Bunge la Afrika Mashariki (EALA) linatarajiwa kuanza vikao vyake Jumatatu ijayo hadi Agosti 16, mwaka huu, mjini Kampala, Uganda.
Rais Yoweri Museveni (pichani) wa nchi hiyo anatarajiwa kulihutubia Bunge hilo Agosti 12 na litaongozwa na Spika wake, Daniel Kidega.
Kwa mujibu wa msemaji mwandamizi wa EALA, Bobi Odiko, ajenda katika kikao hicho cha wiki mbili itakuwa kujadili miswada muhimu itakayowasilishwa na kusomwa mmoja kwa mara ya pili na mwingine kwa mara ya tatu.
Aliitaja miswada hiyo kuwa ni Muswada wa Sheria ya Elekroniki wa 2014 na Muswada wa Sheria ya Ubunifu wa Viwanda wa 2015.
Alisema Muswada wa Elektroniki unataka kuweka mazingira ya kutumia teknolojia hiyo katika shughuli za kibiashara katika dunia ya sasa.
Kwa mujibu wa Odiko, muswada huo pia unataka kukuza teknolojia katika matumizi ya mawasiliano, shughuli za Bunge, kuendeleza usalama, kulinda na kuweka mazingira mazuri ya walaji, biashara na serikali za nchi wanachama.
Alisema EALA tayari imekwishapokea maoni mbalimbali ya wadau kuhusu muswada huo.
Akizungumzia Muswada wa Sheia ya Ubunifu na Viwanda wa 2015, ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza Januari mwaka huu, alisema madhumuni yake makubwa ni kukuza ubunifu na viwanda katika nchi wanachama.
"Muswada unaka kuanzisha Baraza la Ubunifu na Viwanda ambalo litaweka mazingira mazuri ya kukuza na kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wananchi," alisema.
Odiko aliongeza kusema kuwa, baraza hilo litakapoanzishwa litahakikisha kuna kuwa na mafunzo maalum yenye viwango vya ubora na ujuzi na maendeleo ya ubunifu na kuanzisha sera na mikakati ya kuziwezesha nchi wanachama kutumia vipaji vya vijana.
0 comments:
Post a Comment