Nahodha wa Ngorongoro Heroes, Aishi Manula
KOCHA wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20, Ngorongoro Heroes, John Simkoko amesema kikosi chake kipo tayari kukabiliana na Nigeria leo katika Mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20.
Simkoko amesema michezo miwili iliyopita dhidi ya Kenya, kikosi chake kilikuwa na matatizo katika safu ya ushambuliaji, lakini kwa sasa amenoa safu yake na kuiongezea makali zaidi.
"Tumejiandaa vizuri na kufanya marekebisho ya safu ya ushambuliaji. Tunafahamu kuwa Nigeria ni timu nzuri na kila mtu anajua, lakini tutaingia kushindana na matokeo yatakayotokea tutayaheshimu". Alisema Simkoko.
Kwa upande wake nahodha wa kikosi hicho, Aishi Manula amewaomba mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kuwashangilia na kuepuka kuwazomea pale wanapofanya makosa.
"Kuna wachezaji wengi hawana uzoefu na hawajazoea presha ya kuzomewa. Tukianza mechi halafu wakakosea na kozemewa watapoteza morali".
"Imefikia wakati wa kuiunga mkono timu na kuacha kuwazomea wachezaji. Tumejiandaaa vizuri na tuko tayari kwa mechi". Alisema Manula.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 2,000 kwa sehemu zote wakati upande wa VIP itakuwa sh. 5,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mechi katika magari maalumu.
Afisa habari wa shirikisho la soka Tanzania, TFF, Boniface Wambura alisema lengo la kuweka kiingilio kidogo ni kuwapa nafasi mashabiki wote kuiona timu yao.
"Kiingilio hakijawekwa kwa ajili ya gharama za mechi. Gharama ni kubwa zaidi, lakini tumeweka kiingilio kidogp ili kutoa nafasi kwa mashabiki wote".
"Wito wetu kwa mashabiki ni kuwaomba wafike kesho kwa wingi ili kuwapa motisha wachezaji". Alisema Wambura.
Fainali hizo za 19 za Afrika zitafanyika mwakani nchini Senegal zikishirikisha timu saba zitakazofuzu kwenye mechi za mchujo, na Senegal wanaoingia moja kwa moja kutokana na kuwa wenyeji.
0 comments:
Post a Comment