August 22, 2015

  • Haki za Binadamu wang’ang’ania uadilifu wagombea wenye kashfa



    Haki za Binadamu wang'ang'ania uadilifu wagombea wenye kashfa
    KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeitaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kutoa orodha ya viongozi wa umma wanaogombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu, ambao walishahojiwa na kuwekwa hatiani kutokana na maadili yao.
    Chombo hicho kimetakiwa kutowafumbia macho viongozi wanaowania nyadhifa mbalimbali ambao walishindwa kuonesha kiwango cha juu cha maadili wakati wa uongozi wao au wakati wakiwa katika nyadhifa walizowahi kushika.
    Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba alisema hayo jana Dar es Salaam, wakati akizungumzia maadili ya viongozi wa umma wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeshabariki kuanza rasmi kwa kampeni za kuwania nafasi hizo.
    "Katika kipindi hiki tumeshuhudia vyama vya siasa vikipitisha viongozi kuwania nyadhifa mbalimbali na katika michakato mbalimbali ya vyama na kuonesha viashiria vya kutoheshimu misingi ya maadili," alisema Dk Bisimba.
    Alisema baadhi ya walioteuliwa wameshahusishwa, kutajwa na kushitakiwa katika vyombo vya kisheria na vya kikatiba kwa tuhuma za utovu wa maadili.
    Alizitaja kashfa hizo kuwa ni rushwa, matumizi mabaya ya ofisi za umma na kutowajibika, vitendo ambavyo ni kinyume na misingi ya Katiba, sheria na ahadi ya uadilifu ambayo kiongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya mwaka 1995 kifungu cha 6.
    Dk Bisimba alisema sheria hiyo inamtaka kiongozi wa umma kuwa mtu atakayekuwa na kiwango cha juu cha maadili kadri iwezekanavyo, ili wananchi kuwa na imani na kutotiliwa shaka katika uadilifu wake.
    Ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutopitisha majina ya wagombea waliopendekezwa na vyama mbalimbali, ambao walishatuhumiwa au kushitakiwa kwa kashfa za rushwa, kujilimbikizia mali na matumizi mabaya ya ofisi za umma.
    Kwa misingi hiyo, Dk Bisimba pia ameisisitiza sekretarieti iweke wazi majina ya viongozi wa umma ambao hawajatoa taarifa kuhusu mali walizonazo kwa mujibu wa sheria.
    Aidha, ameitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kwa kuzingatia Sheria za Kupambana na Kudhibiti Rushwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi, kuweka na kusimamia mkakati utakaodhibiti mianya ya rushwa na matumizi yasiyo halali ya fedha katika kampeni hizo.
    *Polisi
    Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini limetaka vyama vyote vyenye vikundi vya ulinzi vyenye mwelekeo wa kijeshi, kuvunja vikundi hivyo mara moja kwa kuwa vimekuwa vikiingilia majukumu ya jeshi hilo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
    Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Makao Makuu ya jeshi hilo, Jijini Dar es Salaam.
    Alitaja vikundi hiyo kuwa ni pamoja na Green Guard, Red Brigade na Blue Guard ambapo alisema kuendelea kumiliki vikundi hivyo kwa kisingizio chochote, ni uvunjifu wa Katiba ya nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa, jambo ambalo jeshi hilo haliwezi kuvumiliana.
    "Hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa kwa chama chochote kitakachoendelea kukaidi amri hii," alisema Changonja. Pia alisema katika kipindi hiki cha kampeni, ni muhimu kila mmoja ajiepushe na makosa yanayoweza kusababisha jinai.
    "Mfano wa baadhi ya makosa hayo ni pamoja na kutokutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ndani ya muda ulioruhusiwa kisheria ambao ni saa 48 kabla ya mkutano wa kampeni kuanza, kufanya kampeni kabla au baada ya muda ulioruhusiwa, kutumia lugha ya matusi na kashfa kwa wagombea wengine.
    "Kueneza uongo dhidi ya mgombea wa chama kingine, kuondoa, kuchana au kubandua matangazo ya wagombea. Kuandika maneno mengine katika matangazo yaliyobandikwa, kuzuia watu wengine kusoma matangazo hayo au kubandika tangazo katika maeneo yaliyozuiliwa au juu ya tangazo lingine," alisema Kamishna huyo.
    Chagonja alikumbusha wagombea wote kwa nafasi zao kuelimisha wafuasi wao umuhimu wa kuheshimu sheria, ili kudumisha amani, usalama na utulivu katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
    Alisema jeshi hilo limejipanga vizuri kuhakikisha mikutano yote ya kampeni inafanyika katika hali ya amani na utulivu hadi siku ya uchaguzi na uwepo wa Polisi katika kampeni hizo unalenga kuzuia uhalifu na sio kudhoofisha kampeni, hivyo wananchi watoe ushirikiano kwa jeshi hilo kwa kutii sheria bila shuruti.
    Kutokana na hali hiyo Jeshi la Polisi limetoa tahadhari kwa wananchi wote na vyama vyote vya siasa, kuzingatia sheria zinazowaongoza, ikiwemo sheria ya vyama vya siasa na miongozo mbalimbali ambayo imekuwa ikitolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva.
    Alisema lengo ni kuhakikisha kipindi chote cha kampeni hadi Uchaguzi Mkuu, kila moja anajiepusha na vitendo vyenye mwelekeo wa uvunjifu wa sheria.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.