POLISI mkoani Morogoro wanashikilia watu 11, wakazi wa Kijiji cha Mpofu wilayani Kilombero kwa tuhuma za kuvamia na kuchoma moto kituo kidogo cha polisi na ofisi ya serikali ya kijiji hicho.
Watuhumiwa hao ni sehemu ya zaidi ya watu 100 wanaodaiwa kufanya uhalifu huo katika kituo hicho cha polisi Mbingu, katika taarifa ya Mgeta.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya tukio hilo wakishinikiza polisi wamwachie mtuhumiwa aliyewekwa mahabusu katika kituo hicho, Bashiri Kadugula (25), kwa tuhuma za kumshambulia mkewe, Veronica Chabula (21) ili wamwadhibu.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alisema jana kuwa, Kadugula aliwekwa ndani kwa kumkata mkewe kwa panga sehemu mbalimbali za mwili kutokana na wivu wa mapenzi.
Alisema katika tukio hilo ni la Agosti 20, mwaka huu saa 4:00 usiku, mtuhumiwa huyo baada ya kufanya kitendo hicho kwa mkewe akitoroka na ndugu wa Veronica walifanikiwa kumkamata na kumfikisha kituo kidogo cha Polisi Mbingu, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Alisema baada ya ndugu kuondoka kituo cha polisi, kitambo kidogo kulitokea kundi la watu wakirusha mawe kituoni hapo, wakitaka wamuue mtuhumiwa huyo kwa kukerwa na kitendo chake cha kinyama. Kamanda Paulo alisema, askari waliokuwepo kituoni hapo walijitahidi kuwazuia watu hao lakini walizidiwa nguvu.
Alisema polisi walifanikiwa kumtoa mtuhumiwa mahabusu na kumwokoa sambamba na kuokoa silaha za kituo hicho.
Alisema, watu hao waliokadiriwa kuwa zaidi ya 100, walivamia kituo hicho kidogo cha Polisi na kukichoma moto ambapo nyaraka mbalimbali zilizokuwa ndani ya kituo hicho ziliungua na kuteketea kabisa.
Kamanda wa Polisi wa mkoa alivitaja vitu vilivyoteketea kwa moto kuwa ni pamoja na pikipiki tano zenye usajili T 979 BGA aina ya Sky Mark, T901 BUJ aina ya Sanlug, T801 BQA aina ya Sanlug, mali ya Askari Wilson, T194 BVR aina ya T-Better, mali ya Askari Isaya na T904 BUJ aina ya Tianda.
Alisema, kundi la watu hao baada ya kukichoma moto kituo kidogo cha polisi, lilivamia pia Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Mpofu na kisha kuchoma moto nyaraka mbalimbali, ambapo katika matukio hayo watuhumiwa 11 walikamatwa.
Amewataja waliokamatwa kutokana na tukio hilo kuwa ni Imani Mwampombe (40), Geofrey Mwaikambo (46), Eugen Kikoti (41), Janken Mwaikambo (55), Meshack Kikoti (42), Eliud Chumbula (52) na Shukrani Lukimo (35) ambao ni wakulima na wakazi wa kijiji hicho cha Mpofu.
Wengine waliokamatwa ni madereva wawili wa bodaboda ambao ni Ramadhani Hussein (29), mkazi wa Kitongoji cha Ngajengwana, Salum Ngala (36), John Mtikila (55) na Rodrick Mwaikambo (36) wote wakulima na wakazi wa Kijiji cha Tandale- Igima.
Kamanda huyo wa Polisi wa mkoa alisema kwamba watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika na kwamba polisi wanaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine waliotoroka na kusisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutii sheria na kuacha kujichukulia sheria mkononi.
0 comments:
Post a Comment