WAMAREKANI wawili wenye asili ya Afrika wamepigwa risasi na polisi katika maandamano ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa kwa mvulana mweusi huko Ferguson, Missouri nchini Marekani.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mtu mwingine amejeruhiwa vibaya katika ghasia hizo baada ya ufyatulianaji risasi uliotokea katika dakika za mwisho za maandamano hayo ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuuawa kwa Mmarekani mweusi Michael Brown na polisi mwaka uliopita.
Mauaji ya Michael Brown yalisababisha mtafaruku baina ya watu wa jamii ya Wamarekani weusi na polisi nchini Marekani.
Polisi wanasema kuwa mtu huyo aliyejeruhiwa alikuwa akisakwa na polisi kwa kipindi kirefu baada ya kupokea habari kuwa alikuwa amejihami kwa bunduki iliyoibwa.
Hata hivyo taharuki imetanda mjini Ferguson baada ya video kuibuka ikionesha polisi wakimpiga risasi Mmarekani mwenye asili ya Afrika.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, jina la mwathirika huyo halijajulikana kwa sasa.
Mkuu wa polisi katika jimbo hilo la Ferguson, Jon Belmar amesema kuwa tayari maofisa 4 wa polisi wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa kina kuhusu kisa hicho.
Picha kadhaa kutoka eneo lilipotokea tukio hilo zilimuonesha mtu mweusi anayetokwa na damu akiwa amelala sakafuni.
Awali, mamia ya watu walisimama kimya kwa muda wa dakika nne na nusu kwa pamoja mjini Ferguson katika sehemu ile ile ambayo kijana Michael Brown aliuawa na polisi wa Kizungu mwaka mmoja uliopita.
Mauaji hayo yalileta mjadala dhidi ya ubaguzi wa polisi nchini Marekani na ulimwenguni kote
0 comments:
Post a Comment