August 25, 2015

  • WASIOONA WATAKA KARATASI MAALUM ZA KUPIGIA KURA



    WASIOONA WATAKA KARATASI MAALUM ZA KUPIGIA KURA

    CHAMA cha Wasioona Tanzania (TLB), kimeomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuandaa karatasi maalumu za kupigia kura kwa wasioona ili kuondoa uwezekano wa mtu aliyeteuliwa kupiga kura kwa niaba ya asiyeona kumrubuni.


    Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TLB, Luis Benedicto alisema, kura ni siri ya mtu na ni haki ya kila mtu kupiga kura kumchagua kiongozi amtakaye.
    Alisema katika chaguzi za nyuma walikuwa wanalazimika kuwa na watu wa kuwasaidia lakini hawana imani ya asilimia 100 na watu hao kwani wanaweza kuwadanganya na hivyo kuchagua kiongozi wanayemtaka.
    "Naweza nikamwamini mtu lakini pia anaweza kunidanganya. Mimi sioni na yeye anaona hivyo anaweza kunidanganya kuwa amemchagua mtu niliyemtaka mwisho wa siku unakuta kadanganya na kumchagua mtu tofauti," alisema Benedicto.
    Aliongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali walizokutana nazo kipindi cha kujiandikisha katika daftari la kupiga kura ambazo wasingependa kukutana nazo siku ya kupiga kura.
    "Tume inapaswa kutumia muda huu kuhakikisha wanashughulikia changamoto hizo ili zisitokee tena. Tulisumbuka sana sababu ya kutoona kwetu. Hatupendi yatokee tena, watumie muda huu kutuandalia mazingira rafiki," alisema.
    Aidha alisema katika mipango ya NEC ya sasa, inapaswa kuona umuhimu wa kuweka wawakilishi wa walemavu wa aina mbalimbali ili kuondoa mkanganyiko uliopo kuhusu haki na fursa zao.
    Pia alisema Tume ya Taifa ya uchaguzi inatakiwa kutoa elimu ya uraia, vifaa vya kupigia kura na miundombinu itakayowawezesha wao kufika kwa uraisi katika vituo vya kupigia kura. "Tumezungumza mara nyingi sana juu ya suala hili, lakini mpaka sasa hatujapatiwa majibu. Tuko njiapanda, hatujui itakuwaje," aliongeza Benedicto.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.