- Ilidaiwa kwamba mtoto huyo alifariki baada ya kuchapwa fimbo mwili mzima, kupigwa ngumi na mateke, kisha kupewa adhabu ya kukimbia riadha kuzunguka nyumba yao usiku wa manane.
Simanzi, vilio na majonzi vilitawala Kijiji cha Misiri, Kata ya Bugarama, wilayani Geita, kutokana na tukio la kifo cha mtoto, John Wiliam (4) aliyefariki baada ya kupewa adhabu na baba yake mzazi.
Ilidaiwa kwamba mtoto huyo alifariki baada ya kuchapwa fimbo mwili mzima, kupigwa ngumi na mateke, kisha kupewa adhabu ya kukimbia riadha kuzunguka nyumba yao usiku wa manane.
Baada ya kumalizika kwa adhabu hiyo alipakwa pilipili machoni na makalio hali iliyosababisha mtoto huyo kuzidiwa na kupoteza maisha juzi jioni.
Baba wa mtoto huyo, William Kibyala (40), anadaiwa kufanya ukatili huo baada ya kumtuhumu mtoto wake huyo kukataa kumfungulia mlango wakati alipotoka matembezini usiku wa manane.
Tukio hilo lilitokea Mei 23, mwaka huu saa 10 jioni, siku moja baada ya baba huyo kufika nyumbani usiku akitoka katika matembezi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Joseph Konyo alisema baba wa mtoto huyo alikamatwa muda mfupi baada ya tukio hilo.
"Baba wa mtoto huyu aligonga mlango ili afunguliwe, lakini kutokana na usingizi, mtoto huyo hakuamka kufungua mlango," alisema Konyo na kuongeza kuwa mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Misiri, Someke Mhangwa alisema: "Ni uamuzi wa mahakama, lakini tunataka akipatikana na hatia apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
"Baada ya kupata taarifa za tukio hili, nilifika nyumbani kwa baba wa mtoto huyo na kukuta mtoto wake akiwa amefariki, huku mwili wake ukiwa umevimba pamoja na kuwa na majeraha sehemu mbalimbali."
Alisema kutokana na kupata taarifa hizo mapema aliwasiliana na Polisi Wilaya ya Geita ambao walifika eneo la tukio na kumchukua mtuhumiwa.
Baadhi ya watoto wa familia hiyo, walisema si mara ya kwanza kwa baba yao kumtesa John na kwamba alikuwa akimnyima chakula.
Mmoja wa watoto hao, Shija William alisema mdogo wao alikuwa akipewa adhabu hiyo kwa madai kwamba mama yao alimbambikia mtoto huyo na hakuwa wake.
"Baba alikuwa anasema kwamba mdogo wetu si mtoto wake na kwamba mama alimsingizia kuwa ni mwanaye wakati siyo kweli,'' alisema William.
0 comments:
Post a Comment