Na Nathaniel Limu, Singida
MKAZI wa Kijiji cha Chang’ombe kata, tarafa na
wilaya ya Manyoni mkoani Singida Andrew Mlunda (40),amefariki dunia akiwa porini
kutafuta na kuchimba dawa ya kienyeji.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa
Singida,SACP, Geofrey Kamwela amesema marehemu aliondoka nyumbani kwake juzi saa
10.00 jioni akiwa amebeba shoka na kuiaga familia yake kuwa anakwenda porini
kutafuta dawa yake ya kifua kwani alikuwa anahisi maumivu.
Kamwela amesema kuwa tangu alipoondoka
hakurudi nyumbani hadi giza lilipoingia na kusababisha hofu kwa familia
yake.Hata alipopigiwa simu,simu yake ya kiganjani haikuweza kupatikana.
Kamanda Geofrey
Kamwela
Kutokana na hali hiyo,amesema kuwa familia
hiyo ilitoa taarifa kwa majirani na mara moja majirani walianza msako wa
kumtafuta ndani ya pori la kijiji hicho.
“Wakiwa porini waliendelea kumpigia simu na
kwa bahati walisikia mlio wa simu kutoka kichakani na waliposogea sehemu mlio wa
simu ulikuwa unatoka,walimkuta Andrew akiwa tayari ameishafariki dunia”,amesema
na kuongeza;
“Walimkuta akiwa ametoka damu nyingi huku
shoka lake likiwa pembeni, baada ya hapo,walitoa taarifa katika kituo cha polisi
Manyoni mjini na askari walifika mara moja na kuuchukua mwili kwa ajili ya
uchunguzi”.
Kamwela amesema uchunguzi wa awali umebaini
kuwa marehemu amefariki dunia baada ya kupigwa na kitu kizito kwenye paji la uso
na watu au mtu asiyejulikana.
Aidha, Kamanda huyo amesema chanzo cha tukio
hilo bado hakijajulikana na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kujua
chanzo.Hata hivyo hakuna mtu au watu waliokamatwa kuhusiana na mauaji
hayo.
0 comments:
Post a Comment