KONDAKTA wa daladala hii            hakufahamu kama angekutwa na haya masahibu. Hakujua kama mdomo            wake ungemponza na kujikuta katika majanga makubwa ya kupoteza            macho. Hakujua kwamba katika daladala wamo watu wenye tabia na            hulka tofauti.
        Hakutaka kuamini ukweli            kwamba, katika usafiri huo wa umma, upo uwezekano wa kuwamo            'wanga' vibaka, majambazi na wacha Mungu. Laiti angelijua            haya, kondakta huyu asingezozana na abiria huyo. Tatizo            alimchukulia kwa mtazamo wa kawaida wa 'kikondakta' kama            ilivyo kwa makondakta wengi dhidi ya abiria. Angejua kwamba            mtu anayezozana naye si abiria wa kawaida, bali ni mtu asiye            na huruma wala utu, huyo kondakta angekubali yaishe.
        Ngoja sasa niwamegee juu            ya kisa hiki. Ingawa jicho langu halikushuhudia moja kwa moja            kisa hiki, lilipata fursa ya kukutana na mashuhuda.            Walisimulia kilichomkuta kondakta na abiria waliokuwa kwenye            daladala moja inayofanya safari zake kati ya Mbezi na Posta.            Mashuhuda hawa wakaeleza kilichojiri baada ya gari hilo kufika            kituo cha Kimara. Wakasema, kondakta na abiria katika daladala            hiyo, walianza kuzozana kwa kujibizana.
        Haijulikani chanzo            ilikuwa ni nini. Lakini kama ilivyo kawaida katika daladala,            mzozo mwingi huanzia ama kwenye kudai nauli au kusogeza abiria            wabanane aweze kupakia wengine. Siyo jambo la ajabu,            kushuhudia makondakta walio wengi wakitoa kauli za kero kwa            abiria. Au wakati mwingine, kushuhudia abiria akimjibu            kondakta vibaya licha ya kuambiwa kwa ustaarabu. Wapo abiria            wengine ni wakorofi na wababe hivyo wakikutana na makondakta            wenye kero, lazima pachimbike.
        Ndivyo ilivyojitokeza            kwenye daladala hiyo. Inadaiwa baada ya kujibizana, huku            kondakta akimdhihaki abiria huyo kwamba hana cha kumfanya,            (abiria) naye alimhadharisha kondakta kwamba atamfanyia kitu            ambacho hatakisahau maishani. Katika mwendelezo wa kuzozana,            inadaiwa abiria huyo alichomoa chupa ndogo iliyosadikiwa kuwa            na kimiminika, akammwagia kondakta machoni. Mashuhuda wanasema            walishuhudia kondakta akihaha kutokana na macho kuathirika.
        Wakati abiria huyo            akishuka haraka kutoka kwenye daladala, kondakta alipiga            kelele za 'mwizi'. Inadaiwa watu waliokuwa karibu kituoni            hapo, walimshambulia huyo abiria na kumpa kipigo cha mbwa            mwizi. Haijulikani kilichoendelea baada ya hapo. Hata mimi            sifahamu kama macho ya kondakta yameona tena. Wala sifahamu            kama abiria huyo amepona baada ya kipigo kutoka kwa watu wenye            hasira. Kwa ujumla haya ndiyo majanga ndani ya usafiri wa            daladala.
        Kwa kuzingatia majanga            haya, nina kila sababu ya kukaribisha kwa mikono miwili mabasi            maalumu yatakayotoa huduma chini ya Mradi wa Mabasi Yaendayo            Haraka (BRT). Uwezekano wa kupumua na vioja vya daladala ni            mkubwa kutokana na sifa zilizotolewa kuhusu mabasi hayo. Idadi            ya mabasi yanayotarajiwa kutoa huduma chini ya mradi, ni 76.            Tayari mabasi mawili yameshaingizwa nchini na yanatumika            kufunza baadhi ya madereva uendeshaji wake.
        Mabasi hayo yenye uwezo            wa kubeba abiria kati ya 100 na 190 kwa mara moja, ujio wake            na kuanza kwa huduma za BRT, ndiyo mwisho wa daladala za            kawaida kati ya Kimara na Kivukoni, katika Barabara ya            Morogoro. Mabasi hayo yanayotarajiwa kutumia dakika 20 kutoka            Kimara hadi Kivukoni, ndani yana viti kwa ajili ya wazee,            wajawazito na wenye ulemavu. Pia yana mikanda maalumu kwa            ajili ya abiria wanaosimama.
        Vituo vitakuwa na ulinzi            kuhakikisha hakuna shughuli yoyote itakayoendeshwa zaidi ya            kuwapo abiria pekee. Kikubwa zaidi, ni kwamba, mabasi hayo            hayatakuwa na makondakta wala wapiga debe kutokana na mfumo            wake wa kisasa wa ukusanyaji nauli. Hakutakuwapo tena mfumo wa            makondakta kukusanya fedha. Badala yake, ukataji tiketi            utakuwa ni wa kisasa; wa kielektroniki ambao utaratibiwa chini            ya mfumo maalumu.
        Aidha, mamlaka            zinazohusika na huduma hiyo, zinasema wanaangalia uwezekano wa            kuhakikisha hakuna mwingiliano kati ya dereva na abiria. Ina            maana kazi ya dereva itakuwa ni moja tu; kusafirisha abiria            kwa ustaarabu na kuwafikisha waendako. Sifa nyingine            zinazoainishwa ni kwamba, madereva wa mabasi hayo wanatarajiwa            kuwa waliofuzu mafunzo. Pia wanatarajiwa kuwa wastaarabu            kuanzia mavazi hadi kauli zao.
        Kama hayo yaliyoelezwa na            mamlaka yatatekelezwa ipasavyo, ni dhahiri vituko, visa mkasa,            kero na karaha za daladala katika njia hiyo ya Barabara ya            Morogoro, vitakoma. Hatimaye, usafiri huo wa umma utageuka            kuwa tegemeo kwa watu wote wakiwamo wanaolazimika kuingia            gharama kubwa kutumia magari binafsi, kuepuka kero za            daladala. Sasa yametimia. Tukaribishe mabasi haya kwa mikono            miwili na tutakie kila la kheri mradi huo ili hatimaye,            tupumue na vioja vya daladala.
        
0 comments:
Post a Comment