August 19, 2015

  • DAR YAKUMBWA NA KIPINDUPINDU



    DAR YAKUMBWA NA KIPINDUPINDU Wauguzi wakiwa katika wodi          iliyotengwa kwa
    Wauguzi wakiwa katika wodi iliyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wenye dalili za kipindupindu katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam, jana. Picha na Salim Shao 



    Dar es Salaam. Ugonjwa wa kipindupindu umeingia Dar es Salaam na kusababisha watu wawili kupoteza maisha na wengine 26 kulazwa katika hospitali za Mwananyamala na Sinza.

    Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kinondoni, Mhandisi Musa Nati alisema watu wengine wa nne wamethibitika kuugua kipindupindu na waliolazwa katika hospitali hizo wameonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
    Alisema wodi mbili zimetengwa katika hospitali hizo kwa ajili ya wagonjwa wenye dalili hizo.
    Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa wanaandaa kambi maalumu kwa ajili ya wagonjwa wa kipindupindu katika eneo la Mburahati.
    Alisema wameanza kuchukua tahadhari kwa kupuliza dawa katika maeneo yaliyoripotiwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo.
    "Maeneo tuliyopuliza dawa ni Manzese, Tandale na vitongoji vya Kijitonyama katika Wilaya ya Kinondoni," alisema Nati
    Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Aziz Msuya alisema mmoja wa wagonjwa alifariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Mwananyamala na mwingine alipoteza maisha akiwa nyumbani na mwili wake kupelekwa Hospitali ya Sinza kuhifadhiwa.
    Alisema katika kuchukua tahadhari ofisi yake imetoa dawa za kunywa na za kupulizia kwa kaya 70 katika maeneo ya Kijitonyama, Mtaa wa Ali Maua.
    Dk Msuya aliwataka wananchi kuchukua tahadhari pale wanapoona mgonjwa anakuwa na dalili za ugonjwa huo ili wamuwahishe katika kituo cha afya. Pia, aliwataka kuhakikisha wananawa mikono kila wakati wanapotoka msalani au kusalimiana kwa kushikana mikono.
    "Tumeshawasiliana na wenzetu wa Bohari ya Dawa (MSD) ili kuhakikisha tunakuwa na dawa za kutosha."
    Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mwananyamala, Sophinias Ngonyani alisema wagonjwa waliothibitika kuwa na kipindupindu ni wawili na wengine 11 bado sampuli zao ziko maabara.
    Alisema wagonjwa hao wanaendelea kupatiwa huduma wakiwa katika wodi maalumu iliyotengwa huku wakisubiri majibu.
    Alipoulizwa juu ya hatua zilizochukuliwa kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa huo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitupa mpira kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik ambaye naye alisema bado hajapewa taarifa kuhusu kuwapo kwa ugonjwa huo.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.