WAZIRI wa Nishati na Madini, George Simbachawene amesema zipo dalili njema za kugundua gesi katika maeneo mengine nchini baada ya kugundulika kwa gesi asilia futi za ujazo trilioni 55.08 katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.
Simbachawene alitaja maeneo ambayo yameonesha dalili ya kuwepo gesi asilia mbali na mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa ni Morogoro na Pangani . Alisema hayo hivi karibuni Makao Makuu ya Wizara, wakati akitoa nyaraka za ufadhili wa masomo kwa Watanzania 22 waliopata ufadhili kusomea masuala ya mafuta na gesi katika ngazi za Shahada za Uzamivu na Uzamili , nchini China.
Alisema kuwa, uwepo wa gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na dalili ambazo zimeonekana katika maeneo mengine ni kiashiria kuwa, Tanzania inaingia katika uchumi wa gesi . Alisema taifa linatarajiwa kunufaika na rasilimali hiyo kwa kuwa kiwango kilichopatikana ni kikubwa cha kuifanya nchi kupiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia rasilimali hiyo.
"Kuna nchi zina gesi futi za ujazo 10 tu lakini wamepiga hatua kubwa ya maendeleo kupitia gesi asilia. Kwa kiasi tulichonacho na ambacho tunaendelea kugundua ni wazi kuwa tunaingia katika uchumi wa gesi na ndio sababu tumeanza kutayarisha wataalamu wetu wenyewe," aliongeza Simbachawene.
Akizungumzia Sheria zilizosainiwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, alisema zinaondoa wasiwasi wa namna taifa litakavyonufaika na rasilimali hiyo. Sheria hizo ni Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia, Uwazi na Uwajibikaji na Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi Asilia
0 comments:
Post a Comment