Hili ni swali ambalo kwa muda              mrefu limekuwa likiibua mijadala katika duru za kisomi na              ndani ya jamii kwa jumla.
          Watu wamegawanyika katika makundi              matatu, wapo wanaotaka Kiingereza, wapo wanaotaka Kiswahili              na wengine wanataka lugha zote zitumike kufundishia.
        Mfumo wa elimu wa Tanzania              unatumia lugha ya Kiswahili pekee kama lugha ya kufundishia              katika elimu ya msingi na Kiingereza kinafundishwa kama              somo.
        Baadaye Kiingereza hutumika              kufundishia katika elimu ya sekondari, huku Kiswahili              kikifundishwa kama somo.
        Mwanzoni mwa mwaka, Rais Jakaya              Kikwete alizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ambayo              imesisitiza matumizi ya lugha ya Kiswahili kwa shule za              umma. Sera hiyo pia inatambua lugha ya Kiingereza kama lugha              ya kufundishia hasa kwa shule binafsi.
        Sera hiyo inakosolewa na makundi              mbalimbali ya watu kwa madai kwamba inamnyima mtoto wa              Kitanzania uwezo wa kuhimili ushindani katika soko la ajira,              ikizingatiwa kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki inaelekea              kuwa shirikisho.
        Watu wanaotaka Kiswahili kitumike              kufundishia elimu ya msingi na sekondari wanatetea hoja yao              kwamba Kiswahili ni lugha yenye asili ya Tanzania. Kwa hiyo,              kama Taifa hili halitatumia lugha ya Kiswahili basi lugha              hiyo haitakua.
        Pia, kundi hilo linasema Kiswahili              ni lugha ambayo inawaunganisha Watanzania; kutumika kwa              lugha hii kutaongeza umoja na mshikamano wa Watanzania,              sambamba na kudumisha amani.
        Kundi jingine linalopendekeza              Kiingereza kitumike kufundishia, linasema hiyo ndiyo lugha              ya kimataifa ambayo inatumika duniani kote. Watanzania              wakitumia lugha hii watanufaika na fursa mbalimbali              zinazojitokeza sehemu mbalimbali duniani.
        Utafiti wa Twaweza
        Hivi karibuni, Taasisi ya Twaweza              ilitoa matokeo ya utafiti juu ya lugha ipi hasa itumike kama              lugha ya kufundishia elimu ya msingi. Utafiti huo umebaini              kuwa watu sita kati ya 10 wangependa Kiingereza kiwe lugha              ya kufundishia katika shule za msingi na sekondari.
        Watu 1,381 wenye elimu tofauti               walihojiwa katika utafiti huo uliofanyika Tanzania Bara kwa              njia ya simu za mkononi 
        Mshauri wa Twaweza, Profesa Kitila              Mkumbo anasema asilimia 63 ya waliohojiwa walisema wanataka              watoto wao wafundishwe kwa lugha ya Kiingereza katika shule              za msingi na sekondari.
        Anasema wazazi wa watoto walio              shule za msingi walisema kubadili lugha kutoka Kiswahili              kwenda Kiingereza kutaleta matatizo. Anasema asilimia 89 ya              wazazi hao walikubali kuwa kuna changamoto, huku asilimia 10              wakisema hakuna matatizo.
        Walipoulizwa kuhusu ubora wa elimu              ya msingi, anasema asilimia 64 ya wazazi walisema uko              vizuri; asilimia 62 ya wazazi wenye elimu ya sekondari              walisema iko vizuri na asilimia 50 ya wenye elimu ya juu              walisema elimu ya msingi ni nzuri.
        "Hapa utagundua kuwa elimu              aliyonayo mzazi pia inasaidia katika kufanya uamuzi sahihi.              Hiyo asilimia 64 waliyosema elimu ya msingi ni nzuri, wao              pia wana elimu hiyo, kwa hiyo wengi wao pia hawana ujuzi wa              upeo mkubwa," anasema.
        Profesa Mkumbo anasema matarajio              ya wazazi hao pia yalikuwa tofauti. Wazazi wengi walitaka              watoto wao wafanye kazi za udaktari na ualimu. Asilimia              mbili tu walisema wangependa kuona watoto wao wakijikita              kwenye kilimo ambacho wengi wanakitegemea.
        Mkurugenzi wa ukaguzi na udhibiti              wa shule nchini, Marystella Wasena anakiri kuwa kuna shida              kubwa katika kuchagua lugha ya kufundishia. Anasema mtu              akitumia lugha ambayo haijui vizuri atashindwa kujiamini na              kufanya jambo la maana.
