August 21, 2015

  • Ajali yaua watu 14, watano wa familia moja


    Ajali yaua watu 14, watano wa familia moja
    Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Charles Mkumbo.

    Watu 14  wakiwamo watano wa familia moja, wamekufa papo hapo na wengine sita kujeruhiwa katika wilaya za Misungwi mkoani Mwanza na Ludewa Njombe baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kupinduka na jingine kutumbukia mtoni.
     
    Katika ajali iliyotokea Misungwi, watu tisa, wakazi wa Mkoa wa Geita, walipoteza maisha baada ya gari aina ya Toyota Noah lenye namba za usajili T812 BJU, walilokuwa wakisafiria kuacha njia na kupinduka juzi saa 11 jioni katika kijiji cha Mwamanga.
     
    Ajali hiyo ilitokea katika barabara kuu ya Shinyanga- Mwanza, baada dereva,  Koplo mstaafu wa polisi, Maurice  Lukenza, kushindwa kulimudu kutokana na kuendesha kwa mwendo kasi.
     
    Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Charles Mkumbo, aliwataja wengine waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni  Malongo Magongo, Shija Somanga, Yun Somanga, Thobias Simon, Michael Simon, Amos Lukenza, Shaban Deus na Samwel Malongo, wakazi wa Geita.
     
    Vilevile aliwataja majeruhi hao ambao walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando iliyopo jijini Mwanza kutokana na hali zao kuwa mbaya kuwa ni  John Nyahunga, mkazi wa Kayenze, Charles Ludahula (Sengerema), Elias Mkeza (Katoro), Shija Magongo (Nyantorotoro), Simon Lukenza (Nzela Geita) na Malongo Samwel wa Kagu, wakazi wa Geita.
     
    NDUGU WATANO WAFA
    Wakati huo huo; watu watano wa familia moja, akiwamo mwanafunzi wa chuo cha uuguzi, wakazi  wa Wilaya ya  Ludewa mkoani Njombe, wamekufa baada ya gari walikokuwa wakisafiria kuacha njia na kutumbukia kwenye korongo kisha mtoni.
     
      Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Willibrod  Mtafungwa, alisema watu walikumbwa na mkasa huo katika eneo la Lugalawa wakati wakisafiri kwa gari aina ya Toyota Cresta lenye usajili T 613 AKA.
     
    Mtafungwa alisema ajali hiyo ilitokea wakati wanafamilia hao wakisafiri kutoka Lugalawa na kuelekea Shaurimoyo baada ya kushindwa kulimudu gari hilo kutokana na kuendesha kwa mwendo kasi.
     
    Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni dereva wa gari hilo aliyejulikana kwa jina moja la Haule, Winslaus Mtweve (40), Upendo Malawa (29), Editor Mtega(35) na mwanafunzi huyo,  Paschal Mlwilo, (22). 
     
    MTOTO AOKOTWA PANGANI
    Katika  tukio jingine, mtoto wa miaka mitatu, Zainabu Adam, ameokotwa katika pango lililopo Mabatini Mtaa wa Nyerere A uliopo jijini Mwanza, baada ya kupotea nyumbani kwao katika mazingira ya kutatanisha.
     
    Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Hassan Maulid, alisema mtoto huyo alikutwa kwenye korongo hilo baada ya baadhi ya wakazi wa eneo hilo kusikia sauti yake wakati akilia. 
     
    "Tulipeleka taarifa kituo cha polisi Mabatini kuhusiana na kelele hizo, tuliongozana hadi eneo la tukio na waokoaji walizama ndani na kumuokota mtoto huyo.
     
    Alisema walimpeleka kituo cha polisi mkoa wa Mwanza na kupatiwa PF3 na kumpeleka hospitalini kufanyiwa uchunguzi wa afya.


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.