lawrence Kaduri, Juni 16.
    Kwa upande wake, Wakili Tarimo alidai kuahirishwa kwa kesi hiyo kunatokana na kucheleweshwa kusomwa kwa rufani yake namba 89 ya mwaka 2013 aliyowasilisha Mahakama Kuu Septemba 14 mwaka 2013.
    Wakili Tarimo alidai kuwa, rufaa hiyo inahusu moja ya shtaka linalomkabili Sheikh Ponda lililotokana na uamuzi uliotolewa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
    Alidai kuwa majalada yote yanayohusu kesi ya Sheikh Ponda yapo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, lakini cha kushangaza kesi imekuwa ikiahirishwa katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, jambo ambalo alidai kuwa limeanza kumtia wasiwasi mteja wake.
    Upande wa Jamhuri unaowakilishwa na Wakili Sunday Hyera uliiomba mahakama hiyo kuahirisha kesi na kupanga tarehe nyingine ya kutajwa wakati jalada halisi la kesi hiyo lililoitishwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, likiendelea kusubiriwa kuletwa kortini.
    MWANANCHI
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.