August 27, 2015

  • NEC yashtuka


    NEC yashtuka
    UENDESHAJI wa kampeni za urais zilizoanza hivi karibuni umeishtua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) hivyo kutoa angalizo kwa vyama kuhakikishia vinazingatia kanuni na sheria.
    NEC imevitaka vyama vya siasa kuzingatia ratiba ya kampeni kwa kuepuka kufanya mkusanyiko wa aina yoyote usio katika ratiba ya kampeni za urais.
    Katika taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima, amesema hivi karibuni kumejitokeza baadhi ya vyama vya siasa vinavyoanza mikusanyiko yenye sura ya kampeni ambayo haipo katika ratiba ya kampeni za urais.
    Kailima katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema mikusanyiko hiyo yenye sura ya kampeni, inaweza kuingiliana na ratiba za kampeni za vyama vingine katika maeneo husika na kusababisha uvunjifu wa amani.
    Alisema, iwapo chama cha siasa kinataka kufanya mikusanyiko yenye sura ya kampeni za uchaguzi, kinapaswa kuwasilisha mapendekezo yake kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi aitishe kamati ya ratiba ya kampeni ya rais inayojumuisha vyama vyenye wagombea wa kiti cha urais ambavyo kwa mujibu wa kanuni vinaweza kukubali au kukataa mapendekezo hayo.
    Aidha, ilisema katika maadili ya uchaguzi ya mwaka 2015 yaliyokubaliwa na kusainiwa na vyama vyote vya siasa, Julai 27, vyama vyote vya siasa vilikubali kuheshimu na kutekeleza maadili hayo na ukiukwaji wowote wa maadili hayo utashughulikiwa kwa mujibu wa kipengele cha 5.11 cha maadili hayo.
    Alisema chama kitakachokiuka maelezo hayo kitakuwa kimekiuka kipengele cha 2.1(a) cha maadili kinachoeleza wajibu wa vyama vya siasa na wagombea kuheshimu na kutekeleza sheria za uchaguzi.
    Alivitaka vyama vyote vya siasa kuzingatia ratiba ya kampeni ya uchaguzi wa rais kwa kufanya mikutano kwa tarehe, sehemu na mahala kwa mujibu wa ratiba.
    Hivi karibuni, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alifanya ziara kwenye maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa kile alichoeleza ni kwenda kushuhudia kero za wananchi. Hata hivyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilipiga marufuku ziara hizo kwa kile ilichoeleza ni sababu za kiusalama.
    Kampeni hospitalini
    Wakati huo huo, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana imepiga marufuku hospitali na vituo vingine vya kutolea huduma za afya kutumika kuendeshea shughuli za kisiasa.
    Wizara imesema itakapoonekana kuwa baadhi ya wagombea wa nafasi za uongozi wana haja ya kutembelea hospitali kwa madhumuni tofauti na yale ya kuwajulia wagonjwa hali zao, itabidi waombe kibali maalumu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
    Taarifa iliyotolewa jana na wizara imesema kwa mujibu wa taratibu na miongozo ya huduma za afya, hospitali ni sehemu inayopokea na kulaza wagonjwa wenye matatizo mbalimbali ya muda mrefu na muda mfupi na wanahitaji kuendelea kupata huduma katika mazingira ya amani na utulivu.
    Onyo hilo la Serikali limekuja siku chache baada ya mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan kutembelea vituo vya afya vya Huruma katika wodi ya wazazi na Hedaru.
    Habari hii imeandikwa na Lucy Lyatuu na Sophia Mwambe


  • 0 comments:

    Post a Comment

    Copyright @ 2013 Michapo | Kisiwa cha Habari.