        Anasema ni jukumu la kila              Mtanzania kutafakari namna ya kulitoa Taifa katika              mkanganyiko uliopo. Wasena anasema lengo kuu ni kumpatia              mwanafunzi elimu ambayo itakuwa na athari chanya kwenye              jamii anayotoka.
        "Inawezekana mitalaa yetu iko              vizuri lakini namna inavyotolewa ikawa ndiyo tatizo. Sera ya              elimu ni nyumbufu, imetoa uhuru wa kutumia lugha ya              Kiswahili au Kiingereza kama lugha ya kufundishia,"              anabainisha mkurugenzi huyo.
        Wasena anasisitiza kuwa watu              wasiangalie matumizi ya lugha ya Kiswahili pekee, bali              waonyeshe na upungufu mwingine kama vile mitalaa, namna              elimu inavyotolewa, miundombinu ya shule au nyenzo za              kufundishia.
        "Miaka mitano iliyopita ufaulu wa              somo la Kiswahili haukuwa mzuri licha ya kuwa Kiswahili ni              lugha inayozungumzwa. Kwa hiyo, lugha isiwe hoja sana, kuna              haja ya kuangalia mfumo mzima wa elimu yetu," anasema              Wasena.
        Maoni ya wadau
        Wadau mbalimbali wa elimu wanasema              Serikali pia ina wajibu wa kufanya utafiti ili kubaini lugha              inayofaa katika kufundishia watoto. Wanasema lugha ni nyenzo              ya kukuza uchumi wa kuleta maendeleo ya Taifa.
        Aliyekuwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu              wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Uttoh anasema hakuna              namna yoyote nchi hii inaweza kukwepa kuwa nchi inayotumia              lugha mbili.
        Uttoh anasema siyo rahisi kutoka              kwenye lugha ya Kiswahili na kwenda moja kwa moja kwenye              lugha ya Kiingereza. Anaongeza kuwa lazima maandalizi              yafanyike ikiwemo kuwaandaa walimu, kuandaa mitalaa na              vitendea kazi.
        "Sera ya elimu iko very clear              (wazi), inatoa uhuru wa kutumia lugha zote mbili kwa wakati              mmoja. Hata nchi nyingine pia zinafanya hivyo, kwa hiyo              tusiibeze sera ya elimu, jambo la msingi ni kusimamia utoaji              wa elimu hii," anasema.
        Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha              (Rucu), Gaudence Mpangala anasema Tanzania haiwezi kuepuka              lugha ya Kiingereza kama inataka maendeleo ya haraka.              Anasema lugha ya kufundishia imeligharimu Taifa hili kwa              kuzalisha vijana ambao hawawezi kuchamgamana na wenzao wa              nchi nyingine.
         "Sera ya elimu nayo ni mbovu.              Ilitakiwa iweke wazi lugha moja ya kufundishia kwa shule              zote Tanzania badala ya kutoa uhuru kwa shule kuchagua              zenyewe lugha ya kufundishia," anafafanua mwanazuoni huyo.
        Mwanafunzi aliyeingia kwenye kumi              bora ya matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, Kelvin Fidelis              anasema lugha ya Kiingereza inafaa kufundishia shule za              msingi kwa sababu itawajengea wanafunzi msingi mzuri              wanapokwenda sekondari.
        "Wanafunzi wengi wanapata shida              wanapoingia kidato cha kwanza na kukuta lugha ya Kiingereza              ambayo hawaijui. Mimi nilisoma shule inayotumia lugha ya              Kiingereza, sikupata shida, lakini wapo wenzangu ambao              walikuwa wanachukua muda mrefu kuelewa," anasema.
        Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya              Lukangao, Innes Tawata anasema huu ni wakati wa sayansi na              teknolojia na dunia imekuwa kama kijiji, kwa hiyo lugha ya              Kiingereza inatakiwa kufundishwa kikamilifu bila kukitupa              Kiswahili.
        "Siku hizi ukienda kwenye usaili               unaambiwa lazima ujue kuongea Kiingereza. Kwa mfumo huu              Taifa letu linazalisha nguvu kazi ambayo haiwezi kukidhi              mahitaji ya soko la ajira," anasema mwalimu huyo.
        Utafiti umefanyika, wadau              wamezungumza; sasa ni wakati wa Serikali kusikiliza hoja za              wananchi na kufanya utafiti wake ili iweze kufanya uamuzi              sahihi katika kujibu swali ambalo pengine majibu yake ya              sasa hayaridhishi.
        
0 comments:
Post a Comment