May 27, 2014

  • Yanga Yatimua Mastaa wawili, Kocha Mnigeria



    Yanga Yatimua Mastaa wawili, Kocha Mnigeria
    YANGA imeshtukia dili na kuamua kufanya uamuzi mgumu kwenye usajili wake wa msimu ujao, baada ya kupiga chini mapendekezo ya kocha wao wa zamani, Hans Pluijm kuhusiana na wachezaji wapya kutoka Ghana.

    Si suala ya wachezaji hao tu, Yanga imetupilia mbali mpaka jina la kocha aliyependekezwa na Pluijm kwa maelezo kwamba hana sifa za kuridhisha na kushawishi akabidhiwe Yanga.

    Pluijm aliondoka Yanga wiki chache zilizopita baada ya kupata dili mpya Saudi Arabia lakini bado mpaka wikiendi iliyopita alikuwa Ghana akimalizana na wachezaji wawili ili wajiunge na Yanga ambao ni winga wa kushoto na kiungo mkabaji.

    Lakini habari za uhakika kutoka ndani ya jopo la usajili la Yanga ni kwamba uongozi umesitisha usajili wa wachezaji hao wa Ghana na kumwambia kocha huyo aachane nao kwa vile hawana mpango nao tena na wanaangalia sehemu nyingine.

    Mwanaspoti linajua klabu hiyo imeamua kugeukia Kenya ambako itamsajili Straika wa Gor Mahia, Danny Sserunkuma. Habari za uhakika ndani ya Yanga, zinasema kuwa bei ya juu ya usajili kwa wachezaji hao wa Ghana ilitajwa kuwa ni dola 10,000 kila mchezaji huku mshahara ukianzia dola 200(320,000) mpaka 500(800,000) kiasi ambacho viongozi wa Yanga walidai kwamba ni kidogo kwa mchezaji bora wa kigeni.

    "Wale wachezaji ni bei rahisi sana ndio maana tukamwambia aachane nao, halafu hata maelezo yao hayakuwa yamenyooka, kuna vitu vingi vilikuwa vinatia wasiwasi,"alidokeza kiongozi huyo.

    Chanzo hicho kililiambia Mwanaspoti kuwa baada ya kushtukia bei hizo, viongozi walimtaka kocha huyo awalete wachezaji hao ili wafanyiwe majaribio jambo ambalo lilikuwa gumu kwake huku akisisitiza kuwa viwango vyao ni vizuri na wanastahili kusajiliwa moja kwa moja.

    Habari za ndani zinadai kwamba kocha huyo aligoma kuwaleta wachezaji hao kwa maelezo ya kiufundi kwamba amekaa na Yanga na anaelewa mambo mengi ya ndani na udhaifu ulipo hivyo ni watu sahihi.

    Kutokana na hilo, viongozi wa Yanga walidai kuwa walishindwa kuamua na kumtaka kocha huyo asitishe huo mpango wake wa kuwatafutia wachezaji hao.

    Mbali na hilo, kocha huyo kupendekeza moja ya makocha ambao wangerithi mikoba yake ambapo pia imeelelezwa kuwa viongozi hawajaridhishwa na sifa zake aliyependekezwa.

    "Hata kocha aliyempendekeza naye hajakidhi vigezo tunavyovihitaji, kwa sasa tunatakiwa kuwa makini katika usajili na kupata kocha ambaye ataisadia Yanga kwa manufaa makubwa," kilisema chanzo hicho cha kuaminika.

    Kiongozi huyo alisema kuwa kwa sasa uongozi umeamua kuendelea na mchakato wao wa kutafuta kocha ambapo anasubiriwa Mwenyekiti Yusuf Manji arudi nchini kwani ndiye mwenye uamuzi wa mwisho.

    "Manji akirudi ndiye atakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu kocha na usajili, naamini suala la kocha litamalizwa mapema tu kwani naye anatakiwa kuhusika katika usajili mpya."


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.