Ghasia zilizozuka mwishoni mwa mechi ya soka iliyozikutanisha timu mbili
maarufu za AS Vita na TP Mazembe za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
zimesababisha watu wanaokadiriwa kufikia 15 kufariki dunia.
Mechi hiyo ambayo ilichezwa Kinshasa nyumbani kwa
AS Vita, ilikuwa ya kuamua ni timu ipi itaiwakilisha DRC katika Ligi ya Mabingwa
Afrika mwakani.
Katika tukio hilo ambalo Watanzania wawili wanaocheza
soka ya kulipwa katika timu ya TP Mazembe, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta
walikuwapo, watu zaidi ya 20 wameripotiwa kujeruhiwa huku idadi ya vifo
ikitarajiwa kuongezeka. Iliwachukua dakika 20, Samatta na Ulimwengu pamoja na
wachezaji wenzao wa TP Mazembe kutoka uwanjani baada ya ghasia hizo.
Hali
ilivyokuwa
Ghasia hizo zilianza katika dakika tatu za nyongeza wakati
winga wa TP Mazembe, Solomon Asante alipokuwa akijiandaa kupiga kona huku TP ya
Lubumbashi ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Gladson Awako katika
dakika ya 35. Ghafla alirushiwa mawe na mashabiki, ndipo mwamuzi alipoamua
kusimamisha mechi baada ya ghasia kuongezeka.
Baada ya kuona ghasia
zinazidi kuongezeka, polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi ili kutawanya
mashabiki waliokuwa wakipambana na kusababisha watu kukimbia ovyo na kukanyagana
na kusababisha baadhi kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Taarifa ya
serikali ya DRC inasema kuwa vifo hivyo vimetokana na watu kukanyagana baada ya
polisi kufyatua mabomu ya machozi uwanjani na kuwafanya mashabiki kutaharuki.
Gavana wa Kinshasa alisema serikali itachunguza kwa kina tukio hilo na
waliohusika watachukuliwa hatua kali.
Matukio kama hayo yameripotiwa
kutokea DRC kwa nyakati kadhaa hasa katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu
wengi. Mwezi uliopita, watu 14 walipoteza maisha katika vurugu zilizozuka wakati
wa tamasha la kumkumbuka msanii maarufu wa DRC, King Kester Emeneya.
0 comments:
Post a Comment