August 14, 2015

  • MADEREVA DAR-TUNDURU KUPIMWA AFYA


    MADEREVA DAR-TUNDURU KUPIMWA FYA
    VITUO vya maarifa sita vitakavyotoa huduma za afya vinatarajiwa kujengwa kando ya barabara kunusuru madereva wa masafa marefu kutoka Dar es Salaam hadi Tunduru. Meneja Mradi wa North Star Alliance anayeratibu ujenzi huo, Edger Mapunda alisema jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.


    Mapunda alisema wanatambua sekta ya usafirishaji inakabiliwa na changamoto ya masuala ya Ukimwi hivyo wameona kuna sababu ya kuwasaidia madereva kwa kuwa wawapo safarini wanakutana na watu mbalimbali. Alisema ujenzi wa vituo hivyo utakapokamilika utawanufaisha pia wananchi waliopo jirani na vituo hivyo.
    Pia watatoa elimu ya afya, upimaji wa magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari pamoja na uendeshaji salama kwa madereva wawapo barabarani. Alisema vituo viwili vitajengwa katika jiji la Dar es Salaam eneo la bandarini, vingine viwili vitajengwa katika mkoa wa Iringa na viwili vitajengwa mkoani Mbeya.
    "Maambukizi ni makubwa katika maeneo hayo. Tulifanya tafiti tokea mwaka 2013 tukagundua mkusanyiko ni mkubwa katika maeneo hayo. Pia Tunduma na Iringa tuligundua huduma za afya sio nyingi," alisema.
    Alisema gharama za mradi mzima ni dola za Marekani milioni moja, na kwamba vituo kama hivyo vimejengwa pia katika nchi ya Kenya ambapo vipo tisa, Afrika Kusini vipo 12 na Malawi viwili.
    Mkurugenzi wa Uraghibishi na Habari Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Jumanne Issango alisema wamekuwa na mkutano wa kujadili uanzishwaji wa mradi wa kujenga vituo sita vya maarifa kandokando ya barabara kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduru.
    Alisema mradi huo utakuwa wa miaka mitatu ulianza Aprili mwaka huu na kumalizika mwaka 2018. Mwakilishi wa madereva wanaosafiri masafa marefu kutoka Chama cha Madereva nchini, Mohamed Sharrif alisema amekuwa na wasiwasi na mradi kama huo unapomalizika huduma zinazokuwepo zinadumaa kwa kukosa mfadhili.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.