May 25, 2014

  • PINDA: WEKENI MPANGO MAALUM KUMALIZA TATIZO LA MADAWATI RUKWA

    3798256_origTAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
    WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa uhakikishe unamaliza tatizo la upungufu wa madawati ili watoto wa shule za msingi wasiendelee kukaa chini.Ametoa agizo hilo jana usiku (Jumamosi, Mei 24, 2014) wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kupokea taarifa ya Mkoa huo, Ikulu ndogo, mjini Sumbawanga.Waziri Mkuu amewasili mkoani Rukwa jana jioni akitokea Dodoma ambapo atamwakilisha Rais Jakaya Kikwete kwenye ibada ya kumuweka wakfu Askofu Mteule Conrad Nguvumali wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Rukwa itakayofanyika leo (Jumapili, Mei 25, 2014) kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.

    Akifafanua kuhusu tatizo la madawati, Waziri Mkuu alisema: “Lazima mjipange kama mkoa ili muweze kusaidia juhudi za Serikali kupunguza tatizo la madawati kwa watoto wetu wa shule za msingi”.
    “Lazima mje na mpango maalum… mathalani kwenye Halmashauri zenu huko, angalieni hizo mbao zinazokamatwa. Badala ya kuziuza, hizo mbao ziende kutengeneza madawati na yakikamilika yaamuliwe kabisa haya yanakwenda shule fulani, na utaratibu uendelee hadi shule zimalizike,” aliongeza.
    Alisema utaratibu huo unaweza kumaliza tatizo la upungufu wa madawati kwa uhakika zaidi kwani hata Halmashauri zinapoamua kupiga mnada mbao zilizokamatwa, fedha inayopatikana huwa haiendi kutengeneza madawati.
    Kwa mujibu wa taarifa kutoka idara za elimu za mkoa wa Rukwa, Halmashauri tatu za wilaya za mkoa huo ambazo ni Nkasi, Kalambo na Sumbawanga Vijijini zinakabiliwa na upungufu wa madawati 33,799, wakati mahitaji ya madawati ni 62,118 na yaliyopo ni 28,319. Manispaa ya Sumbawanga ilisema ina upungufu wa madawati 675 bila kutaja yaliyopo ni mangapi wala mahitaji yake ni kiasi gani.
    Akizindua Wiki ya Elimu Kitaifa mjini Dodoma Mei 3, mwaka huu, Waziri Mkuu  aliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ambayo inasimamia sekta ya elimu iandae utaratibu wa kuzibana Halmashauri ziwe za mjini au vijijini kwani zote zina uwezo wa kupunguza tatizo hilo kulingana na fursa zilizonazo. “Nasisitiza jambo hili liwe ni ajenda ya kudumu,” alisema Waziri Mkuu.
    Mei 14, 2014, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 30 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Tanga, Waziri Mkuu aliwataka Mameya na Wenyeviti wa Halmashauri kuhakikisha wanamaliza tatizo la madawati kwani nyenzo wanazo kupitia Halmashauri wanazoziongoza.
    Mapema, akiwasilisha taarifa ya Mkoa wa Rukwa, Mkuu wa Mkoa huo, Mhandisi Stella Manyanya alisema mkoa huo kupitia kamati za shule na uongozi wa kata umeweka mkakati wa kutatua tatizo la madawati kama njia mojawapo ya kuboresha taaluma katika mpango wa Matokeo Makubwa na ya Haraka (BRN).
    Akizungumzia kuhusu hali ya miundombinu katika Mkoa huo, Eng. Manyanya alisema kazi za ujenzi wa barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami unaendelea sasa baada ya msimu wa mvua kumalizika na baadhi ya wakandarasi kupatiwa fedha na Serikali.
    Kuhusu usanifu wa Daraja la Mto Momba lililoko mpakani mwa mikoa ya Rukwa na Mbeya, Eng. Manyanya alimweleza Waziri Mkuu kwamba kazi hiyo imesimama kutokana na kina cha maji kupanda licha ya kuwa ilipaswa kukamilika tangu Machi mwaka huu.
    “Usanifu ulitarajiwa kukamilika Machi 2014, lakini kutokana na kina cha maji kupanda, uchunguzi wa matabaka ya udongo chini ya maji umeahirishwa mpaka maji yatakapopungua,” alisema.
    Hata hivyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wanatarajia kazi ya usanifu na uandaaji wa nyaraka za zabuni utakamilika mwezi Mei mwishoni na baada ya hapo zabuni kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo itatangazwa.
    IMETOLEWA NA:
    OFISI YA WAZIRI MKUU,
    JUMAPILI, MEI 25, 2014
  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.