Kikosi cha wekundu wa Msimbazi Simba kesho (Jumamosi) kitacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwa ajili ya kujipima nguvu wakati kinajiandaa kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara inayotarajia kuanza hivi karibuni.
Simba itacheza mchezo huo dhidi ya timu ya URA ya Uganda inayoshiriki ligi kuu ya Uganda na mechi hiyo itapigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Afisa habari wa Simba SC Haji Manara amesema, timu ya URA imeshawasili toka jana na maandalizi ya mchezo huo yameshakamilika kinachosubiriwa ni timu hizo kuoneshana kazi uwanjani.
"Kesho timu ya Simba itacheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki na timu ya URA ya Ugana mchezo utakaofanyika kwenye uwanja wa Taifa kuanzia saa 10:00 jioni, timu ya URA tayari imeshawasili kutoka nchini Ugana. Maandalizi yote ya mchezo huo yameshakamilika na kilakitu kipo sawa".
"Mchezo huo utatumiwa na Simba kuwajaribu wachezaji wake wapya wawili, mshambuliaji mmoja na golikipa".
"Kiingilio cha juu kwenye mchezo huo kitakuwa ni shilingi 20,000 na kiingilio cha chini kitakuwa shilingi 5,000 nawaomba wapenzi wa mpira hususan wa mkoa wa Dar es Salaam waje kuiangalia timu yao kwenye mchezo unaotarajiwa kuwa mgumu ukizingatia kwa mechi kadhaa tulizocheza na URA tumekuwa tukipoteza".
Juma lililopita Simba ilicheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na timu ya SC Villa ambayo pia ni ya Uganda mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa katika kilele cha sherehe za kuadhimisha Simba Day na Simba wakafanikiwa kushinda mechi hiyo kwa goli 1-0.
0 comments:
Post a Comment