MSAKO wa Fisi waliovamia makazi ya Vitongoji
vitatu vya Kijiji cha Hungumalwa Kata ya Hungumarwa wilayani Kwimba mkoani
Mwanza, umezua maajabu.
Maajabu
hayo yamehusishwa na imani za kishirikina, baada ya fisi wawili kati ya 12
waliouawa, kukutwa wamevalishwa shanga na Rozali, kiunoni.
Msako huo
wasiku tatu ulioanza juzi (Jumapili) unahusisha mamia ya wananchi wa Kijiji
hicho na vitongoji vyake vya Mwanzabalemi, Mwanega na Mwang’ombe, wanaotumia
siraha za jadi na mbwa wapatao 50.
Habari za
ndani kutoka Kijijini humo zimesema kwamba, kabla ya wananchi hao kuingia
‘vitani’ kusaka wanyama hao ambao baadhi wanadaiwa kumilikiwa na watu wachache
wanaojihusisha na vitendo vya ushirikina, wazee wa Kijiji na Vitongoji hivyo,
walifanya mazindiko (kinga) ya kujikinga na nguvu za washirikina ambazo zinge
kwamisha zoezi hilo.
Kwa mujibu
wa baadhi ya wazee wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina yao yaandikwe,
walisema kuwa makamanda wa jadi wanaoongoza msakao huo pamoja na mbwa wao, wana
kinga za kupambana na imani za kishirikina vinginevyo wasingeweza kuua fisi
wenye shanga na Rozali wanaotumiwa kishirikina.
Diwani wa
Kata ya Hungumalwa Shija Malando akizungumza na waandishi katika Kijiji hicho
jana, alisema wananchi walifikia maamzi ya kufanya msako huo wa siku tatu, baada
ya kundi kubwa la Fisi hao wanaokadiliwa kuwa zaidi ya 80, kuwa tishio kwa
watoto na mifugo.
Alisema
kuwa, kwa muda wa miaka miwili iliyopita hadi sasa, licha ya wanyama hao
kuharibu hekali moja ya matunda aina ya Tikiti Maji yaliyokuwa yamelimwa na
mwanchi mmoja, wameua ng’ombe 109, Mbuzi 135, kondoo 127 na Nguruwe 15 katika
Vitongoji hivyo.
“Njooni
muone maajabu haya.” Alisema Malando na kufafanua “Jana (juzi Jumapili) wananchi
walifanikiwa kuua fisi kumi wawili kati yao wakiwa na maajabu. Mmoja aliukuwa na
Rozali kiunoni na mwingine akiwa na shanga kiunoni huku uume wake ukiwa
umetahiriwa kama binaadam.”
Alisema
fisi waliokutwa na vitu hivyo kiunoni, kwa imani za kabila la Kisukuma,
wanadaiwa kumilikiwa na baadhi ya watu wenye imani za kishirikina na kwamba,
waliuawa majira ya saa 8 hadi saa 10 mchana kwenye eneo la mlima wa
Mwanzabalemi.
Alifafanua
kuwa, fisi kumi waliuawa (jumapili) siku ya kwanza ya msako huo na wengine
wawili waliuawa jana asubuhi na kwamba maeneo ya milima ya Mwanangi katika
Kijiji cha Buyobo na Kitongoji cha Mwanzabalemi yanasadikiwa kuwa na fisi wengi
zaidi.
“Pamoja na kushambulia mifugo wetu,
ilifika mahali wananchi walikuwa hawawezi kutembea kwa uhuru nyakati za usiku na
baadhi ya watoto wanaosoma mbali kukatisha masomo kwa kuhofia kuliwa na fisi
hao.” Alieleza Mwenyekiti wa Kijiji cha Hungumalwa, Clement
Kaswahili.
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Mwang’ombe Joseph Kisena alisema hadi kufikia leo (siku ya tatu
ya msako huo) watakuwa wameua fisi wengi zaidi kutokana na ushirikiano mzuri wa
Vitongoji hivyo vinavyotumia mbwa 50 na siraha mbalimbali za jadi ikiwemo
mikuki, mapanga na marungu.
Kisena
alisema, pamoja na maajabu ya fisi kuvaa shanga na Rozali kiunoni ambayo
wamejionea na kuzua imani za ushirikina kwa baadhi ya wananchi, hawatarudi
nyuma, hadi walitokomeze kundi la wanyama hao ambalo ni tishio kwa wananchi na
mifugo wao.
0 comments:
Post a Comment