May 29, 2014

  • UHARIBIFU WA MAGHUBA CHANZO CHA TAKA MBEYA




    Baadhi ya wananchi wakiwa wanaendelea kutoa takataka nje ya Ghuba na kuziweka katika sehemu husika ukiwemo na Mzoga wa Mbwa .



    MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza, amesema tatizo la uchafu uliopo katika maeneo mbalimbali Jijini umetokana na kuharibika kwa maghuba kumi ya kuzolea taka.
     
     
    Zungiza alisema chanzo cha kuharibika kwa maghuba hayo kumetokana na watumiaji wa maghuba hayo kuchoma taka ndani ya maghuba hayo ali inayopelekea kupasuka na kuvujisha taka.
     
     
    Alisema kutokana na kuharibika kwa maghuba hayo maeneo mbalimbali yameathirika na kusababisha wananchi kutupa taka chini na kwamba magari yaliyopo kwa ajili ya kuzoa taka ni machache hivyo kuleta mrundikano wa taka kwa muda mrefu na kuwa kero kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kutupa taka.
     
     
    Mkurugenzi alisema tangu amefika Jijini Mbeya ameweza kukarabati maghuba sita yaliyokuwa yameharibika na sasa maghuba kumi yameharibika hivyo wako mbioni kukatabati pindi utaratibu wa serikali katika manunuzi kukamilika.
     
     
    Alisema  kutokana na uzalishaji mkubwa wa taka unaotokana na ungezeko la wakazi na viwanda wameagiza maghuba mengine 84 yatkayoondoa kero ya muda mrefu ya mrundikano wa taka Jijini Mbeya.
     
     
    Aidha alisema hivi sasa wanajitahidi kuzoa kwa kutumia magari yaliyopo ingawa yanalemewa na uwingi wa taka katika Kata 36 za Jiji ni magari matatu tu yanayofanya kazi kila siku hivyo baadhi ya maeneo ya masoko kutopitiwa mara kwa mara na magari hayo.
     
     
    Aliongeza pia mkakati wa Serikali ni kuongeza magari mengine ya kuzolea taka sambamba na marekebisho ya magari ya kisasa ya kuzolea taka ambapo mazungumzo ya awali baina ya Jiji na Wahisani kutoka China yanaendelea vizuri.
     
     
    Kwa upande wake Afisa Usafishaji Jiji la Mbeya Samwel Bubegwa alisema kuwa mbali ya mikakati hiyo Halmashauri ya Jiji inakusudia kubinafsisha shughuli za usafi kwa vikundi vya vijana vitakavyokuwa na jukumu la usafi katika kila Kata hivyo kuongeza ajira kwa vijana katika kila Kata.
     
     
    Bubegwa alisema utafiti uliofanywa katika Kata ya Iyunga umeonesha mafanikio makubwa hivyo mbali ya kutoa ajira utaboresha usafi katika maeneo yote kutokana na vikundi hivyo kuwa karibu ya wananchi.
     
     
    Afisa huyo alisema hivi sasa vijana katika kila Kata wajiunge ili kuanzisha vikundi hivyo kwani Jiji litatoa tenda kwa vikundi na si mtu binafsi ili vijana waondokane na tatizo la ukosefu wa ajira.
     
     
    Mkurugenzi Mussa Zungiza amemaliza kwa kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jiji la Mbeya kwa kufuata taratibu za usafi ikiwa ni pamoja na kuacha kutupa samadi katika maghuba na mizoga hali inayohatarisha afya za wakazi wanaoishi karibu na maghuba kuwa hatarini na magonjwa yanayotokana na hewa.

    NA MBEYA YETU
     
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.