Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec),            imesema kuwa imeunda timu ya ushindi ya kuhakikisha matokeo ya            uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu yanatangazwa kwa wakati, ya            kweli na haki kwa pande zote.
                Akizungumza na Nipashe jana            lililotaka kujua mipango ya Tume ili kuondoa malalamiko ya            wananchi, vyama vya siasa, wagombea na wadau kuhusu            kucheleweshwa matokeo na kuzua hofu ya uchakachuaji,            Mkurugenzi wa Nec, Ramadhani Kailima, alisema timu hiyo            itakuwa na wajibu mkubwa na hakuna kulala hadi matokeo yote            yawe wazi.
        "Tutakuwa na timu ya ushindi            kutangaza matokeo yote mapema, hakuna kulala hadi tutoe            matokeo kwa wakati, ya haki na kweli na yanayoaminika kwa            wapigakura," alisema.
        Alisema malalamiko ya kupendelewa            kwa chama chochote hayana msingi wowote kwa kuwa Tume haina            chama na haitapendelea chama zaidi ya kuweka wazi matokeo yote            itakayoyapata kwa wakati kwa kuwa watakuwa wanafanya kazi            kisasa zaidi.
        Alipoulizwa juu ya uzoefu wa Tume            miaka ya nyuma kuhusiana na kuchelewesha matokeo hata ya            maeneo ya mijini kunakofikika kirahisi, Kailima alisema kama            kutakuwa na ucheleweshaji sababu zitawekwa wazi na wapigakura            watatangaziwa bila kificho.
        "Ya 2010, yasizungumziwe sasa kwa            kuwa tunafanya kazi kisasa kuhakikisha matokeo yanakuwa wazi            na kila hatua wananchi watatangaziwa," alisema na kuongeza:
        "Tunawaomba wananchi mara baada ya            kupiga kura wakae mbali na ikiwezekana waende nyumbani kwa            kuwa kila kituo cha kupigia kura kutakuwa na mawakala kama            kuna tatizo lolote la kufanya matokeo yasitangazwe kwa wakati,            watajulishwa mapema." 
        Kailima alisema Nec iko huru na            inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni na            haiingiliwi kokote kwani katika kugawa majimbo, Chama Cha            Mapinduzi (CCM) ambacho kinadaiwa kubebwa na Tume,            kimelalamika na kama wangekuwa wanapendelewa, ni wazi kuwa            malalamiko yao yangesikilizwa, lakini Tume imeamua kufanya            kazi zake kwa uhuru.
        "Uhuru wetu siyo jina, bali ni            kutekeleza majukumu ya kikatiba na sheria bila kuingiliwa,            kiwe chama au mtu hawaruhusiwi kutangaza matokeo ya uchaguzi,            bali msimamizi wa uchaguzi wa kata atatangaza ya kata, ubunge            yatatangazwa na Mkurugenzi wa Manispaa, mji au halmashauri na            Tume itatangaza matokeo ya urais," alisema.
        Alisema watumishi wote wa Tume kabla            ya kufanya kazi huapishwa kujiondoa au kukana itikadi ya chama            chake na kuanza kutekeleza majukumu yake ili kusiwe na            upendeleo kutokana na itikadi.
        Alipoulizwa kuhusu matukio kadhaa            yaliyotokea katika uchanguzi mkuu wa mwaka 2010 ikiwamo            wasimamizi wa baadhi ya majimbo mfano, Shinyanga mjini            kutoroka baada ya kutangaza matokeo yenye utata yaliyompa            ushindi mgombea wa CCM na kuzua vurugu, Kailima alisema:
        "Tuko 2015, tumejipanga kikamilifu,            ndiyo maana tuna timu ya ushindi kuhakikisha hakuna            ucheleweshwaji wa matokeo. Itakuwa Tume tofauti na ya miaka            mingine." 
        
0 comments:
Post a Comment